Mpenzi msomaji wa JAMHURI, katika toleo lililopita tuliona jinsi ambavyo Mwalimu Nyerere alijizatiti kutetea Muungano na mambo mengine mengi kwa maslahi ya Taifa letu. Sasa endelea na sehemu hii ya mwisho ya makala hiyo…
Endelea kutafakari. “As President of Tanzania it is my duty to safeguard the integrity of the United Republic. But if the masses of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the Union was prejudicial for their existence, I could not advocate bombing them into submission. To do so would not be to defend the Union. The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.”
Maneno hayo yanapatikana ukurasa wa 247 wa kitabu cha Profesa Issa G. Shivji kiitwacho “Pan-Africanism or Prognatism?” Binafsi naona ibara ya 2 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, inadhihirisha kuwa Muungano haupo kwa sababu “The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members (Zanzibar?) was withdrawn” na “consent” kutoka Tanganyika isiyokuwapo (does not exist) inaendelea kuwapo kwa vipi na kwa namna gani?
Nimalizie makala yangu kwa hitimisho hili. Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwasisi wa Taifa letu kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kila kiongozi wa Taifa letu ajue anapimwa kwa misingi na maadili aliyoyaweka na kutuachia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Wakati wa enzi za Mwalimu anachokilalamikia aliyewahi kuwa Waziri Mkuu Frederick Sumaye na Cyprian Musiba kisingekuwapo. Na rushwa katika uchaguzi wa CCM wenyewe wanataka tukubaliane nao kuwa “it’s the only game in town”.
Hili ni janga la Taifa kwa sababu chama cha waabudu rushwa huzaa serikali ya wala rushwa waliokubuhu – qualis peter talis filius – kama alivyo baba, ndivyo alivyo mwanaye. Wanaosimama kwenye majukwaa na kujiapiza kuwa wanamuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere huku wakishindwa vibaya kuishi kwa vitendo, misingi na maadili aliyotuachia, hao ni wanafiki wakubwa wasiostahili hata chembe kuitwa viongozi. Dawa yao, nguvu na mamlaka ya umma, viko jikoni vinachemka taratibu kwa muda wa miaka takribani mitatu iliyobaki. Wakati ukifika lazima waiywe dawa hiyo.
Sijui kama makala imefanikiwa kuonesha kuwa pamoja na sifa chanya tele tele za Mwalimu, alibaki kuwa binadamu aliyeweza kufanya makosa. Kuna sentensi yake maarufu ya “tusifanye makosa, kwani sisi malaika? Wakati mwingine Mwalimu alituonya akisema yale mabaya acheni. “Tatizo lenu ni kuwa hata yale ya msingi mnayahoji”.
Haya ni maneno ya kiongozi mkweli kwa nafsi yake, mnyenyekevu, kiongozi anayekubali kuwa yeye ni mtumishi wa watu. Naamini ni kiongozi anayetambua kuwa kauli ya watu ni kauli ya Mungu, na hivyo kuomba msaada wa Mungu katika kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia waja wake Mwenyezi Mungu.
Viongozi, hususani watawala wa nchi yetu kwa sasa kwa yale mema ya Mwalimu, si dhambi kuanza upya na kumfuata Mwalimu kwa vitendo. Kwa viongozi wajao, wajue jambo hili. Mtahukumiwa kwa kuacha kuyaishi na kutekeleza kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu, uadilifu na misingi aliyotuachia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mungu ibariki Tanzania.
Mwandishi wa makala haya, Arcado Ntagazwa, amewahi kushika nyadhifa katika taasisi, Mbunge na Waziri katika Wizara mbalimbali. Kwa sasa ni mwanachama hai wa Chadema. Anapatikana kwa simu namba
0786 – 617777.