Na Munir Shemweta,JamhuriMedia, Mwanza

Katika kinachoonekana kuwajali wananchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameridhia msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi la pango la ardhi ya shilingi Bilioni 21.3 kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.

Kufuatia msamaha huo, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 31.5 kama deni la msingi la msamaha wa riba uliotolewa na Rais.

Awali Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alitoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi la pango la ardhi kuanzia mwezi julai hadi Desemba 31, 2022 kabla ya kuongeza muda ambapo sasa msamaha huo unaishia April 30, 2023.

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango akizungmza na wananchi wa Buswelu mkoani Mwanza wakati wa ziara yake tarehe 12 April 2023.

‘’Nimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuridhia msamaha wa riba ya shilingi bilioni 21.3 ambapo wamiliki waliosamehewa wanaendelea na maisha yao na hizo fedha zitawasaidia kwa shughuli nyingine kwa hiyo wamelipa deni la msingi na ile riba wamesamehewa’’ amesema Dkt Mabula.

Hayo yamebainishwa tarehe 12 April 2023 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango mkoani Mwanza aliposimama kwa muda kata ya Buswelu manispaa ya Ilemela.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hadi kufikia tarehe 12 April 2023 jumla ya wamiliki wa ardhi 8,726 wamenufaika na msamaha huo huku akianisha mkoa wa Mwanza kuwa na idadi kubwa ya watu waliotumia fursa ya msamaha huo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika eneo la Buswelu Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango mkoani humo tarehe 12 April 2023.

Aidha, Dkt Mabula amesema wizara yake kwa sasa inakwenda kufungua mifumo yote aliyoieleza kuwa haikuwa rafiki kwa Tanzania ambapo tayari ramani za ardhi pamoja na zile za mipango miji zimebadilishwa kwa asilimia mia moja kutoka analogia kwenda digitali.

Pia alieleza kuwa, wizara yake imeajiri kwa muda vijana wapatao 26 kwa lengo la kubadilisha mifumo itakayomuwezesha kila mtanzania kupata taarifa zake za ardhi hususan zile za kodi ya pango la ardhi kupitia simu yake ya mkononi ili kuwaepusha wananchi kufuatilia madeni yao wizarani ama ofisi za ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mpaka kufikia tarehe 12 April 2023 mikoa 12 taarifa zake zimeingizwa katika mfumo ambapo wamiliki wake wataanza kupata bili zao kupitia simu ya kiganjani.

Vile vile, Dkt Mabula alimshukuru Rais Samia kwa kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi huku akianisha manispaa ya Ilemela kuwa moja ya halmashauri zilizonufaika na fedha hizo iliyopatiwa jumla ya shilingi bilioni 3.589 ambapo viwanja vimepimwa na wananchi wameanza kununua kwa uwazi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Naibu Waziri TAMISEMI Deo Ndejembi katika eneo la Buswelu wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango mkoani humo tarehe 12 April 2023. Kulia ni Waziri wa Maji Jumaa Awesu.