▪️Mradi wa visima 10 Nzuguni A kuzalisha lita 20m kwa siku
▪️Visima zaidi kuchimbwa maeneo ya pembezoni ya Jiji kupunguza Mgao
▪️Waziri Aweso aweka kambi Dodoma kushughulikia suala la Maji
▪️Mbunge Mavunde apongeza jitahada za serikali kutatua kero ya maji
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Rais Dkt. Samia S. Hassan ameelekeza utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya Bilioni 45 kutatua changamoto ya Maji Jijini Dodoma wakati ikisubiriwa utekelezaji wa Miradi ya kuleta maji kupitia Ziwa Victoria na mradi wa Bwawa la Farkwa.
Waziri Aweso ameyasema hayo leo wakati akishuhudia utiaji wa saini wa mkataba wa mradi wa kusambaza maji kupitia visima vya maji vya Nzuguni A wenye thamani ya Tsh 5bn unaotarajiwa kuwanufaisha watu 123,095.

“Mbunge wenu alileta maombi kwa Rais Samia juu ya uchimbwaji wa visima virefu wakati wa mkutano wa Mh. Rais pale Mpunguzi na sisi Wizara tukapata maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi.
Tunamshukuru Mh. Rais Samia kwa kulivalia njuga suala la maji hapa Jijini Dodoma kwa kuelekeza utekelezaji wa miradi ya maji ya zaidi Tsh 45bn ambayo itasaidia sana kupunguza tatizo la mgao wa maji katika maeneo mbalimbali.
DUWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine kama vile Nala (3.8bn), UDOM,(1.2bn), Mji wa Serikali (35.6bn), n.k. Aidha wizara ya maji kwa kushirikiana na taasisi
zake (DUWASA na RUWASA) imeunda timu zinazo endelea na Utafiti wa Maji chini ya Ardhi na Uchimbaji wa visima katika maeneo ya Mzakwe, Nzuguni, Kisasa, Nkuhungu, Miganga, Zuzu, Msalato na Ihumwa.

Nipo hapa Jijini Dodoma na kesho naanza ziara maalum kukagua utekelezaji wa miradi hii ili wananchi wa Dodoma wapate maji ya uhakika” alisema Aweso.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amesema utekelezaji wa mradi wa usambazaji kupitia Nzunguni utasaidia kupunguza adha ya mgao wa maji kwa wananchi wa maeneo ya Nkuhungu,Miganga,Chidachi,Nzuguni, Kisasa-Bwawani,Mwangaza, Ipagala, Ilazo, na Swaswa, Mpamaa na Njedengwa.
Akitoa taarifa yake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA) Eng. Aron Joseph amesema Mradi huu unalenga kuhudumia watu wapatao 123,095 katika maeneo yaliyotajwa hapo juu.
Kukamilika kwa mradi huu kutapelekea ongezeko la uzalishaji kutoka lita milioni 81 hadi 91 kwa siku sawa na ongezeko la 30% kutoka chanzo cha Nzuguni.




