Geneva, Uswisi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameombwa kuwa miongoni mwa viongozi kinara katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu Duniani kufuatia utekelezaji bora wa afua zinazolenga kutokomeza ugonjwa huo hadi ifikapo 2030.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Stop TB Partinership Dkt Lucica Ditiu, yenye makao Makuu yake mjini Geneva Uswisi wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.
Awali akizungumza Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya Tanzania imepiga hatua katika kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu kutoka asilimia 49 mwaka 2016 hadi asilimia 65 mwaka 2022 na kusogeza huduma za uchunguzi wa Kifua Kikuu na tiba karibu na wananchi
Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika ugunduzi wa wagonjwa wapya wa Kifuu hususani kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile migodini.
Aidha ametoa taarifa kuwa Tanzania hupoteza takribani watu 70 kwa siku kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu.
“Mwezi Machi mwaka huu Serikali ilizindua Mpango unaoshirikisha sekta nyingine ili kuongeza kasi ya kutokomeza Kifua Kikuu kupitia sekta hizo kuweka kipaumbele katika masuala ya ugonjwa huo”, ameeleza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amemuahidi Dkt Ditiu kuwa atafikisha maombi hayo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samaia Suluhu Hassan kuwa yeye binafsi amekuwa mstari wa mbele nchini katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.
Lakini pia amesisitiza Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Stop TB partnership ili kuhakikisha ugonjwa wa Kifua Kikuu unatokomezwa kupitia utekelezaji wa miongozo na makubaliano ya kimataifa na kikanda
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Stop TB Partinership Dkt Lucica Ditiu ameipongeza Tanzania kwa kupunguza maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu.
Vile vile Dkt. Ditiu ametoa wito kwa Tanzania iwe moja ya nchi kinara barani Afrika katika jukwaa la Viongozi wakuu wa nchi 10 duniani wenye lengo la kutokomeza Ugonjwa huo ifikapo 2030.
Hata hivyo amesema wito huo umetokana na Tanzania kuonyesha ubunifu katika utoaji wa huduma za kinga na tiba pamoja na kufikia malengo ya viashiria vya kutokomeza ugonjwa huo.