Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemsifu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akisema ni mtu muhimu aliyejenga umoja wa Afrika na ustawi wa binadamu.
Ametoa sifa hizo kwenye misa maalumu iliyohudhuriwa na watu zaidi ya 500 kutoka Uganda na Tanzania kwa ajili ya kumwombea Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Nyerere ili awe mwenyeheri na baadaye mtakatifu.
Misa hiyo kufanyika katika Kanisa Katoliki la Watakatifu Mashahidi wa Uganda, Parokia ya Namugongo jijini Kampala; Juni mosi ya kila mwaka. Huu ni mwaka wa sita mfululizo misa hiyo imekuwa ikifanyika.
Siku hiyo ni maalumu kwa ajili ya kumwombea Mwalimu Nyerere ambaye kwa sasa ni Mtumishi wa Mungu.
Rais Museveni ambaye anajitambulisha kama ‘mtoto wa kwanza’ wa Mama Maria, amempongeza yeye na familia kwa juhudi zao za kupanua wigo wa washiriki wa misa hiyo kutoka Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi, Nigeria na kwingineko.
Amesema hija siyo siasa, bali ni njia ya kuimarisha umoja kwa nchi za ukanda huu na Afrika kwa jumla.
Misa iliendeshwa na Charles Kasibante kwa niaba ya Askofu Mkuu Cyprian Lwanga. Katika mahubiri yake alisisitiza watu kuimarika kiroho na amani katika taifa na umoja kwenye familia.
Amesema Juni mosi ni siku maalumu ya kuwakumbuka Mashahidi wa Uganda, sambamba na kufanya misa maalumu ya Mwalimu. Amempongeza Mama Maria na wana hija wengine kutoka Tanzania ambao huhudhuria misa hiyo ambayo huwa ni utangulizi kabla ya maadhimisho ya mashahidi ambayo huadhimishwa na madhehebu ya Anglikana na Katoliki, Juni 3 ya kila mwaka. Akaishukuru serikali kwa kuimarisha ulinzi pamoja na mchango wake katika maendeleo ya kanisa.
Rais Museveni aliwashukuru Waganda kwa kujitokeza kwa wingi kujumuika na mahujaji Watanzania, akiwamo Mama Maria na baadhi ya wana familia.
Akasema kwa takriban miaka milioni 4.5 iliyopita, hakuna Mwafrika aliyejitokeza kupigania umoja wa Waafrika na uhuru wao kama alivyofanya Mwalimu Nyerere.
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dk. Aziz Mima, alisema Mwalimu alikuwa mwanajumuiya wa Afrika aliyepigania ubinadamu, ukombozi, demokrasia na uhuru wa mataifa mengi ya Afrika.
Kwa upande wake, Profesa Mark Mwandosya, aliwashukuru watu mbalimbali, akiwamo Rais Museveni. “Tunapaswa kusali, kusali, kusali kwa Mungu ili Mungu awezeshe Nyerere awe mtakatifu,” amesema.
Mwakilishi wa familia ya Mwalimu, Anna Nyerere, ambaye ni mtoto wa pili wa Mwalimu Nyerere, alimshukuru Rais Museveni kwa kuunga mkono mchakato unaoendelea.
Jumuiya ya Stella Maris College Nsuube ya Nkokonjeru, Buikwe ambako Mama Maria alisoma pia ilijumuika kwenye misa hiyo ya kumuombea Mwalimu Nyerere aweze kutangazwa mwenyeheri na baadaye mtakatifu.