Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Shinyanga
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya ya jamii na kutoa fursa kwa wadau na mashirika kutoa huduma katika mikoa mbalimbali.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ambapo amebainisha kuwa Mkoa huo ni miongoni mwa Mikoa iliyonufaika sana.
Amesema kuwa maboresho makubwa ya miundombinu ya utoaji huduma za afya katika Mkoa huo na Mikoa mingine nchini yametoa fursa kwa washirika wa maendeleo kufanya shughuli zao kwa weledi mkubwa.
Amepongeza Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wake wa Afya Hatua kwa kushirikiana na Afya Plus na Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani cha CDC (The US Center for Disease Control) kwa kufanikisha huduma ya tohara kinga ya hiari kwa wanaume Mkoani humo.
Dkt Ndungile amebainisha kuwa mradi huo ambao unatekelezwa na Shirika hilo kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na ukimwi PEPFAR (The US President’s Emergency Plan for AIDS Relief) hadi sasa umenufaisha wanaume zaidi ya 25,000.
Amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa katika Mikoa ya Kigoma na Shinyanga kuanzia Nov 2021 hadi 2026 umelenga kupunguza maambukizi ya VVU kwa watu wazima wakiwemo wanaume katika Mikoa hiyo kupitia huduma ya tohara kinga.
‘Hadi sasa mradi huu umefikia jumla ya wanaume 26,752 wenye umri wa miaka 15 na kuendelea katika robo ya kwanza tu ya mwaka wa tatu wa mradi (2023/2024) ikiwa ni asilimia 29 ya lengo la kufikia wanaume 91,022’, alisema.
Amesisitiza kuwa mradi huu umekuwa na mwitikio mkubwa sana wa wanaume kupata huduma ya tohara, hivyo akawataka kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma katika vituo 35 vilivyoanishwa ili kudhibiti maambukuzi ya VVU.
Dkt Ndungile ameongeza kuwa pia wameendelea kutoa elimu ya magonjwa ya zinaa ambayo huambukizwa kupitia via vya uzazi na elimu ya ukatili wa kijinsia kutokana na Mkoa huo kuwa na matukio mengi ya namna hiyo.
Meneja wa mradi wa Afya Hatua Mkoani hapa Dkt. Amos Scott amesema kuwa THPS kupitia mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua imesaidia upatikanaji wa huduma za tohara kinga ya hiari kwa wanaume (VMMC) kama moja ya afua za kuzuia maambukizi ya VVU katika mikoa hiyo.
Amebainisha kuwa THPS kwa kushiriana na mradi wa Afya Plus wanaendelea kutekeleza huduma za tohara kinga katika halmashauri zote 6 za Mkoa huo ili kuongeza ubora na usalama wa utoaji huduma hizo kwa wanaume na vijana.
Dkt Scott amebainisha kuwa mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua ulioanza kutekelezwa nchini Oktoba 2021 hadi Septemba 2026 unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya vya Mikoa ya Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Ameongeza kuwa huduma hizo ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za tohara kinga kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wa mkoa wa Shinyanga.
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoani hapa Dkt. Peter Mlacha amesema kuwa tohara kinga imesaidia sana kupunguza maambukizi ya VVU kwa wanaume na kuachana na imani potovu dhidi ya tohara.