Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi anatarajia kufungua Mkutano wa sita wa masuala ya anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kesho visiwani Zanzibar ambao utajadili mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya usalama wa anga.
Akizungumza na waaandishi wa habari leo wizarani kwake Kisauni nje ya Mji wa Zanzibar, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji,Dk Khalid Salum Muhammed, amesema Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo ambao utafanyika ndani ya siku mbili ambao unakauli mbiu isemayo mustakbali wa usafiri wa anga ,kudumisha mifumo ya usafiri wa anga yenye ustahamilivu”.
Amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili mambo mbalimbali ikiwemo ulinzi na mazingira,ubunifu na teknolojia na wajumbe hao watabadilishana uzoefu na utaalamu na kuweka mipango ya pamoja katika uwekezaji na moundombinu katika usalama wa usafiri wa anga.
“Mkutano huu unafanyika ikiwa ni kuimarisha usafiri wa anga hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inategemea sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa buluu”amesema.
Aidha amesema jitihada za uwekezaji zimefanywa na serikali katika usafiri wa anga na ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kituo cha biashara katika uwanja wa Abeida Amani Karume na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ambao utahusisha utanuzi wa njia za ndege na kuwezesha ndege za kimataifa kutuwa katika kiwanja hicho.
Pia amesema jengo la abiria la tatu katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume limeshazidiwa na abiria ambapo kwa mwaka jana imepokea wageni Milioni moja na laki tisa na sasa serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la pili la abiria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Masuala ya Anga Jumuiya ya Afrika Mashariki,Hamza Johari amesema kwa sasa usafiri wa anga umekua na safari za ndege zimekuwa nyingi tofauti na miaka ya nyuma.
Amesema kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi Udhibiti wa Usalama wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ambalo litawakutanisha wadau zaidi ya 200 wa tasnia ya anga,watoa huduma wa usafiri wa anga kutoka Uganda,Afrika Kusini,Sudan,Burundi, Somalia, Ethiopia, Kenya na nchi zingine.