Na Mwandishi Wetu, JAMHURI MEDIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara hususan mnpakani mwa Tanzania na Malawi ili wananchi waweze kunufaika na biashara zao.
Rais Samia ameyasema hayo kabla ya kuhitimisha ziara yake ya Kiserikali ya siku 3 nchini Malawi, ambapo pia amehudhuria sherehe za miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ziara yake nchini Malawi kwenye Mkutano uliofanyika Blantyre nchini humo tarehe 7 Julai, 2023.


Kwa pamoja, Rais Samia na Rais wa Malawi Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wamewataka mawaziri husika kukaa chini na kutafakari namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara ili maono ya Serikali zote mbili yaweze kufikiwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Malawi Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wakati wakishuhudia utiaji Saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Malawi kuhusiana na mashirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mara baada ya mazungumzo yao Lilongwe nchini Malawi tarehe 7 Julai, 2023. Aliyeketi (kulia) ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye wakisaini Mkataba huo pamoja na Waziri wa Habari na TEHAMA wa Malawi Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa wa kwanza (kushoto)


Rais Samia pia ameshuhudia utiaji saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Malawi kuhusiana
na na mashirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA).
Katika mkataba huo, upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye pamoja na Waziri wa Habari na TEHAMA wa Malawi Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Malawi Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera kwenye picha ya kumbukumbu na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye pamoja na Waziri wa Habari na TEHMA wa Malawi Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa mara baada ya kushuhudia utiaji saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusiana na mashirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Lilongwe nchini Malawi tarehe 7 Julai, 2023.


Vile vile Rais Samia ameipongeza Malawi kwa kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika shule zake na kusisitiza kwamba lugha hiyo ndio itakayowaunganisha Waafrika.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ametembelea eneo la Kapeni view point Blantyre na kujionea athari zilizotokana na kimbunga Freddy ambapo watu wengi walipoteza maisha, mali na makazi.