RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi za biashara kuondoa urasimu ili kutengeneza biashara zaidi Kwa mustakabali wa kujenga uchumi wa nchi.

Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifunga Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama sabasaba.

Amesema serikali zote mbili yaani ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania Bara zina nia ya kuboresha mazingira ya biashara Kwa kuondoa tozo na kodi ili kukuza uchumi.

Amesema katika maonesho hayo jumla ya masoko tisa yamepatikana.  Baadhi yakiwa kutoka Afrika Kusini, Malawi, Uturuki na Saudi Arabia, pia ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE) iendelee kutafuta masoko zaidi.

Hafla ya kufunga Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba 2024)

“Wadau ongezeni uzalishaji wa bidhaa kama sukari, samaki, mwani ili kujitosheleza zaidi na kuweza kuuza nje ya nchi,” amesema.

Amesema kwa sasa kuna fursa ya masoko  mbalimbali ikiwemo Soko Huru la Afrika (ACFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hata Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo kwa pamoja kuna nchi 54 zenye idadi ya jumuiya nane na kwamba TANTRADE ifanye uchambuzi wa masoko hayo Ili wafanyabiashara wayatumie.

Amesema maonesho hayo yamekuwa ni jukwaa muhimu kwa wafanyabiashara kujifunza na kupata masoko ambapo jumla ya kampuni za ndani na nje zimeshiriki.

Amewapongeza wafanyabiashara kwa kutumia fursa ya maonesho hayo kukuza mahusiano ya biashara ambayo  ni muhimu kwa kuongeza ajira na mapato ya nchi.

“Maonesho yameenda sawia  na kuibuabfursa za uwekezaji na kwamba Wizara za viwanda na Biashara  zishirikiane kukuza biashara na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo,” amesema.

Amesema TANTRADE imefanya tafiti na kubaini kuwa vijana wengi wana kiu ya biashara na kwamba wadau wamepata wabia wa biashara ambayo italeta tija kwa uchumi wa nchi.

Aidha amehamasisha sekta binafsi kushiriki katika Maonesho ya Japan Expo yatakayofanyika mwakani April 2025 na kuvutia nchi zaidi ya 180 na yakitumika vizuri yatakuwa ni fursa kutangaza bidhaa za Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jaffo amesema Maonesho ya Sabasaba yametoa elimu na maarifa na wengine wameweza kuingia makubaliano Kwa ajili ya  biashara.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo

Amesema maonesho yametoa mafundisho kwa wafanyabiashara Tanzania kushiriki vyema kwenye maonesho hata ya Afrika Mashariki.

“Tanzania ni Mahali Salama pa Biashara na Uwekezaji na kuna fursa mbalimbali kwa Tanzania na Zanzibar,” amesema na kuongeza kuwa Maonesho ya Sabasaba yanaipa fursa Tanzania kushiriki katika maonesho mbalimbali ikiwemo ya China.

Amesema TANTRADE itatengeneza  taaluma kwa wafanyabishara  Ili kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira.

“Maonesho ya sabasaba yatakuwa tunu Kwa Watanzania kushiriki maonesho mbalimbali,wafanyabiashara watafundishwa dhamana ya kulipa Kodi,” amesema na kuongeza kuwa maonesho ni Jukwaa ya kujifunza Kwa lengo la kujenga nchi kiuchumi.

Mkurugenzi wa TANTRADE, Latifa Khamisi amesema Maonesho ya 48 yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo yamekuwa na washiriki 3,886 na kutoa ajira zipatazo 21,518.

Aidha watembeleaji wamefikia 53,000 mpaka jana na kuwa na mauzo ya bilioni 3.65, wafanyabiashara wapya asilimia 76.1, masoko ya nje asilimia 2.4, masoko ya ndani asilimia 73.3, wabia asilimia 10 na sekta maalum kufikia asilimia 8.8.

Amesema katika maonesho hayo kumekuwa na siku maalum Kwa nchi saba na tayari nchi moja imeshaomba kuwa na siku maalum kwa maonesho mengine yajayo ya 49.

Amesema miongoni mwa faida ya maonesho hayo, Nchi ya Iran imekubali kushirikiana na Wizara ya Mifugo kwaajili ya kuzalisha chanjo na pia kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa na programu ya kubadilishana madaktari.