Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa kuongeza saa 24 za uokoaji katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo.
Rais Dkt. Samia ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza kwa njia ya simu na Mhe. Majaliwa kuhusiana na zoezi la uokoaji na kusema:
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalum wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuweza kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo. Ninakupa maelekezo ya kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi ili kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai “
Aidha, Rais Dkt. Samia pia ameongeza kusema kuwa:
“Kwa vikosi vyetu vyote na wananchi wote wanaopambana kuokoa maisha ya ndugu zetu katika zoezi hilo ninaomba ufikishe salamu zangu na uwaeleze kuwa natambua na nina wathamini sana. Wameonyesha utu, uzalendo mkubwa na uchapakazi wa hali ya juu sana. Hivyo nawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania ndugu zetu kwani ninyi ni mashujaa wa taifa letu”
Rais Dkt. Samia anawaombea kwa Mungu awalinde na kuwapa nguvu muda wote wakiwa wanateleleza jukumu hilo kubwa na la kizalendo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amewasihi wananchi, ndugu na jamaa kuendelea kuwa na subira na kama taifa tuendelee kuwaombea ndugu zetu na wapiganaji wetu ili tufanikishe zoezi hili kwa mafanikio makubwa.
Mwenyezi Mungu tunakuomba utufanyie wepesi kwenye zoezi hili. Amin
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu