Ndugu Rais, sehemu ya kwanza ya waraka huu niliishia kwenye maneno ya hekima ya uhifadhi yaliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Agosti 10, 1975. Kwa ufupi Mwalimu alieleza matokeo ya dhambi ya kuteketeza wanyamapori na misitu iliyotendwa na Wazungu katika mataifa yao. Mwalimu alituasa tusitende dhambi hiyo.
Ndugu Rais, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 27, inasema: (1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.
Sina kitu cha kuongeza kwenye maneno haya murua kabisa yaliyoainishwa ndani ya Katiba yetu. Katiba inatutaka “watu wote”, pamoja na mambo mengine, kupinga aina zote za uharibifu wa rasimali za nchi. Watu wote tunatakiwa kujiona ndiyo “waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa letu” – kwa kuhakikisha tunalinda urithi huu tuliopewa na Mungu. Mimi si mtaalamu wa Katiba, lakini nadhani rasilimali za nchi kwa muktadha wa Katiba kwenye waraka huu hii ni misitu na wanyamapori. Siyo ng’ombe. Tuulinde Katiba.
Ndugu Rais, kama yupo anayetilia shaka mapenzi yako kwa Watanzania, hasa wale walio wanyonge, huyo atakuwa na lake jambo. Umejitanabaisha kama mtetezi mkuu wa wanyonge.
Isitoshe, msimamo wako wa Januari 15 ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020. Sehemu ya Ilani hiyo inasema katika kipindi cha miaka mitano, pamoja na mambo mengine, CCM itafanya haya: “Kutatua migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo ya jirani na hifadhi kwa kushirikisha wadau katika kuhakiki mipaka ya maeneo ya hifadhi kwa kuweka alama za kudumu; kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi; na kuzingatia utawala wa sheria katika kusimamia rasilimali za maliasili…”
Ilani hiyo hiyo inatambua umuhimu wa kuyahifadhi mazingira kwa kusema: “Mazingira ni suala mtambuka ambalo linagusa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Aidha, upo uhusiano tegemezi kati ya mazingira na maendeleo na kwamba uharibifu wa mazingira si tu husababisha umaskini, bali umaskini nao husababisha uharibifu wa mazingira.”
Ndugu Rais, kuwatetea wanyonge ni jambo jema, lakini muhimu zaidi ni kuhakikisha huruma na utetezi huo havigeuzwi kuwa janga kwa hao wanaotetewa. Kugusa maeneo ya hifadhi kwa namna yoyote iliyo nje ya uhifadhi ni kukaribisha umaskini na maafa kwa taifa.
Mazingira ndiyo mama na baba wa uhai wetu. Binadamu anayeishi msituni hata kama hana mavazi, ana amani moyoni na akilini kuliko binadamu anayeishi katika mji wenye majengo ya fahari usio na mazingira mazuri.
Kilimo cha kuhamahama kimezuiwa hata kwenye Biblia. Katika Agano la Kale Mungu aliamuru mashamba yapandwe na kuvunwa kwa miaka sita, kisha kulimwa na kuachwa bila kupandwa mbegu kwa mwaka wa saba ili kujaza tena virutubishi vya udongo. Yote mawili (Kutoka 23:10-11; Mambo ya Walawi 25:1-7).
Uhai wa mwanadamu na viumbe wengine umo ndani ya mazingira. Mazingira ndiyo nyumba ya viumbe hai wote. Humo kunapatikana hali ya hewa nzuri, maji, vyakula na dawa zinazotokana na miti. Ni kwa sababu hiyo kwa watu makini suala la mazingira ni la ama kufa au kupona.
Naomba nirejee kwa muhtasari maudhui yaliyomo kwenye tamko. Umezuia wavamizi kuondolewa maeneo yaliyohifadhiwa; umeagiza wataalamu/viongozi wa wizara husika watambue na kurasimisha vijiji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi; umeagiza maeneo ya wanyamapori na misitu yasiyo na rasilimali hizo yagawiwe kwa wafugaji na wakulima; na mwisho umeagiza sheria ya vyanzo vya maji iangaliwe ili ikiwezekana wakulima walime ndani ya mita 60 kutoka eneo la chanzo cha maji.
Tumeona kuwa kati ya hekta milioni 44 za ardhi zinazofaa kwa kilimo nchini, ni asilimia 20 tu zinazotumika. Hatuna uhaba wa ardhi ya kilimo nchini. Tuna ardhi kubwa mno.
Ndugu Rais, kwenye ufugaji tusipokuwa makini tutajikuta tunarudi nyuma ilhali dunia ikienda mbele. Badala ya kuhamasisha umegaji wa maeneo ya hifadhi, viongozi wahamasisheni waanze kufuga badala ya kuchunga. Tujifunze kwa marafiki zetu Botswana. Ili mchungaji wa Tanzania apate faida kama ile ya ng’ombe mmoja wa Botswana, hana budi kuwa na ng’ombe kama 50. Huu ni utumwa.
Tamko lako, Ndugu Rais, la kumega ardhi na kuwapa wafugaji linalenga kutenga ardhi kubwa zaidi ili wafugaji waendeleze ufugaji wa kijima. Dunia gani inayoendelea ambayo watu wanang’ang’ana kuongeza maeneo badala ya kuongeza tija kwenye mifugo? Maeneo yanayoachwa na wafugaji ni yale yaliyoharibiwa, yakakosa rutuba, yakakosa malisho.
Kama utaratibu utakuwa huu huu wa kumega hifadhi na kuwapa wachungaji na wakulima kila wanapokuwa wameharibu walipo, nani anaweza kula kiapo cha kutuhakikishia kuwa ugawaji huu uliotangazwa utakuwa wa mwisho? Ndugu Rais, una hakika mwaka kesho hautaombwa tena na hawa wafugaji na wakulima uwamegee maeneo ya hifadhi?
Kwa mgawo wa ardhi wa staili hii kila mwaka, hifadhi gani ya wanyamapori na misitu itasalimika?
Nililo na hakika nalo ni kuwa hata kama wachungaji hawa watapewa eneo lote la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, na kama ufugaji utakuwa huu huu, kamwe hawataridhika!
Ufugaji huu wa kijima hauna tija. Ng’ombe anaswagwa kutoka Nyang’hwale hadi Sumbawanga. Wanavushwa hadi Kasesya, Zambia. Huyo ng’ombe hawezi kuingia kwenye soko la dunia. Sana sana atauzwa kwa makabwela wenzetu Comoro. Ng’ombe wenye maradhi kwa sababu ya kukosa chanjo na tiba nyingine watauzwa soko gani la kimataifa?
Tunapambana na adui ujinga. Watoto hawa wa wachungaji tunawaandalia maisha gani katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia? Watawezaje kupata elimu ilhali kila leo wako machungani – wakitoka upande mmoja wa nchi hadi upande mwingine?
Ndugu Rais, tangu ulipotoa msimamo wako kumejitokeza mamia kwa maelfu ya wafugaji nchini kote ‘kuandamana’ kukupongeza. Nakuomba pongezi hizi uzipokee kwa hadhari. Hii ni kama furaha ya mtoto anayeambiwa “leo hakuna masomo.” Atashangilia kwa sababu hajui kukosa kwake masomo kuna athari kwenye maisha yake yote.
Watashangilia na kukupa majina matamu matamu. Watasema hawajawahi kuwa na kiongozi mzuri wa aina yako. Watakuimbia na kukuandalia zawadi. Lakini ni hawa hawa ambao ukishaondoka madarakani na hifadhi zote zikiwa zimeshakufa; na wao wakikosa maji wataanza kukulaani. Usikubali sifa hizi za muda. Wakikosa maji hawatakumbuka uliwakubalia wamegewe hifadhi za misitu. Mifugo yao itakapokufa kwa kukosa maji watakushutumu na kuhoji kwanini ulikubali kufanya ambayo watangulizi wako hawakuyabariki.
Huruma yako imepotoshwa na inaendelea kupotoshwa. Wapo wanaodhani kwa amri yako umewaruhusu wajitwalie maeneo yaliyohifadhiwa. Hata wale walio nje ya hifadhi sasa wamekwenda kujikatia mapande ya ardhi ndani ya hifadhi. Wanasema: “Tunaitikia mwito wa rais.”
Bonde la Kilombero tayari linavamiwa. Hifadhi za jumuiya za wanyamapori (WMA’s) zinavamiwa. Loliondo tayari ng’ombe kutoka Kenya wameshaanza kuvushwa kupelekwa kwenye ‘shamba la bibi.’
Vyanzo vikuu vya maji vinavyoifanya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iwe hai viko Loliondo. Hii ndiyo roho ya Serengeti. Asilimia 50 ya maji yanayoingia hifadhini humo yanatoka Loliondo. Loliondo ikifa, Serengeti itazikwa.
Tulipaswa kwanza kuainisha maeneo yote ya uhifadhi ‘yaliyokufa’ ili hatimaye yagawanywe kwa wakulima na wafugaji kama ulivyoagiza.
Ndugu Rais, kuhusu hifadhi ya mita 60 ya mito, maziwa na bahari; bila shaka sheria hii ilitungwa ili kuepusha hatari za kimazingira na kiafya. Kilimo kwenye kingo kinasababisha tope kujaa katika mito na maziwa, kinasababisha viuatilifu kuingia kwenye maji, hivyo kuua viumbe hai na hata binadamu. Fikiria sumu inayopulizwa kwenye pamba iingie mtoni! Viuatilifu vinatumika sana katika kilimo cha zama hizi. Kilimo kinapofanywa mbali na vyanzo vya maji husaidia kupunguza ukubwa wa madhara ya viuatilifu. Kuruhusu kilimo kwenye kingo ni kukaribisha majanga kwa viumbe hai, lakini pia kwa uhai wa hiyo mito na maziwa. Tujiulize, sababu gani za sasa zinazoondoa uhalali wa sheria hiyo? Ndugu Rais, hili tunakuomba ulitafakari kwa jicho la uhifadhi.
Ndugu Rais, ninayo mapendekezo machache. Mosi, nashauri taasisi kubwa za uhifadhi, yaani Mamlaka ya Ngorongoro, TANAPA, TAWA na TFS zipewe kazi ya kuainisha maeneo yanayofaa kwa uhifadhi na yale yaliyopoteza sifa za uhifadhi. Kazi hii ifanywe na wataalamu, na kamwe wanasiasa wasipewe fursa hiyo maana wao wanachoangalia zaidi ni kuwafurahisha wapigakura na si kuangalia hatima ya nchi. Tena kwa Mkoa wa Arusha tupia jicho huko.
Pili, eneo kukosa wanyama hakuna maana kwamba halifai kwa uhifadhi. Mapito ya wanyamapori (ushoroba) yaendelee kulindwa kisheria kwa sababu wanyama wana njia zao. Ni suala la ikolojia.
Tatu, wanaoishi katika vijiji 366 ndani ya maeneo ya hifadhi wahakikiwe kama kweli wote ni raia wa nchi hii. Unajua wazi namna maeneo ya magharibi mwa nchi yalivyovamiwa na wageni. Kuna taarifa zisizo na shaka kuwa wapo wageni wengi walioanzisha makazi ndani ya misitu ya hifadhi.
Nne, serikali na wadau washiriki kubadili mindset za Watanzania tutoke kwenye kilimo na uchungaji wa kutangatanga na twende kwenye kilimo na ufugaji wa kisasa uliotulia eneo moja. Twende na dunia inavyobadilika.
Tano, tujiridhishe kama kweli kilio cha malisho ni cha ‘wanyonge’ kweli au ni matajiri wanaotakatisha fedha kwa kununua ng’ombe na kugeuza hifadhi kuwa sehemu za kunenepeshea. Miaka minne iliyopita nilifanya utafiti Hifadhi ya Serengeti. Nikapata orodha ya wanasiasa, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na matajiri wenye ng’ombe maelfu kwa maelfu, lakini wamewapa maskini wawatunzie kwa makubaliano maalumu.
Ndugu Rais, naomba niishie hapa kwa leo. Nimeyasema haya kwa nia njema ya kuona rasilimali hii uliyoipokea kutoka kwa watangulizi wako inaendelea kudumu daima na milele. Nayasema haya ili ndege tulizonunua ziwalete na kuwarudisha watalii kwao. Watalii hawaji kuangalia kondoo, mbuzi au punda vihongwe. Hawaji kuangalia jangwa, maana tayari kuna majangwa mengi duniani. Wanakuja kutazama na kufurahia kazi ya uumbaji wa Mungu inayopatikana kwenye misitu ya hifadhi. Nakushuru sana.