Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameiagiza Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kuhakikisha inasajili taasisi zote za umma na binafsi kabla ya Desemba mwaka huu.
Aidha Rais Samia ameitaka ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha ifikapo Disemba mwaka huu mifumo yote ya Tehama iwe inasomana.
Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 3, 2024 wakati akizindua tume hiyo pamoja na mifumo ya usajili na malalamiko ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa Taarifa Binafsi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ihakikishe taasisi zote za umma na binafsi zinapaswa kusajiliwa. Zinasajiliwa na kutekeleza Sheria ya Ulinzi wa taarifa binafsi kabla au ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, taasisi nyingi kama sio zote ziwe tayari zimesajiliwa.
“Taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi zihakikishe zinazingatia matakwa ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na ninaitaka Tume kutoa elimu na kusisitiza wajibu wa taasisi hizo. Maofisa wa tume mna kazi kubwa ya kufanya, nataka muifanye kwa weledi na ubora Zaidi…ninyi ni wadhibiti lakini zaidi ni wawezeshaji. Nendeni mkafanye uwezeshaji ili wakaguzi mbalimbali waridhike na utendaji wa haki,” amesema Rais Samia.
Vilevile, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ipeleke taarifa ya utekelezaji mara mbili kwa mwaka ili ajue mwenendo wake.
“Lakini hapa niseme Mkurugenzi Mkuu wa Tume hii ni polisi na Mwenyekiti wa bodi ni polisi pia, kwahiyo ninategemea kuona utendaji wa haki, kesi uendeshaji wake na mambo mengine yale yote yanakwenda…pia Mheshimiwa Waziri hii ni taasisi mpya na jukumu jipya wizara yako hivyo kwa upande wa sera hakikisheni mnafatilia kwa ukaribu kazi za Tume, fuatiliani kwa ukaribu ili malalamiko yanayoibuliwa yashughulikiwe kwa haraka.
“Baada ya kuwa na mfumo wa kisera na kisheria wa kulinda taarifa binafsi, sasa naitaka ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha mifumo ya Tehama yote inasomana. Mifumo ya Tehama isomane siyo yule anaelekea kushoto mwingine anaelekea kulia yule yuko Magharibi, mwingine Mashariki hakuna kusoma hakuna mawasiliano ndani ya serikali, sasa natoa wito ifikapo Disemba mwaka huu mifumo yote ya serikali iwe inasomana,” amesema na kuongeza:
“Hivyo mawaziri, manaibu Waziri na hasa makatibu wakuu mwende mkasimamie hili liwezekane, kwasababu nyinyi miweka mguu chini Waziri hawezi kufanya kazi, lakini makatibu wakuu mkitaka mkiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara husika haya mambo yanawezekana, hivyo mkashirikiane,”.
Awali Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuwa na usalama mtandaoni.
“Kuwepo kwa taasisi imara kama TCRA na sasa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni moja ya vijenzi vinavyoifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa usalama mtandaoni Barani Afrika. ” amesema Waziri Nape.
Aidha, amesema uzinduzi wa Tume hiyo ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi utaiingiza Tanzania katika orodha ya nchi za wastaarabu duniani wanaoheshimu utawala wa kisheria, wanaoheshimu ubinadamu, wanaoheshimu haki na wanaoheshimu faragha za watu.