Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ustawi wa jamii kama elimu, maji na afya ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo.
Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akifungua Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe katika kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali itahakikisha wananchi wote wanapata haki yao ya elimu kwa kuimarisha miundombinu ya Skuli ili kuendana na ongezeko la idadi ya watoto wanaohitaji kupatiwa elimu bora.
Rais Samia pia amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na ya Muungano zitahakikisha kunakuwepo mazingira bora ya kujifunza na kufundishia kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani ili kufikia lengo la wanafunzi 45 kwa darasa.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Elimu Zanzibar kwa kuunda Kikosi Kazi cha kuishauri Serikali mageuzi muhimu ya elimu ambayo yatakidhi mahitaji ya ulimwengu wa sayansi na teknolojia katika karne ya 21.
Vile vile, Rais Samia amesema utekelezaji wa Dira ya Zanzibar ya 2050 pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Taifa (Zanzibar Development Plan) unategemea upatikanaji wa wataalamu kupitia sekta ya elimu.
Hivyo, Rais Samia amesema Serikali haina budi kuimarisha wataalamu kwa kuwapatia fani zinazoendana na mahitaji ili kuiwezesha Zanzibar kufaidika na matumizi ya rasilimali ya bahari kupitia mkakati wa kuimarisha Uchumi wa Buluu.