Na Albano Midelo JamhuriMedia,Songea

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa tani 71,000 za mbolea ya ruzuku katika mkoa wa Ruvuma katika msimu wa mwaka 2022/2023.

Takwimu zinaonesha kuwa kiasi hicho cha mbolea ya ruzuku kilichotolewa mkoani Ruvuma ni kikubwa ukilinganisha na mbolea ya ruzuku iliyotolewa katika mikoa mingine nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa kipaumbele kikubwa cha mbolea ya ruzuku katika msimu huu mkoani Ruvuma ukilinganisha na usambazaji wa mbolea hiyo katika msimu 2021/2023 ambapo jumla ya tani 33,501.07 za mbolea ya ruzuku zilisambazwa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiwa ofisini kwake mjini Songea

“Makadirio ya Mahitaji ya mbolea za aina zote kwa Mkoa ni zaidi ya tani 67,000. Aidha, Hali ya upatikanaji wa mbolea katika msimu huu ni ya kuridhisha’’,alisema.
Hata hivyo amesema kutokana na kushuka kwa bei ya mbolea ya ruzuku kutoka mfuko mmoja kati ya shilingi 130,000 hadi shilingi 140,000 hadi kufikia kati ya 50,000 na 70,000 msimu huu, Wakulima wengi mkoani Ruvuma wamemudu gharama za mbolea, hali iliyosababisha wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba na kutumia mbolea za viwandani kwa wingi.

Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Husen Bashe alipofanya ziara mkoani Ruvuma kukagua maghala ya kuhifadhi mbolea ya ruzuku mjini Songea


Amesema Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) ulitekeleza mpango wa utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa Wakulima msimu wa 2022/2023 na kwamba Mfumo huo ulienda sanjari na zoezi la kusajili wakulima wote, mawakala na kampuni zilizoingiza mbolea.

Kanali Thomas amesema Mkoa wa Ruvum una utoshelevu wa chakula na kuwa na ziada na kwamba Chakula kilichozalishwa katika msimu 2022/2023 kinatarajia kutumika hadi msimu wa 2023/2024 ambapo mazao ya chakula zilizalishwa tani 1,598,163 na kati ya hizo zao la mahindi zimezalishwa jumla ya tani 1,043,324.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao amesema hadi kufikia Juni,2023 Mkoa ulikwishalima hekta 897,171 za mazao ya chakula, biashara na mazao ya bustani sawa na asilimia 97 ya lengo.
Amesema hekta hizo zimetoa mavuno ya tani 1,870,800 sawa na asilimia 95 ya lengo la mavuno.ambapo katika mazao ya chakula hekta 550,310 zililimwa na kutoa mavuno ya tani 1,598,163.

ghala kuu la kuhifadhia mazao katika Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru ambalo limekuwa likijaa mazao na kusafirishawa kupisha mazao mengine yanayokusanywa kutoka katika vyama vya msingi


Kulingana na Afisa Kilimo huyo katika kilimo cha mazao ya biashara hekta zilizolimwa ni 332,459 ambazo zimetoa jumla ya tani 94,741 za mazao na kwamba mazao ya bustani hekta 14,402 zililimwa na kutoa mavuno ya Tani 177,897.

Kwa mujibu wa sensa ya watu ya 2022 Mkoa una jumla ya watu 1,848,794 ambao mahitaji yao ya chakula aina ya wanga ndani ya Mkoa kwa msimu 2023/2024 ni tani 554,638 na kuufanya Mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 1,043525.