Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini kupitia sekta ya utalii yanayoitangaza Tanzania kimataifa na kuitambulisha duniani kuwa nchi ya kwanza Afrika inayofanya vizuri kwa utalii na ya sita dunia nzima.

Amesema mafanikio hayo ni juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu ya utalii ikiwemo kuendelea kuliimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Pamoja na kuhamasisha mashirika mengine ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na nchi zenye masoko ya utalii, kujenga barabara na reli za kisasa zinazounganisha vivutio vya utalii, kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, na kuimarisha huduma nyengine muhimu za utalii.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2024 kwenye hafla ya ufunguzi wa Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahil (S!TE 2024) katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es salaam.

Amesema kutokana na juhudi za Rais Dkt. Samia za kukuza utalii nchini, Tanzania imeshuhudia idadi kubwa ya watalii wa kimataifa wanaotembelea sehemu mbalimbali za nchi pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa utalii ni sekta yenye ushindani hasa kwa sekta ya utangazaji, bila kutangazwa kimataifa haiwezi kufikia malengo yaliyojiwekwa.

Vilevile Rais Mwinyi ameeleza kwa mujibu wa takwimu kutoka sekta ya utalii, hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 zinaonesha kuwa Tanzania imepokea idadi ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kuwahi kufikiwa kwenye historia ya Tanzania na mapato yatokanayo na sekta hiyo, kufikia Dola za kimarekani bilioni 3.5.