Rais wa Kenya William Ruto ameyataja matukio ya Jumanne ambapo waandamanaji wanaopinga nyongeza ya kodi waliingia bungeni na taasisi nyingine za serikali kuwa ni uhaini.
Alionya kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya waandamanaji watakaojihusisha na ghasia.
Watu sita wamethibitishwa kufariki na zaidi ya 100 wamejeruhiwa. Lakini idadi hiyo huenda ikaongezeka.
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kutoka Ikulu, Bw. Ruto alitaja waandamanaji hao kama wahalifu hatari na kuonya vikali wafadhili na waandalizi wa maandamano hayo.
Tofauti na maandamano ya awali – kwa kawaida yakiongozwa na upinzani – haya hayana kiongozi.
Vijana walihamasishana kupitia mitandao ya kijamii kuzungumzia muswada wa fedha unaolenga kuwasilisha ushuru mpya.
Licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kuwakemea maafisa wa polisi kwa kutumia risasi kuwatawanya waandamanaji, rais alipongeza juhudi zao katika kujaribu kuzuia hali hiyo.
Wakati huo huo jeshi la Kenya limetumwa kote nchini kusaidia polisi katika kurejesha utulivu.
Maandamano mengine yanatarajiwa siku ya Alhamisi, wakati wabunge watakaporatibiwa kupiga kura yao ya mwisho kuhusu mapendekezo ya kodi, kabla ya kuidhinishwa na rais.