●NIRC yasaini mikataba ya ununuzi mitambo ya kuchimba vidima virefu nchiniI
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, imesaini mkataba wa ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima virefu na kampuni ya utengenezaji mitambo hiyo ya Uturuki iitwayo Acarkardesler, ambapo mitambo hiyo itagharimu Dola za Kimarekani 2,821,028.
Akizungumza wakati ya utiaji saini wa makubaliano hayo Mkurugenzi Mkuu Tume yaa Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, amesema mitambo hiyo inatarajia kuwasili nchini ndani ya miezi miwili na kisha kuanza kazi.
Mndolwa amesema lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha sekta ya kilimo cha Umwagiliaji inakua nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa.
Pia ametia saini mkataba na kampuni ya Garnite Co. Limited kwa ajili ya ununuzi wa mitambo aina nya Support Trucks, inayotumika kubeba vifaa vya uchimbaji visima, ambayo imegharimu thamani ya shilingi bilioni 4,330,600,000; na kwamba mitambo hiyo pia inatarajiwa kuwasili mwezi wa sita mwaka huu
“ Mitambo hiyo itatumika kuchimba visima 67,500 katika halmashauri 184 kwa kipindi cha miaka nane ambapo mradi huo wa visima utakuwa na wanufaika wa moja kwa moja zaidi ya 100,000 hususani vijana na wanawake katika maeneo ya vijijini huku eneo litakalomwagiliwa ni wastani wa ekari 2.5 kwa kila mkulima,”amesema.
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa mwaka huu wa fedha itachimba visima 1,300 ambapo kati ya hivyo visima 70 vitakavyohudumia mikoa 16 ikiwemo Pwani, Tanga, Mara, Songwe, Singida, Manyara, Dodoma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita, Morogoro, Simiyu, Ruvuma na Njombe vitachimbwa na wakandarasi na visima vinavyobaki vitachimbwa kupitia mitambo inayonunuliwa.