Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya maendeleo ya Shule ya Sekondari ya Seminari Uru, mkoani Kilimanjaro.
Mchango huo umetolewa ili kuweka alama ya kumbukumbu ya kumuenzi marehemu Padri Canute Mkwe Shirima AJ, aliyewahi kuwa Baba Gombera wa shule hiyo, mojawapo ya seminari maarufu nchini.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, alitangaza mchango huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia alipokuwa akitoa salaam za pole na rambirambi katika ibada ya mazishi ya Padri Shirima, iliyofanyika Seminari ya Uru, Alhamisi, Machi 20, 2025.

“Haya yote niliyoyasema hapa kumhusu Baba Gombera mstaafu Padri Canute Shirima, alivyokuwa mlezi mzuri akifundisha nidhamu na uwajibikaji, nilimwambia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nilimtaarifu kuwa nakatisha ziara ili kuhudhuria mazishi haya. Mheshimiwa Rais akaniambia anatoa shilingi milioni 50 kwa Seminari ya Uru ili mtengeneze jambo lolote litakaloenzi heshima ya Padri Shirima,” alisema Balozi Nchimbi.
Akizungumzia marehemu Padri Shirima, Dkt. Nchimbi, ambaye pia aliwahi kuwa mwanafunzi wa seminari hiyo, alisema alikuwa mwalimu mahiri aliyesisitiza nidhamu na uwajibikaji kwa wanafunzi wake.
Aliongeza kuwa uongozi wa Padri Shirima ulisaidia Seminari ya Uru kupata sifa kubwa kwa kutoa wahitimu waliodhihirisha uwezo mkubwa katika nyanja mbalimbali.
“Tunawashukuru sana wazazi wa Padri Shirima kwa malezi mazuri waliyompa, ambayo nasi tuliyapata kupitia yeye. Asanteni sana Mapadri Watume wa Yesu Kristo na mapadri wote mliopo. Asante sana Baba Askofu Minde kwa heshima hii ya kuja kuongoza ibada ya kumuaga mwalimu wetu,” alisema Balozi Nchimbi.

Akiongoza ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Askofu Rudovick Joseph Minde ALCP/OSS, alisema marehemu Padri Shirima alikuwa zawadi ya Mungu kwa jamii aliyowatumikia.
“Kwa namna alivyoshuhudiwa hapa na umati huu uliokusanyika, mmeona na kusikia jinsi alivyolea watu wakubwa sasa, wakiwemo maaskofu, mapadri, viongozi wa juu serikalini, na hata tumepata salaam kutoka Ofisi ya Rais… Padri Canute alikuwa zawadi ya Mungu kwetu,” alisema Askofu Minde.
Padri Canute Mkwe Shirima, wa Shirika la Watume wa Yesu, ambaye alifariki akiwa katika utume nchini Afrika Kusini, alizikwa kwa heshima zote za Kanisa Katoliki katika makaburi ya Shule ya Sekondari ya Seminari Uru, Moshi, Kilimanjaro.




