Na Stella Aron, JamhuriMedia, Zimbabwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili kwenye uwanja wa ndege wa Robert Mugabe jijini Harare nchini Zimbabwe na ndege ya Shirika la Ndege la ATCL kuhudhuria Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika Agosti 17, 2024 jijini humo.

Rais Mhe. Dkt. Samia amepokelewa kwenye uwanja huo majira ya saa kumi na mbili kasoro robo kwa saa za Zimbabwe kwa gwaride maalum la kijeshi la ukaribisho lililoandaliwa kwa ajili yake.

Miongoni mwa viongozi waliokuwepo uwanjani hapo kumpokea Rais Dkt. Samia ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Thabit Kombo na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Balozi Saimon Sirro.

Mkutano huo wa 44 wa SADC utatanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Troika chini ya Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais Haikande Hichilema wa Zambia anayekabidhi uenyekiti huo itakutana kesho Agosti 16 kumteua Rais Dkt. Samia kuwa Mwenyekiti mpya wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ on Politics, Defence and Security Cooperation)

Rais Dkt. Samia atashika uenyekiti huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na atapokea kutoka kwa Rais wa Zambia
Mhe. Hakainde Hichilema aliyemaliza kipindi chake cha uenyekiti cha mwaka mmoja.

Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC.

Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025

Please follow and like us:
Pin Share