Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Aidha Sherehe hizo ziliwakutanisha wanachama, wakereketwa, na wapenzi wa CCM kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Samia amewataka wanachama wa chama hicho kutojivunia tu uimara wa CCM, bali pia kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujitolea ili kuhakikisha chama kinakua na kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.
Ameweka wazi kuwa CCM imejipanga vema katika kuhakikisha kuwa inapata wagombea bora na wanaokubalika katika uchaguzi ujao, ili kuhakikisha ushindi katika nafasi za udiwani, ubunge, na urais.
Rais Samia amesisitiza kuwa mwelekeo wa chama chake na mustakabali wake unategemea uwezo wake katika kutatua changamoto za wananchi kwa wakati, huku akielezea umuhimu wa CCM kuendelea kubaini matatizo yanayowakabili wananchi na kuleta suluhu za haraka.
Ameeleza kuwa, kama sehemu ya jitihada za kuboresha maisha ya wananchi, Serikali itaendelea kutoa ajira kwa vijana na kuhakikisha kuwa wanapata fursa za kujiajiri na kukuza uchumi wa taifa.
Pia, Rais Samia amezungumzia umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika siasa na ushawishi wa chama.
Amesema kuwa CCM ina wanachama zaidi ya milioni 12 na wapenzi wengi, na hivyo ni muhimu kwa viongozi wa chama kuhakikisha wanawafikia wananchi kwa njia za kisasa(Tehema).
Pamoja na hayo amefafanua kuwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ni muhimu katika kuwasiliana kwa haraka, kutoa taarifa, na kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi kwa ufanisi.
Rais Samia amewahimiza wanachama wa CCM kutembeleana na kushirikiana ili kueleza mafanikio ya serikali kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa kipindi hiki cha uchaguzi ni muhimu kwa kila mwanachama kueleza mazuri yaliyofanywa na serikali chini ya uongozi wa CCM.