Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ameifungua Skuli ya Kwanza ya Ghorofa Kisiwani Tumbatu iliyogharimu Shilingi Bilioni 7.015.
Akizungumza na wananchi baada ya kuifungua Skuli hiyo ya Sekondari ya Tumbatu iliyopo Wilaya ndogo Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja Rais Dk, Mwinyi ameziagiza Mamlaka zinazoshughulika na ajira kuhakikisha zinatoa fursa za ajira kwa Vijana wa Tumbatu wenye sifa zinazohitajika.
Aidha,amezitaka mamlaka hizo katika sekta za afya, elimu, miundombinu, maji, umeme na nyinginezo kusimamia agizo hilo ili miradi iliyomo Tumbatu ilete tìja kwa wananchi na kuongeza ufanisi.
Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inakusudia kujenga nyumba za Walimu na Dahalia ili walimu watakaofundisha katika Skuli ya Tumbatu waishi katika nyumba hizo.
Amewahakikishia wananchi wa Tumbatu kuwa kinaçhofanyika sasa ni utekelezaji wa ahadi zake na kwamba zitaendelea kutekelezwa zaidi.
Akizungumzia suala la Utalii ameeleza kuwa Serikali haina nia ya kupeleka shughuli za Utalii Kisiwani humo na kuwataka wananchi kuepuka maneno yasio na ukweli yanayoenezwa na watu wasiopenda maendeleo.
“Sina nia ya kuleta Utalii Tumbatu, utalii utapelekwa kwa watu wanaoutaka sio Tumbatu,” amesisitiza Dk.Mwinyi.
Amewahimiza vijana kusoma kwa bidii kwa lengo la kuongeza ufaulu kufuatia kuwepo kwa Skuli yenye viwango vya Ubora, Maktaba, Maabara ya Kisasa ya Sayansi na Madarasa mazuri.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi ameliagiza Shirika la Umeme kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara alilolielezea kuwa ni la nchi nzima.