Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema ameambukizwa Uviko-19 baada ya moja ya vipimo vitatu vilivyofanyiwa uchunguzi kubainika kuwa na virusi.

Museveni, ambaye alitoa hotuba ya hali ya taifa mapema Jumatano, alisema alijihisi kuwa na homa kidogo, hali iliyomfanya kupimwa.

Katibu wa kudumu katika wizara ya afya, Diana Atwine, alisema rais amepata dalili za mafua lakini yuko katika hali nzuri na ataendelea na majukumu yake.

Alisema rais atafuata taratibu za kawaida za kuzuia maambukizi ya ya Uviko wakati akitekeleza jukumu lake.

Uganda ilikuwa na baadhi ya nchi za barani Afrika zlizochukua hatua kali kudhibiti kusambaa kwa virusi wakati wa kilele cha janga hilo, ikiwa ni pamoja na amri ya kutotoka nje kwa muda mrefu na kufungwa kwa shule na biashara.

Nchi hiyo iliondoa vikwazo hivyo mwezi Februari 2022.