Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Leo ni Desemba 31, 2024. Tunaumaliza mwaka. Ikiwa unasoma makala hii, basi ujue nawe ni mmoja wa wateule wa Mungu alioendelea kuwajalia pumzi.

Ni vema na haki tumshukuru Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai, kwani wapo wengi wangetamani kuwa duniani, ila Mungu amewapenda zaidi. Msomaji itumie siku ya leo japo kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu, jamaa na marafiki kuwapongeza kwa Mungu kuendelea kuwakirimia siha njema.

Kichwa cha makala hii kinampongeza Rais Samia Suluhu Hassan na kumwambia ameweza. Sehemu ya pili ya kichwa cha makala hii, inasema ‘Sasa tunaingia mwaka wa fitina.” Sina wasiwasi kuwa ujumbe huu unaeleweka. Tunaingia mwaka 2025, mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Ni mwaka wa mshikemshike kweli kweli.

Sitanii, nimempongeza Rais Samia labda niwakumbushe kidogo tu, timbwili lililokuwapo kuelekea Januari, 2022. Desemba kama ya leo mwaka 2021 maji yalikuwa yametibuka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Yalianza kuchomoza makundi yaliyoonekana ni mwiba kwa Serikali ya Rais Samia. Zilianza kutoka kauli za kubeza kazi zake.

Ni jukumu la vyombo vya habari na waandishi kukumbusha historia kwa ajili ya kuweka msingi bora wa siku zijazo. Tunakumbuka yaliyoanza kama uvumi, baadaye yalikuja hadharani hadi Januari 6, 2022, aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai akajiuzulu. Si ajabu katika hatua hiyo, waliodhani wao ndio CCM wenye mzizi mrefu, walitaka kumjaribu Rais Samia, ila wakakuta sivyo.

Mwaka 2022 ndio ulikuwa kipimo cha urais wa Rais Samia. Alifanya mabadiliko ya Mkuu wa Jeshi la Polisi akamwondoa Simon Sirro akamteua Camillus Wambura kuwa IGP. Kwa ujasiri mkubwa akabadili wakurugenzi wa Usalama wa Taifa wanne. Amewabadili Diwani Athumani Msuya, Said Hussein Massoro, Balozi Ali Idd Siwa na sasa Mkurugenzi Mkuu ni Suleiman Mombo.

Sitanii, hii yote alikuwa anatafuta kuweka sawa mambo na kupata dira ya uongozi aitakayo. Na kweli wakati Rais Samia anaingia madarakani tulikuwa hatulali. Msamiati wa watu wasiojulikana ulitamalaki. Kwa sasa taifa letu chini ya Mombo tunaingia mwaka mpya kwa amani. Matukio ya kutisha yamepungua kwa kiasi kikubwa. Rais na wateule wake wanastahili pongezi katika hili.

Yapo mengi ya kuonyesha kuwa Rais ameweza. Baada ya kumteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusufu Mwenda, hatusikii tena migomo ya wafanyabiashara Kariakoo. Ndiyo bado yapo matukio ya baadhi ya maofisa wachache wa TRA kutishia watu kwa kodi, lakini matukio ya akaunti za watu binafsi na kampuni kufungwa na fedha zikachukuliwa bila taarifa yamekoma.

Miaka michache iliyopita, nilipata kuandika makala kuwa TRA ikitumia mbinu za kiungwana kukusanya kodi inaweza kukusanya trilioni tatu. Rafiki yangu mmoja alinipigia simu akasema ninaota ndoto za mchana. Nakumbuka wakati naandika makala hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ilikuwa imevunja rekodi ikakusanya Sh trilioni 1.8 kwa mwezi.

Sitanii, leo nilichokisema kimeishatokea. Kamishna Mkuu Mwenda ametangaza mwezi Oktoba 2024 kuwa mwezi Septemba 2024, TRA imekusanya Sh trilioni 3.1. Bila mabavu. Sasa niruhusu leo nitabiri tena. Kwamba kwa mwenendo huu wa Rais Samia kutaka zikusanywe kodi za haki, natabiri si muda mrefu TRA itakusanya Sh trilioni 5 kwa mwezi. Subiri wakati unakuja.

“Hivyo, jinsi uchumi wetu unavyokua, tutaendelea kuongeza makusanyo kupitia mifumo madhubuti ya ukusanyaji na kuhakikisha kodi inakusanywa kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria,” alisema Rais Samia katika hotuba ya mwaka mpya kuingia mwaka 2024. Kodi inakusanywa kwa kuzingatia sheria. Ni kwa msingi huo, Rais Samia ameunda Tume ya Kodi inayochunguza wapi kuna shida ili suala hili limalizwe jumla.

Mambo aliyofanya Rais Samia ni mengi. Nchi yetu imeweka historia ya kuzindua matumizi ya Treni ya Umeme ya Mwendo Kasi (SGR) Julai, mwaka huu. Safari ya Dodoma sasa ni saa 3:30 kutoka wastani wa saa 8 hadi 10 kwa gari miezi sita iliyopita. Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere limekwishaanza kuzalisha umeme. Tanzania sasa inazalisha zaidi ya megawati 3,000 na ni ya kwanza katika Afrika Mashariki na Kati kwa wingi wa umeme.

Umeme umekuwa mwingi kwa kiwango ambacho Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, Desemba 11, 2024 wakati anazidua ujenzi wa njia ya msongo wa KV 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma, amesema imefika wakati Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) linalazimika kuzima mitambo ya kuzalisha umeme, kwani umeme ni mwingi kuliko mahitaji. Hii ni kauli ambayo haijazoeleka katika masikio ya Watanzania. Ni mafanikio ya aina yake umeme kuwa mwingi kuliko mahitaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Mh Gissima Nyamo-Hanga, alipewa miezi 6 kumaliza mgawo wa umeme na hili amefanikiwa. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mh Hassan Saidy ndiye amefanya komesha. Umeme vijijini nguzo zinapelekwa hadi maporini ilimradi uwepo msingi au kibanda kilichojengwa. Zamani watu walihonga kupata nguzo ya umeme, sasa hivi wanabembelezwa kuwekewa nguzo!

Ujio wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, umekuja sambamba na ajenda ya Rais Samia ya Nishati Safi. Kuna baadhi ya watu ajenda hii ilipoanza kutangazwa, wakasema kuna wajanja wanatafutiwa dili. Narudia, wapo watu ambapo tangu wazaliwe huona sufuria ikiwa nyeupe ndani na nje ikiwa nyeusi kwa masizi, wakidhani ndivyo sufuria zinavyotoka kiwandani. Kumbe nishati safi ya umeme na gesi, inaokoa maisha ya mpikaji.

Sitanii, makala ya leo nataka tukumbushane yaliyotokea chini ya Rais Samia. Sidhani kama naweza kuyamaliza yote, ila nitagusia kadiri nitakavyoweza maana amefanya mengi. Rais Samia ameheshimisha sekta binafsi. Kwa sasa ni lugha ya kawaida kumsikia Rais au waziri katika hotuba yake akisema tushirikiane na sekta binafsi.

Msamiati huu ulikwishakufa hapa nchini. Sekta binafsi walichukuliwa kama wezi, ila Rais Samia amewarejeshea heshima. Asante sana Mh. Rais. Wawekezaji wengi sasa wanakuja Tanzania, wakati walikwishaanza kufunga biashara na kuondoka. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa sasa karibu kila nyumba inafanya ukarabati au ujenzi wa aina fulani. Haya yalisimama kwa miaka 7 iliyopita.

Sekta ya kilimo kwa sasa ina utoshelevu wa chakula kwa asilimia 124. Hii ina maana kuwa nchi yetu watu wake wanaweza kula chakula zaidi mwaka mzima bila kuzalisha.

Ajira serikalini ilikwishakuwa msamiati. Katika hotuba ya mwaka mpya tunaoumaliza Rais alisema serikali imeajiri wataalamu wa afya 17,309. Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 190.9 kwa ajili ya kununua dawa. Kwa taarifa yako mwaka 2019 serikali ilitenga bajeti sifuri ya dawa. Rais Samia amebadili hilo.

Nafahamu wengi tunajua kuwa Rais Samia hatangazi sana ayatendayo, ila ifahamike kuwa amejenga zaidi ya vituo 400 vya afya ambavyo ukipita maeneo mbalimbali vijijini vina madirisha ya alumini (aluminum). Ameuimarisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kumteua Dk. Irene Isaka, ambaye amefanya mageuzi makubwa, ikiwamo kurejesha “Toto Afya Kadi.”

Kwenye elimu ndiyo usiseme. Kwa mara ya kwanza Januari, mwaka 2024 hakuna mzazi aliyeambiwa achangie fedha za madarasa au madawati. Rais Samia amejenga madarasa 18,000 nchi nzima, madarasa yakawa mengi kuliko wanafunzi. Katika diplomasia Tanzania imechukua tena nafasi yake. Mikutano mikubwa yote ya dunia, Tanzania inaalikwa na kusikilizwa ina maoni gani katika ajenda iliyoko mezani. Ya karibuni ilikuwa ni ya G20 iliyofanyika Novemba, jijini Rio de Janeiro nchini Brazil, ambapo Rais Samia alipewe heshima ya pekee.

Sitanii, makala hii ina sehemu mbili. Nimeandika kwa kirefu kidogo katika eneo la kufanikiwa. Nilihitimishe kwa kueleza jinsi uamuzi wake wa kurejesha mikutano ya hadhara ulivyorejesha siasa za ushindani Tanzania. Vyama vya upinzani vilikuwa vimekufa kwa miaka 7 viliyokaa bila kufanya siasa. Ndiyo maana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ukiacha figisu walizofanyiwa katika baadhi ya maeneo, kati ya nafasi 64,000 wapinzani walisimamisha wagombea 14,000. Kwa maana hiyo CCM walishindana wenywe katika nafasi 50,000.

Nimesema sasa tunaingia mwaka wa fitina. Mwaka tunaouanza kesho wa 2025 ni wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Walau nina uzoefu wa kuona uchaguzi tangu mwaka 1980 nikiwa shule ya msingi Kyakailabwa, Bukoba. Mwaka huu sasa tunakwenda kushuhudia baadhi ya watendaji na viongozi wanaoongozwa na “Roho Mtakavitu” badala ya “Roho Mtakatifu”.

Ni mwaka wa hatari kwa ndugu zetu wenye ualbino. Muda wa “masangoma” kula mbuzi umewadia. Matapeli wa kisiasa tayari wananoa midomo. Kamati za ufundi ziko “studio” zikifanya “production”. Wataalamu wa fitina wanapita si katika chama tawala tu, bali hata katika upinzani wakipanga safu na kuchoma utambi kwa wasiowataka.

Sitanii, muda wa mgeni kufika nyumbani kwako akaanza kukueleza unavyokubalika au Balile na marafiki zake wanvyokufitini umewadia. Wakati mwingine atatumia sauti bandia kwa kutumia teknolojia ya Akili Tarakirishi (AI) ionekane Balile na wenzake walikuwa wanakusimanga. Ukiwahukumu bila kuwasikiliza utaujua ukweli ikiishapita miaka mingi. Viongozi na Watanzania wenzangu tunapaswa kutuliza vichwa.

Tujipe nafasi ya kuwapima na kuwachekecha wanaokuja mbele yetu katika nyakati hizi. Najua lipo kundi lililopo kwenye udiwani na ubunge ambalo nalo linafahamu kuwa waliingia kwa mkono wa “Maradona”. Hawa wana ugomvi na kila awaye kwenye kata na majimbo. Wanasubiri mchezo wa kupitishwa kwa kuzuia wapinzania wao wakidaiwa hawajui kusoma na kuandika.

Kama hiyo haitoshi, katika ngazi ya udiwani na ubunge ndani ya CCM mwaka 2025 ni kusuka au kunyoa. Wapo wenye kambi zao, wapo wanasubiri neema za Mungu na wapo watumishi wa kweli wasiopepeta jungu walio tayari kuisaidia serikali itakayoshinda. Kwa taarifa nilizonazo kuna baadhi ya mikoa na majimbo tayari joto ni kali sana. Wapo wakuu wa mikoa wanaotuhumiwa kutumiwa, eti kwa sababu tu wamesimamia haki. Tusubiri tuone.

Ukiniuliza katika ngazi ya urais kwa CCM, sioni akipata ujasiri mtu kujitokeza kumpinga Rais Samia. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekwishapendekeza kuwa mwaka 2025 itolewe fomu moja tu, ya Rais Samia. Kwa uzoefu wangu katika siasa za nchi hii, naamini kwa CCM itatoka fomu moja tu, wakijitokeza washereheshaji, itakuwa wanatafuta kujenga jina.

Katika Uchaguzi Mkuu, tunashuhudia mtiti unaoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, bila shaka wanajipanga kupanga safu zao kwa atakayeshinda uenyekiti. Hapana shaka tutarajie kuona mbio na mtifuano Oktoba, 2025.

Makala hii imekuwa ndefu. Naomba niihitimishe kama nilivyoanza, kwamba mpaka sasa Rais Samia hajawakatisha tamaa Watanzania. Aliyoyatenda yanajisemea na wala si ya kutafuta kwa tochi. Hata hivyo, bado naamini Watanzania watapata nafasi ya kushiriki uchaguzi na kupitia sanduku la kura kuyathibitisha haya niyasemayo au kama yupo mwingine aliyetenda sawa na haya, tuishuhudie demokrasia ikichukua mkondo. Mungu ibariki Tanzania.

0874 404827