Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wakurugenzi wa mashirika mbalimbali ya serikali leo Februari 24, 2023
Amemteua Nehemia Kyando Mchechu, kuwa Msajili wa Hazina. Kabla ya uteuzi huo Mchechu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).Mchechu anachukua nafasi ya Mgonya Benedicto ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Rais Samia amemteua Hamad Abdallah, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kabla ya uteuzi huo, Abdallah alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Gimcoafrica Limited na anachukua nafasi ya Mchechu ambaye ameteuliwa kuwa Msajili wa Hazina.
Aidha Rais Samia amemteua Mussa Mohammed Makame, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Kabla ya uteuzi huo, Makame alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na pia ni Mshauri Mwelekezi wa masuala ya mafuta na gesi nchini Tanzania. Makame anachukua nafasi ya Dkt. James Mataragio ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Uteuzi huu ni kuanzia tarehe 24 Februari, 2023