Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Usiku wa kuamkia leo tumeshuhudia kishindo kikubwa katika siasa za Tanzania. Kishindo hiki kimetokana na kalamu ya Rais Samia Suluhu Hassan, juu ya ‘maamuzi magumu’ aliyoyafanya kwa mawaziri wanne.
Ametengua uteuzi wa mawaziri wawili; January Yusufu Makamba na Nape Moses Nnauye.
Hawa wawili nitawajadili kidogo. Pia nitamzungumzia Naibu Waziri aliyetenguliwa, Stephen Lujwahuka Byabato.
Makamba alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Nape alikuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Byabato alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hawa chumvi imetiwa kwenye kidonda. Nitawajadili kwa haki.
Rais pia amewateua Balozi Mahmoud Thabiti Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jerry Silaa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius John Ndejembi amekwenda kumrithi Silaa.
Ridhiwani Jakaya Kikwete ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Cosato David Chumi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye atapangiwa kituo cha kazi.
Deus Clement Sangu ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Dennis Lazaro Londo ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Rais Samia amemteua Eliakim Chacha Maswi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Huyu alipata kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, ndiye aliyeanzisha mabadiliko makubwa TANESCO kwa kuondoa rushwa na ugoigoi, japo alipata ajali ya kisiasa.
Kabla ya uteuzi huu Maswi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Ni mchapa kazi.
Sitanii, kwa kuwa makala hii ni ya uchambuzi, mnisamehe wengine ambao mmeteuliwa sijawataja, kwani ninaaminni tayari majina yenu yamekwishasomeka pakubwa.
Yanipasa kuwajadili angalau mawaziri watatu waliotenguliwa. Jambo moja niliseme kwa kutumia maneno ya Mwalimu Julius Nyerere; “Ulevi wa madarakani ni jambo baya sana.”
Ijulikane na ifahamike kuwa muda wowote, wakati wowote, Rais aliyeko madarakani ndiye ameshika mpini. Wengine wote katika serikali wanapaswa kufahamu kuwa wanapokea maelekezo kutoka kwake.
Na hata inapotokea mteule yupo sehemu yoyote, iwe ni kikazi au ziara binafsi, kichwani mwake anapaswa kufahamu kuwa chochote anachokitenda au anachokisema, kupitia yeye jamii na hadhira aliyopo inamwona Rais wake. Hili lifahamike kwa kina.
Nimepata fursa ya kuwasiliana na Nape baada ya kauli yake ya Bukoba. Ni wazi ameonekana kujutia matamshi yake juu ya njia za kupata ushindi katika uchaguzi na amewaomba radhi Watanzania.
Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi hali ya hewa ilishachafuka. Sura ya Rais Samia ilikwishawekwa rehani na kauli ile.
Ikumbukwe kuwa Nape anakumbukwa na Watanzania kwa kauli yake ya ‘Goli la Mkono’. Na kwamba Nape aliwaaminisha Watanzania kuwa akisema yeye, Rais Samia amesema.
Huku nje watu walikuwa wanatuletea taarifa kuwa yeye ni mmoja wa ‘watoto wa mama’. Kwa kivuli hiki, kauli ya Nape watu waliiona kuwa ni kauli ya Rais Samia.
Nikiri kuwa zipo nyakati tumefanya kazi pamoja na Nape, mimi kama Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF). Kuna nyakati Nape alitenda yaliyo mema nikafurahi na kumpongeza, lakini kuna nyakati nilishindwa kumtafsiri iwapo ni Nape yuleyule tuliyekuwa tunajadili pamoja vifungu vya mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake; tukawa na msimamo fulani, au ni Nape mwingine?
Nape alipata kupigania haki za wanahabari, tunamshukuru katika hili na tunamtakia kila la heri katika nafasi yake mpya ya ubunge pekee. Hata hivyo, hata kama alikuwa anafanya utani, hili sasa litufundishe kuwa kuna utani usiostahili kufanywa. Suala la uchaguzi, nchi yetu ina vidonda ambavyo bado vinavuja damu.
Watanzania wana kumbukumbu ya uchaguzi wa mwaka 2015, 2019 na 2020, ambao wengine wanadiriki kuuita ‘Uchafuzi’ na si Uchaguzi.
Kuna watu wapo bungeni leo kimwili, lakini kiakili wanafahamu kuwa uchaguzi wa mwaka 2025 bila kutumia polisi na watu wa hovyo wa kuiba kura, hawarejei bungeni. Huko majimboni wana migogoro na kila anayeonekana anaelekea kuwa mbunge mtarajiwa.
Wapo wawakilishi wa kweli wa wananachi wanaosubiri uchaguzi huru na wa haki waingie bungeni na wawe wawakilishi wa wananchi kupitia ama chama tawala au vyama vya upinzani.
Uchaguzi ni fursa ya kumpima mbunge iwapo anakubalika kwa wananchi na iwapo wananchi wanathamini na kuona kazi aliyowafanyia au hakufanya chochote.
Sitanii, sanduku la kura limewekwa kupima uwajibikaji wa viongozi wetu tuliowachagua. Nape kutamka kuwa zitatumika mbinu halali na haramu kumbakiza mbunge madarakani, amewakosea Watanzania.
Wabunge wanapaswa kutambua kuwa wao si wa kwanza na wala hawatakuwa wa mwisho kushikilia majimbo waliyonayo. Wajiulize kama watangulizi wao wasingeondoka, wao wangepataje ubunge?
Ubunge si ajira, ni kazi ya kuwakilisha watu. Kuwasemea. Ni bahati mbaya baadhi ya wabunge wameona ni haki yao kuwa wabunge milele, hata kama hawafanyi chochote.
Unapoanza kuwaza hivyo, unaona ni haki yako kushinda hata kama itakuwa ni kwa dhambi ya kuiba kura. Najiuliza, iwapo Nape alikuwa tayari kumsaidia Byabato kuiba kura, jimboni kwake anafanyaje?
Hofu kubwa zaidi, ni je, Nape anazifahamu hizi mbinu peke yake au ana mtandao? Na kama upo mtandao wa wizi wa kura, nchi hii inao akina Nape wangapi? Je, si itakuwa sahihi nikisema baadhi ya watu wanaingia madarakani kwa kuiba kura hivyo hawaoni kama wanawajibika kwa wapiga kura ndiyo maana hatupati hata maendeleo?
Leo, Rais Samia Suluhu Hassan amejitoa kimasomaso kutafuta fedha na kujenga barabara za vijijini na mijini. Hapigi kelele, na kama alivyosema, anazungumza kwa kalamu.
Hakika kwa mara nyingine tumemshuhudia akinena kwa kalamu usiku wa kuamkia Julai 22, 2024.
Ametengua mawaziri wawili walioaminika kuwa ni mibuyu. Mawaziri walioaminika kwa jamii kuwa Rais hasemi neno hadi ashauriane nao kwanza!
Jamii ilielekea kuaminishwa kuwa hata mbinu mbadala za kupata ushindi alizosema Nape, Rais Samia alishauriana naye kwanza kabla ya kutoa kauli hiyo!
Kwa hakika hii ni kutomtendea haki Rais Samia. Rais Samia ameitoa nchi shimoni. Kutoka enzi za watu kupotea, siasa kugeuka uwanja wa vita, mikutano ya hadhara kuzuiwa, fedha kuchukuliwa kwenye akaunti za watu bila taarifa na isivyo haki… akaja na 4R; Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga Upya.
Akaunda Kikosi Kazi cha Hali ya Siasa Nchini. Kikosi Kazi kikatoa mapendekezo muhimu, akayafanyia kazi kwa kutunga sheria tatu na kubadili Tume ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na mambo mengine mengi.
Sitanii, Samia ni Rais pekee aliyewahi kuhudhuria mkutano wa chama cha upinzani CHADEMA akiwa mgeni rasmi. Juhudi zote hizo, anafanya maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na kujenga upya, ila mtu mmoja anatoboa jahazi kwa kuwaaminisha Watanzania kuwa uchaguzi wa 2025 utakuwa kama wa 2020, ambapo msamiati wa ‘demokrasia’ ulikuwa umefutwa katika ‘Kamusi ya Tanzania’.
Nape hukutenda haki katika hili. Kwa nchi za wenzetu, ungepaswa kuchukua hatua moja mbele kuhusu ubunge wako kwa sura ya uwajibikaji na kuonyesha majuto. Nakushauri hili ulifikirie.
Byabato. Huyu naye chumvi imetiwa kwenye kidonda. Sijui kama anakubaliana na kauli ya Nape au aliipinga pale mkutanoni Kashai! Ila kwa vyovyote iwavyo, kwa siasa ninazozifahamu za Bukoba, hapa nimshauri kwa nia njema tu, kuwa mafao yake ya ubunge ayapangie mradi mzuri, awekeze. Kwa ubunge wa Bukoba Mjini; ni bora apite anaaga.
Najua hawakosekani watu wa kumtia moyo hewa, wakamwambia kuwa anakubalika, atatoboa. Mimi huwa ni muwazi. Byabato unafahamu mlango ulioingilia kwenye ubunge hapo Bukoba, sina uhakika kama mlango huo bado uko wazi.
Usiponisikiliza ukawa sawa na Rais Joe Biden wa Marekani wiki za kwanza alivyoshupaa ndani ya chama cha Democrat, majuto ni mjukuu.
Nakushauri tena, mafao yako ufungue mradi utakaosaidiana na uwakili wako, maisha yaendelee.
Sitanii, heri mimi ninayekushauri hadharani, maana najua kwa kukushauri hivi utaniongeza katika orodha ya watesi wako. Ukumbuke kilio ulichoangua pale stendi, Mradi wa Stendi uliotelekezwa Kyakailabwa, soko la Bukoba, barabara za baadhi ya mitaa kwa kata zote 14 za Jimbo la Bukoba, hasa zile 8 za Green Belt – Nyanga, Kagondo, Buhembe, Nshambya, Kahororo, Kibeta, Kitendaguro na Ijuganyondo.
Kata za katikati ya mji za Bakoba, Bilele, Hamugembe, Kashai, Miembeni na Rwamishenye, nazo wanalia hali ya usalama si shwari, wizi umezidi.
Kimsingi, najua hukosi marafiki wa kukwambia; “ni wewe tu!” Lakini usiponisikiliza mafao yako ukayaekeza katika kutafuta ubunge kipindi cha pili, utajuta.
Na kama huamini kauli yangu, wapigie simu Balozi Hamisi Kagasheki na Joseph Mujuni Kataraiya. Ni wana CCM wenzako, watakusaidia ushauri wa kichama.
Sitanii, January Makamba ameandaa anguko lake mwenyewe. Unapokuwa na Rais aliyeko madarakani, ni wazi unafahamu kuwa mwenye mamlaka yote ni mmoja tu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata usemi kwamba wewe unasubiri 2030, hukupaswa kuutoa kama ulikuwa unatania kweli. Inawezekana ile ya kuwa katika ‘tano bora’ mwaka 2015, ilikulevya.
Hukupata fursa ya kukaa chini ukabaini kuwa mpasuko wa Rais Jakaya Kikwete na hayati Edward Lowassa, ndiyo pekee uliokufanya wewe na hayati Bernard Membe mpenye hadi hatua hiyo ya ‘tano bora’.
Balozi Amina Sulum Ali, unajua kilichomponza. Kauli kuwa angefanya kazi na mzee Lowassa pale ukumbini, ilikuwa na neema kwake, lakini ikawa maumivu kwa aliyeshika rungu.
Utakumbuka kabla ya matokeo kutangazwa, maana nilikuwapo ukumbini, Mwenyekiti alimwambia Msimamizi wa Uchaguzi: “Matokeo ndiyo yenyewe?” Akapewa akayaangalia, kisha akasema: “Sawa sawa, sasa haya kayatangaze.”
Hujawasikia Balozi Amina wala Balozi Dk. Asha Rose Migiro waliofika hatua ya ‘tatu bora’ wakilalamika kokote au wakipiga jaramba na kujitangazia umalkia.
Leo, January unatajwa kila kona. Bahati mbaya hutajwi kwa mazuri. Nikizungumza na mawaziri, wengi walikuwa wakikulalamikia. Uliwajengea taswira kuwa unachosema wewe ndicho kinakuwa.
Tukiwa Uturuki, Ufaransa na Korea, kumbuka ulivyokuwa na wenzako. Korea pekee ndipo ulizungumza na waandishi wa habari na wahariri ukiwa ziarani, lakini hii ni baada ya kukuomba, si kwamba ulipanga.
Angalia mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi nyingine wakiwa na marais wao kwenye ziara wanavyofanya. Wanakuwa na mikutano na waandishi zaidi ya mara tatu kwa siku.
Angalia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza wa sasa, David Lammy, ambaye amekuwa Mbunge wa Jimbo la Tottenham tangu mwaka 2000 au Waziri wa 71 wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, wanavyowatangaza wakuu wao wa nchi wakiwa ziarani nje.
Bila Waziri kuzungumza na vyombo vya habari kuonyesha kazi kubwa anayoifanya Rais ziara za nje, uvumi unaanza kuenea kuwa Rais hafanyi kazi yoyote nje ya nchi.
Inafika mahala, ofisi binafsi ya Rais ndiyo inapambana kupata waandishi wa kusafiri nao waeleze kazi kubwa anayoifanya Rais kwa ajili ya nchi, wakati kwa nchi nyingi duniani hilo ni jukumu la msingi la Waziri mwenye dhamana na Mambo ya Nje.
Kila kona anapokwenda January, anahusishwa na ukusanyaji wa mafungu kwa ajili ya 2030, na bahati mbaya, sijaona akikanusha. Zipo nyakati pia amehusishwa na mbio za urais mwaka 2025, ila hii angalau ameikanusha kwa kusema yeye ni hadi 2030. Najiuliza kwa nini mtu uhusishwe na habari mbaya nawe usizikanushe?
Ilifika mahala wawili hawa; Nape na Makamba, wakagombana na Rais John Magufuli, ingawa katika hilo Nape namtetea maana alifukuzwa uwaziri kwa kutetea uhuru wa vyombo vya habari, hata kama nyuma ya pazia walikuwa na ugomvi wao yeye na Paul Makonda, ambaye sisi wanahabari tunaamini Makonda hakuwatendea haki Clouds.
January tuhuma zilizomwondoa kwenye Serikali ya Magufuli zilikuwa ni kujitukuza na kupenda ukuu, akaonekana yeye ndiye mhimili wa Serikali na hivyo bila yeye, serikali haiwezi kwenda.
Tuhuma zilezile, zimerejea na kumwandama aliporejeshwa serikalini na Rais Samia, lakini hakuonekana kuzijali. Kumbe kwa kufanya hivyo, amejipalia makaa ya moto.
Sitanii, Rais Samia ameliambia taifa mara kadhaa kuwa kusema “naomba” isichukuliwe kuwa ni udhaifu. Shida ninayoipata, naona baadhi ya watu ni kama hawajifunzi.
Wangejiuliza kama Rais Samia amepata ujasiri wa kubadili Katibu Mkuu Kiongozi na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kwa siku moja, na ndani ya miezi saba Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa akamwondoa, miezi 11 baadaye akamwondoa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa mwingine na sasa amewaondoa mawaziri wawili waliowaaminisha watu kuwa wana nguvu sana na hawagusiki, amewafagia kwa siku moja, huyu ni mtu wa kuchezea kweli?
Narudia, huyu Mama si wa kumchezea. Ukimtafsiri kwa sauti yake na jinsia yake, utakuwa umeumia sana. Aliwahi kusema hatutasikia akifoka na kutishana, ila; “…nitaongea kwa KALAMU✍”.
Ndugu zangu mawaziri mliosalia na mlioingia, msimjaribu huyu Mama, hajaribiki. Kikubwa chapeni kazi. Ukiwa Waziri wa Maji au Kilimo, yabebe matatizo yote ya maji au kilimo, Rais abaki kupata taarifa za ufanisi.
Mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na watendaji wengine, kazi yenu si kupika majungu, bali mnapaswa kuangalia vitendea kazi (instruments) mnavyopewa siku ya uteuzi, kisha mjiwekee malengo ya kuvitekeleza.
Katika kufikia malengo hayo, uwazi na ushirikiano katika ofisi zenu viwe vigezo viwili vya mwanzo. Ugomvi, ubinafsi, kubadili viti, madereva na watendaji mnapoingia ofisini si sehemu ya maagizo aliyowapa Rais wakati anawateua.
Sitanii, tulikuwa tunamsema Mzee Lowassa kuwa ni “Mzee wa Maamuzi Magumu”, akaja Magufuli, lakini kwa muda niliomfuatilia Rais Samia, ni Rais wa Maamuzi Magumu kweli kweli!
Angalau nikitaja machache ninayoyafahamu, Rais Samia alipoingia madarakani amekumbana na madeni yenye riba za kutisha. Kuna mikopo mingine ilikuwa ya kibiashara. Najua kuna watu wananichukia nikiliandika hili, ila ukweli ni sawa na ncha ya mkuki, haupigwi konzi.
Rais Samia alikutana na ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo ujenzi wake ulikuwa katika wastani wa asilimia 33 wakati Rais Magufuli anafariki dunia.
Namshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kufanya uamuzi wa kuanza ujenzi wa Bwawa la Nyerere ambalo sasa limeanza kuzalisha megawati 705 mwaka huu kati ya megawati 2,115 zinazolengwa.
Hapa kubwa ninalosema ni kupata fedha zaidi ya Sh trilioni 6.5 za kulijenga na baadhi ya mikataba yake ya maagizo aliyoikuta, halikuwa suala la mchezo.
Ujenzi wa Daraja la Magufuli (Busisi) wakati Rais Magufuli anafariki dunia, ilikuwa ndiyo wanapeleka vifaa ‘site’. Nampongeza Magufuli pia kwa wazo hili kubwa.
Wakati anafariki, halikuwa na hata nguzo moja, ila leo liko hatua ya mwisho. Reli ya Mwendokasi (SGR) kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro, Dodoma na baadaye Dodoma – Tabora – Mwanza na Tabora – Kigoma, nayo ni hadithi nyingine.
Treni ya Dar es Salaam – Morogoro tayari imeanza kazi na Dar – Dodoma inaanza wiki hii, yaani Julai 25, 2024. Tunakwenda kuondokana na usafiri wa mabasi kwa saa 8 hadi 10 barabarani, ambapo tutatumia saa 3 Dar – Dodoma. Nawahurumia sana baadhi ya matrafiki waliowekeza matumaini yao katika rushwa za madereva barabarani!
Safari moja nje ya nchi ya Uturuki, Rais Samia amepata dola bilioni 6.5, sawa na Sh trilioni 17.3 kwa ajili ya ujezi wa reli kwa kipande cha Dodoma kwenda Tabora – Kigoma, na tayari fedha za kipande cha Tabora – Mwanza ziliishapatikana.
Amejenga madarasa 18,000, vituo vya afya zaidi ya 400 nchi nzima, barabara za vijijini na mengine mengi.
Nimeyagusa haya, kuonyesha umuhimu wa kutambua nguvu na ubavu alionao Rais Samia kuwa si mtu wa kumpuuza na kumchukulia poa. Wateule wake wakiendana na kasi yake, ukiangalia maendeleo anayoyafanya na kazi ya kukuza demokrasia, si muda mrefu Tanzania tunakwenda kuwa nchi tajiri, nasi tutaanza kutoa misaada kwa nchi maskini.
Kwa vyovyote iwavyo, kuwawajibisha mawaziri hawa wawili kwa kauli na matendo yao, nafahamu kuwa wao na familia zao wanasikitika, lakini Watanzania wamemwelewa vizuri na kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi huu.
Wengi walionipigia simu na kunitumia ujumbe mfupi, wamempongeza Rais Samia kwa kusimama na sheria na kutuma ujumbe mzito kuwa yeye ndiye Rais hivyo kama yupo anayedhani sikio ni kubwa kuliko kichwa, akamuulize Job Ndugai. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827