Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema utalii ni kipaombele chake cha kwanza kwenye mnyororo wa sekta za Uchumi wa Buluu kutokana na kuchangia asilimia 30 ya pato la taifa mbali ya sekta nyengine za maendeleo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Tony Blair aliefika na ujumbe wake.
Dk. Mwinyi alimueleza mgeni wake huyo kwamba, Zanzibar ina utalii wa asili wa fukwe na urithi lakini kwa sasa inahitaji kwenda mbali kuboresha utalii wake kwa kuangalia zaidi utalii wa mikutano na michezo.
Rais Dk. Mwinyi amezitaja sekta nyengine za Uchumi wa Buluu ni pamoja na bandari ambayo inamchango mkubwa wa uchumi wa Zanzibar na ina mahitaji ya uwekezaji kwenye eneo hilo hasa bandari jumuishi itakayotoa huduma zote ikiwemo kuruhusu meli kubwa kushusha na kupakia mizigo mingi ya vyakula, nafaka, mafuta na mahitaji mengine ya uchumi.
Akizungumzia Sekta ya usafirishaji kwenye Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Mwinyi alisema kwa vile Zanzibar imezungukwa na bahari sekta hiyo pia ni muhimu kwa uchumi wake hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuuimarisha usafiri wa majini kwa abiria na mizigo.
Kuhusu sekta ya Mafuta na gesi, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Mkuu huyo wa Zamani wa Uingereza kwamba Zanzibar inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuimarisha sekta ya biashara na uchumi kupitia bandari.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza, ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taasisi ya Tony Blair hasa kwenye miradi mbalimbali ya huduma za jamii iliwemo elimu na afya.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza alisifia uzuri kisiwa cha Zanzibar ulivyobarikiwa kuwa na haiba na mwambao mzuri wa kumvutia kila mgeni aingiae na kuongeza kuwa Zanzibar imejijengea sifa duniani ya kuwa na vivutia vizuri vya utalii.
Aidha, aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza mvuto zaidi kwa kuendelea kukipatia sifa nzuri kisiwa cha Pemba kwani ni bahati kubwa kwa Zanzibar kuwa na kisiwa kizuri kama hicho ambacho ni mfano mzuri wa kivutio cha utalii duniani.
Hivyo, aliishauri Serikali kuendelea kudumisha vivutio vyake vya utalii na kuendelea kuiongezea sifa Zanzibar kiutalii duniani kote.
Tony Blair ni mwanasiasa mkongwe nchini Uingereza aliehudumu nafasi ya Uwaziri mkuu kutoka mwaka 1997 hadi mwaka 2007 anakua Waziri Mkuu wa pili kuongoza nafasi hiyo kwa muda mrefu Uingereza baada ya Magret Thatcher aliehudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 11. Blair pia ni Mwenyekiti wa taasisi ya Tony Blair (TBI).