Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema malengo makuu ya Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ni kugusa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki pamoja na kuwa na Dira jumuishi ambayo itamshirikisha kila mwananchi kutoa mchango wake kwa maendeleo ya Taifa.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipozindua rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali za SMT na SMZ akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Aidha , Rais Dk.Mwinyi ameiagiza timu kuu ya wataalamu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 kukutana na wadau mbalimbali kuhakikisha kazi ya kupokea maoni inakamilika kikamilifu ili kuwa na Dira yenye kubeba maono ya wananchi wote.
Vilevile Rais Dk. Mwinyi ameziagiza Tume za Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaratibu zoezi la uhakiki kwamba linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuisambaza rasimu hiyo kwa vyombo mbalimbali na kuweka mfumo halisi wa kupokea maoni.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi ameisisitiza timu hiyo ya Kitaalam kuhakikisha inamfikia kila mwanchi kote nchini ili kutoa maoni bila kujali tofauti za dini, siasa, jinsia, makundi maalum au eneo mtu analotoka kwani Rasimu hiyo ni ya Watanzania wote, hivyo alieleza ni lazima ibebe maono yao ya miaka 25 ijayo.
Kwa upandemwingine, Rais Dk. Mwinyi ameishauri timu hiyo ya kitaalamu kuandaa usimamizi mzuri wa kukusanya maoni ya wadau kwa kuzunguka nchi nzima na kuandaa makongamano na majadiliano na wadau.