Rais Samia Suluhu Hassan amesema Bara la Afrika linahitaji kuongeza juhudi zaidi kwa kuongeza jitihada mbalimbali zitakazoendeleza mpira wa miguu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 10, 2022 alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia katika ufunguzi wa Mkutano wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jijini Arusha.
“Rais Samia aliamua na kukubali kuwa mdhamini wa mashindano ya Klabu Bingwa kwa vilabu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (SAMIA CUP) ili kuunga mkono maendeleo ya mpira wa miguu Afrika na duniani.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Samia anaamini mkutano huo utafungua njia kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano mingine ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na CAF na kutoa fursa ya kuandaa mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na CAF na hata FIFA.
Amesema kuwa kwa miongo kadhaa Tanzania kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekuwa na mahusiano mazuri na CAF pamoja na FIFA. “Mahusino hayo yamekuwa chachu ya kuhamasisha na kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.”
“Ujenzi wa vituo viwili vya michezo chini ya TFF kwenye miji ya Tanga na Dar es Salaam ni kielelezo cha mahusiano hayo mazuri. Tunawashukuru sana FIFA kwa uwekezaji huo na kuendelea kutuunga mkono katika kuboresha mchezo huu unaopendwa na watu wengi nchini na duniani kwa ujumla”
Waziri Mkuu amesema ni matarajio ya Tanzania kuwa FIFA itaendelea kubuni miradi mingi zaidi kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya ujenzi wa miundombinu ya michezo. “Tanzania kwa upande wake ipo tayari kuendelea kuimarisha uhusiano wake na FIFA na wanachama wake na CAF ikiwemo”
Naye, Rais FIFA, Gianni Infantino amesema kuwa wataendelea kulinda timu za taifa kwa kuwa ni muhimu katika kukuza mpira wa miguu duniani. “Wachezaji wanafuraha kuchezea timu za taifa na hata mataifa yanayo furaha kuona wachezaji wao wanawakilisha timu zao za taifa, FIFA pia tutaendelea kuwekeza na kuhakikisha soka la Afrika lina kua zaidi.”
Amesema kuwa Mwaka 2022 ni mwaka ambao dunia itaungana katika kusherehekea michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya kupitia kipindi cha ugonjwa wa UVIKO 19. “Tunaamini ni mwaka ambao moja ya nchi ya Afrika inaweza kubeba kombe la dunia”
Kwa upande wake, Rais CAF Dkt. Patrice Motsepe amesema watu wa Afrika wanapenda mpira wa miguu kwa kuwa ni sehemu ya furaha kwa waafrika wengi na anaamini shirikisho hilo litafanikiwa kuhakikisha soka la Afrika linakuwa na ushindani duniani. “Afrika ni moja ya bara ambalo limezalisha wachezaji wengi wanaofanya vizuri duniani.”
Awali, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa wanashukuru kwa mchango mkubwa unaotolewa na CAF na FIFA katika kukuza mchezo wa mpira wa miguu nchini, Afrika na Duniani kwa ujumla.