Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Dar es Salaam

Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kati ya Tanzania na Uganda ni moja ya kielelezo kwa nchi za Afrika MAshariki za kuweka jitihada mbalimbali za kukuza uchumi kupitia sekta ya mafuta na gesi.

Akiongea wakati wa kufunga kongamano la 11 na Maonesho ya sekta ya Petrol kwa nchi za Afrika Mashariki yaliyofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kujadili fursa za maendeleo na uwekezaji katika sekta hiyo, Rais Mwinyi alisema kuna umuhimu kwa nchi za Afrika Mashariki kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi na ubunifu wa kiteknolojia ili kukuza uchumi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiteta jambo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kulia) punde mara baada ya kufunga Kongamano la 11 na Maonesho ya Petroli Afrika Mashariki lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere ( JNICC), jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP ni moja ya jitihada za kukuza uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia sekta ya mafuta ghafi.

“Tunahitaji kuona miradi mingine mingi ikivuka mipaka ya nchi zetu na kukuza uchumi kupitia sekta ya gesi na mafuta kwa maendeleo ya nchi zetu,” alisema Rais Mwinyi.

Amesema maendeleo ya kiteknolojia ni muhimu kwenye sekta ya mafuta na gesi kwa sababu dunia inakwenda kasi katika masuala ya uvumbusi wa sekta hiyo.

Pia amesifu juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuweka mazingira mazuri ya kuvutia kwa uwekezaji.

Aidha, amemsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza uchumi na kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa EACOP.

“Tunaona utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa ukiendelea ukiwemo mradi wa EACOP ambayo ni kielezo cha dhamira ya nchi katika kujipatia maendeleo kupitia fursa zinazopatikana katika sekta ya mafuta na gesi,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema ufinyu wa bajeti ni muhimu ukapewa kipaumbele katika kuendeleza sekta ya mafuta katika kanda ya Afrika Mashariki ili kufadhili miradi ya vyanzo vya nishati.

Amesema kuwa jumuiya ya EAC inapaswa kunufaika na rasilimali za mafuta na gesi zilizopo kama ilivyoaninishwa katika mpango wa maendeleo wa jumuiya hiyo wa 2050.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipokea tuzo kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kulia) punde mara baada ya kufunga Kongamano la 11 na Maonesho ya Petroli Afrika Mashariki lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere ( JNICC), jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Hakuna wakati mwingine zaidi ya sasa katika utekelezaji wa mpango wa kuanzishwa kwa mfuko wa mafuta na kutimiza ahadi iliyoainishwa katika kifungu cha 114 cha mkataba wa jumuiya hiyo,”.

“Kifungu hiki kinahimiza ushirikiano bora katika usimamizi wa rasilimali zilizopo katika nchi zetu kwa manufaa ya pamoja,” amesema Rais Mwinyi na kuongeza;

“Napongeza jitihada zinazochukuliwa na nchi za EAC kuvutia fursa za uwekezaji na ufumbuzi wa sekta ya mafuta na gesi .”

“Kupitia ufumbuzi, tutapanua ugunduzi wa mafuta na gesi katika ukanda wetu na kuwa wachangiaji wakuu katika jukwaa la kimataifa,” alisema katika mkutano huo uliojumuisha wadau kutoka nchi mbalimbali za jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini (TPDC) Bw Fransis Lupokela alikiri wazi kuwa uwekezaji wa EACOP kwenye mradi huu ni chachu ya maendeleo kwa nchi ya Tanzania na Uganda kupitia sekta ya mafuta.

“Uwepo wa mradi huu nchini umetoa fursa kwa watanzania wengi kupata ajira na fursa za kutoa huduma katika maeneo ambayo mradi huu unapita na sisi tukiwa sehemu ya wanahisa tunafurahishwa na maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa,” amesea.

wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wadau kutoka sekta ya mafuta na gesi ( hawapo pichani) wakati wa kufunga Kongamano la 11 na Maonesho ya Petroli Afrika Mashariki lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere ( JNICC), jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Petroli kutoka Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Maji na Mafuta (Ewura) Bw Gerald Maganga amesema mradi wa EACOP unatelezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Mradi wa EACOP una urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania. Washirika wa bomba la mafuta la EACOP ni TotalEnergies ikiwa na asilimia 62, huku mashirika ya Maendeleo la Mafuta nchini Tanzania (TPDC) na UNOC la Uganda yakimiliki asilimia 15 kila moja wakati lile la China (CNOOC) likiwa na asilimia 8.