Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Kigoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa vijijini Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.
Wakiongea na JAMHURI DIGITAL kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo wamesema Rais Samia amepunguza kwa kiasi kikubwa kero ya upatikanaji huduma za afya baada ya kuipatia halmashauri hiyo mabilioni ya fedha kwa ajili ya uboreshaji miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa Zahanati, Vituo vya afya na Hospitali mpya ya Wilaya hiyo.
Mzee Mustafa Nyandwi (80) mkazi wa Kijiji cha Lalambe ambaye ni Mwalimu Mstaafu amesema sasa hawahangaiki tena kwenda hospitali za mbali kufuata matibabu kwa kuwa Rais amewasogezea huduma hizo katika vijiji vyao.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Nyenge kilichoko katika kata ya Kurugongo Wilayani humo Dkt Makame Heri amesema maboresho makubwa ya miundombinu ya afya yaliyofanywa na serikali ya awamu ya 6 yamewaongezea ufanisi katika utoaji huduma hizo kwa wananchi.
‘Tunampongeza sana Rais kwa kujenga Vituo vya afya na Zahanati za kutosha katika vijiji mbalimbali, hali ilikuwa mbaya, wananchi walikuwa wanatembea umbali mrefu sana kufuata huduma hizo’, ameeleza.
Amebainisha kuwa ujenzi wa vituo hivyo umeenda sambamba na kuajiri watumishi wapya wa sekta hiyo hali ambayo imeboresha utoaji huduma kwa jamii.
Naye Afisa Muuguzi wa Kituo hicho Dkt Richard Marwa amempongeza Rais Dkt Samia kwa kuwapatia zaidi ya sh mil 800 kwa ajili ya ujenzi wa maabara, wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, kuhifadhia maiti, kufulia na ununuzi wa vifaa tiba.
Amefafanua kuwa kuboreshwa kwa Kituo hicho kutawanufaisha wakazi wa zaidi ya vijiji 10 vilivyoko katika kata hiyo na kata jirani.
Ametaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni Kabulanzwili, Nyenge, Malalo, Kitema, Shunguliba, Lalambe, Titye, Migunga, Kurugongo na Chekenya.
Akiongea kwa niaba ya akina mama wenzake Mary Muhange (45) mkazi wa Titye ameishukuru serikali ya Rais Samia kwa kujali afya za wananchi wake na kumhakikishia kuwa watamuunga mkono kwa kumpa kura zote katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.