Mchana wa tarehe 31 Desemba 2023 kijijini Msoga wilaya ya Chalinze mkoani Pwani ukoo wa Kikwete walikuwa na sherehe kubwa ya jando na unyago.
Sherehe hiyo ilihusisha wavulana 11 na wasichana 7, wakiwemo watoto wa Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na ndugu zake.
Wavulana na wasichana hao waliotoka siku hiyo ni wajukuu wa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kaka zake na dada zake.
Sherehe hizo zilizofana sana kwa nyimbo na ngoma za kitamaduni zilifanyika baada ya vijana hao kumaliza takriban wiki mbili za mafunzo maalum kwenye kambi yao porini kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la Wakwere.
Kwa mujibu wa wanakijijij wa Msoga waliohudhuria sherehe hizo, Wakwere bado wanaendeza mila ya jando na unyago kwa wavulana na wasichana wao ili kulinda na kudumisha kwa vitendo mila na desturi zinazohakikisha mtoto au kijana wao, kabla ya kuingia katika umri wa ki-utu uzima, anapata maarifa au stadi za maisha zinazomfanya awe kijana shupavu, anayejitambua na anayewajibika kikamilifu katika jamii na taifa.