Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kwa kazi nzuri ya uwakilishi ambayo inaonekana kwa kuongezeka kwa masoko ya bidhaa za Tanzania, biashara, uwekezaji, utalii na tekbolojia nchini.
Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Aprili 22, 2024 alipokuwa anawahutubia mabalozi hao kwa njia ya mtandao ambao wamekusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya siku 4 ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje iliyoanza Aprili 21 na itakamilika Aprili 24, 2024.
Mhe. Rais Samia amesema kuwa nchi inawategemea sana Mabalozi katika utekelezaji wa majukumu yao Ili iweze kusonga mbele kiuchumi na kwa kuliona hilo, Rais Samia amesema amechukua hatua mbalimbali ili kuibadilisha Wizara ya Mambo ya Nje iwe ya kisasa zaidi na kuwa na uwezo wa kuitangaza nchi.
Lengo la Mabadiliko hayo ni kuifanya nchi iendelee kuheshimika na kuwa na ushawishi zaidi duniani kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma ya wakati wa harakati za ukombozi na baada ya ukombozi.
Hatua ambazo Mhe. Rais Samia alizitaja kuwa ni pamoja na kuteua Naibu Waziri na Katibu Mkuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, kuanzisha Idara ya Diplomasia ya Uchumi, kusaini mikataba ya Kuzuia Utozaji wa Kodi mara Mbili na Kulinda Vitega Uchumi na nchi mbalimbali duniani, kuridhia mkakati wa uendelezaji wa majengo ya ofisi za Mabalozi na makazi na mchakato wa uboreshaji wa Sera ya Mambo ya Nje na Hadhi Maalum kwa raia wenye asili ya Tanzania wanaoishi Nje ya nchi ambao umefikia hatua nzuri.
Mhe. Rais aliwasihi Mabalozi kuwa jicho la Tanzania kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili nchi isipitwe na Mabadiliko makubwa yanayotokea duniani.
Mhe. Rais pia alizungumzia misingi sita ya Sera ya Mambo ya Nje ambayo Nchi yetu inaisimamia tangu ilipopata uhuru na kutufikisha hapa tulipo. Aliitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na kulinda uhuru wa kujiamulia, kuheshimu mipaka ya nchi; kulinda uhuru, haki za binadamu na usawa wa kidemokrasia; kudumisha ujirani mwema; kuunga mkono Umoja wa Mataifa, kuendeleza mshikamano wa Umoja wa Afrika na kuunga mkono Sera ya kutofungana na Upande Wowote.
Rais Samia aliwambia Mabalozi katika Maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje yanayoendelea, amependekeza kuongeza msingi wa saba ambao ni kulinda maslahi ya kiuchumi na maadili ya watu. Katika msingi huu, Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi yetu na Utamaduni wake. Alisema nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo madini hadimu. Alisema endapo nchi haitakuwa na mpango madhubuti wa kulinda rasilimali hizo na kunufaifika nazo, basi badala ya kuwa fursa kwa Taifa zinaweza kugeuka na kuwa janga.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda Utamaduni wetu kwani kuna juhudi za makusudi zinaxoendelea duniani za kulazimishwa tamaduni zilizo kinyume na maadili yetu.
Mhe. Rais Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha Mabalozi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pande mbili, Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo katika majukumu yao ya uwakilishi, wakumbuke vipaumbele vya Zanzibar, hususan kukuza utalii na uchumi wa buluu.