Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameidhinisha miswada ya sheria minne ili iweze kuwa sheria.
Akilitaraifu Bunge la 12 Mkutano wa 15 mjini Dodoma leo , Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema katika mkutano wa kumi na nne wabunge walipitishwa miswada minne ya sheria, ambayo sasa imepata kibali rasmi kwa Rais Samia ili ianze kutumika kwa mujibu wa sheria.
Miswada hiyo ni pamoja na Mswada wa Sheria wa Uchaguzi wa Rais na Madiwani ya mwaka 2023, Mswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi 2023, Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2023 na Mswada wa Sheria ya Marekebisho mbalimbali ya mwaka 2023.
“Kwa taarifa hii napenda kulitaarifu bunge hili tukufu kuwa tayari miswada hiyo minne imeshapata kibali cha Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na kuwa sheria za nchi,” amesema Spika wa Bunge.
Kwa sasa sheria hizo zitaitwa: Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024, Sheria ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi namba 2 ya mwaka 2024,Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa namba 3 ya mwaka 2024 na Sheria ya Marekebisho mbalimbali ya Sheria namba 4 ya mwaka 2024.