Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo wanaanza kikao chao cha siku mbili ambacho pamoja na mambo mengine watakupiga kura ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Nafasi hiyo iliachwa wazi na Abdulrahman Kinana aliyeandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Julai, mwaka jana.
Mbali na kujaza nafasi hiyo, pia mkutano mkuu huo utakuwa na kazi ya kupokea taarifa ya chama kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 na kupokea taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Mkutano huo umetanguliwa na vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ambavyo vimefanyika Ikulu ya Chamwino na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama, Rais Samia Suluhu Hassan.