Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani ameshuhudia utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa reli ya SGR kipande cha Tabora-Kigoma kati ya Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania TRC na kampuni za ubia za China Civil Engneering Corporation CECC na China Railways Construction Corporation CRCC.
Utiaji Saini huo umefanyika leo Desemba 20, 2022 katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es salaam ambapo Rais samia amesema serikali itaendelea kujenga miradi ya kimkakati kama SGR ili kukuza uchumi.
“Ndugu wananchi, serikali kwa upande wake itaendelea kujenga miradi hii ya kimkakati ili kuendelea kukuza uchumi. Uwekezaji unakwenda pande zote, kwenye SGR pia tunafufua reli za zamani ili kuunganisha bandari zote na reli zote.” Amesema Rais Samia
Rais Samia amesema lengo la serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji, kutokana na kuwa mahali pazuri kijografia ikipakana na nchi nane katika ukanda wake jambo ambalo ni fursa kibiashara.
“Lengo la serikali ni kufanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara. Nawataka wote wanaohusika na usimamanizi wa ujenzi wa miradi hii kufanya wajibu wao kama inavyotakiwa.”Amesema Rais Samia
“Tanzania tumewekwa pahali pazuri na Mwenyezi Mungu, tuna bahari, maziwa makubwa, mito na nchi yetu inapakana na nchi nane. Nataka kusisitiza kwamba fursa hii haiwezi kunufaisha taifa kama hatutaitumia vyema. Tutumie fursa yety hii kijografia.”Amesema Rais Samia
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa amesema, utiaji Saini huo unafanya utimilifu wa reli ya kati, kutoka Dar- Mwanza na ile ya Dar-Kigoma,na reli hiyo kutoka Tabora-Kigoma itakuwa na kilomita 506 ukigharimu dola za kimarekani Bilioni 2.7 sawa na Shilingi Trilioni 6.34 ukitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 48
“Utiaji Saini huu wa leo unafanya utimilifu wa reli ya kati, kutoka Dar- Mwanza na Dar-Kigoma, kwingine kote kutakapofuata ni reli za matawi”Amesema Kadogosa.
“Ujenzi wa Tabora-Kigoma una kilometa 506, tutakuwa na station 10, vituo vikubwa vya miziko Uvinza na Katosho.Thamani ya mkataba ni Dola bilioni 2.21 bila kodi, ukijumuisha kodi inakuwa Dola bilioni 2.7 sawa na Tsh. Trilioni 6.34 na ujenzi huu unatarajiwa kutuchukua miezi 48.”Amesema Kadogosa
Aidha Kadogosa amesema kuwa TRC itashirikiana na TANESCO kujenga line ya umeme wa kujitegemea ambayo haitaingilia line yoyote ili kupata umeme wa uhakika.
“Pamoja na ujenzi wa miundombinu, TRC kwa kushirikiana na TANESCO tunajenga line ya umeme wa kujitegemea, kwa maana tutakuwa na line ya kwetu haitaingiliana na line yoyote kwa ajili ya kupata umeme wa uhakika.”Amesema Kadogosa
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla akizungumza katika hafla hiyo amempongeza Rais samia kwa ujenzi wa SGR na kwamba anayoyafanya Rais Samia yapo kwewnye liani ya Chama Cha Mapinduzi.
“Unayoyafanya yameandikwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, chama cha siasa kazi yake ni kushika dola, unayoyafanya unatekeleza kile kilichopo kwenye ilani.”Amesema Makalla
Vilevila Makala ameongelea swala la upinzani kuwa na Bunge la Mtandao na kusema kuwa wanafanya mchezo
“Ukishaona mtu mzima anacheza michezo ya kitoto kwa mfano ‘hide and see’ au kujipikilisha ujue mambo sio mazuri, juzi tumesikia wenzetu wanachagua Bunge la Mtandao, linaitwa Bunge na lina Spika, sasa hapo tunaona kabisa wanacheza mchezo wa hide and see, wamechanganyikiwa, hii ni kutokana na kazi nzuri unayofanya.”Amesema Makalla