📌Azindua mradi wa usambazaji nishati safi ya kupikia

📌Sekta binafsi kupewa kipaumbele matumizi ya nishati safi kwa bei nafuu

📌Apongeza ubunifu wa teknolojia za nishati safi ya kupikia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuubeba mkakati wa nishati safi ya kupikia ili watanzania asilimia 80 watumie nishati safi na salama ifikapo 2034.

Hayo yamebainishwa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa usambazaji mitungi ya gesi ya kupikia na majiko banifu kwa bei ya ruzuku iliyofanyika leo Februari 27, 2025 wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

“Niiombe wizara iendelee kusimamia vizuri, lakini niiombe REA iendelee na mkakati huu na sisi kwa ujumla kama Serikali tutaendelea kutunga Sera na Sheria zitakazotufanya tuende haraka na mkakati huu, ” Amesema Rais Samia.

Vilevile ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kutunga Sera rafiki zitakazowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka watanzania kuendelea kuhifadhi mazingira ili kuendelea kuhifadhi vyanzo vya maji nchini.

“Tunapoelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia tunakwenda kuondosha hatari zote za afya ikiwemo maradhi ya kupumua, macho, kulinda afya na mazingira, ” Amesema Rais Samia.

Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa wananchi wamechangamkia fursa hiyo na hadi sasa mitungi yote 3,255 katika wilaya ya Muheza imeshanunuliwa kwa bei ya ruzuku.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Advera mwijage amesema mitungi ya gesi 452,445 yanye gharama ya shilingi bilioni 8.64 inakwenda kusambazwa nchini ambapo kila wilaya itapata mitungi 3,255.