Mpendwa msomaji, ni katika hali isiyo ya kawaida leo nimelazimika kuandika makala mbili katika Safu hii ya Sitanii. Nimechukua hatua hii kutokana na uzito wa hoja hizi mbili. Mwanzo niliwaza kuzichanganya, lakini nikaona kila moja ina uzito wa ina yake.

Hapo juu nimezungumzia mchezo hatari unaokaribia kuligharimu taifa letu kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

Hapa nazungumzia hatari inayonyemelea ustawi na uwepo wa Muungano wetu. Nimesoma mapendekezo ya Rasimu ya Katiba kama ilivyotolewa na Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba. Nimeyaona mapendekezo juu ya kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.

 

Kwa wenye kumbukumbu, niliandika makala nyingi nikichagiza Serikali ya Tanganyika irejeshwe. Nashukuru Mungu yale niliyokuwa nikiyaandika, Tume ya Marekebisho ya Katiba imeyachukua na kuirejesha Serikali ya Tanganyika.

 

Katika hotuba ya kuzindua rasimu hii, Jaji Warioba alisema wameangalia uwezekano wa kuwa na Serikali moja, imekuwa vigumu, lakini pia wameangalia uwezekano wa kuwa na Serikali mbili, wakaona ingewezekana lakini baada ya kufanya mabadiliko makubwa, na wakaangalia Serikali tatu, wakaona angalau hizi zinaweza kuufanya Muungano ukaendelea kuwapo.

 

Katika rasimu ya mapendekezo, wanafuta cheo cha Waziri Mkuu, wanataka Serikali ya Muungano ibaki na Rais na Makamu wa Rais, wakiunda Baraza lenye mawaziri wasiozidi 15, na kati ya mawaziri hao akiwamo waziri mkazi (resident minister) kutoka kila upande.

 

Nimesoma mawazo ya Profesa Issa Shivji, nikayaunganisha na wasiwasi uliotanda miongoni mwa Watanzania. Baada ya kuunganisha hayo yote imenilazimu kujifungia kwenye chumba nikiwa peke yangu na kujaribu kufikiri tunawezaje kuwa na Muungano endelevu.

 

Kinachonivutia, hakuna kati ya wote wanaozungumza anayetaja kuvunjwa kwa Muungano. Sote tuna nia ya Muungano kuendelea kuwapo, ila unaendeleaje ndiyo tatizo letu la msingi.

 

Sitanii, baada ya kuchekecha yote hayo nimepata jibu mwafaka. Ikiwa kweli tunataka kudumisha huu Muungano, sasa nimuombe Jaji Warioba na wajumbe wake wafanye haya yafuatayo:-

 

Mosi, sisi Watanzania tuwe wa kwanza kubuni aina ya mfumo tunaoutaka katika Muungano wetu, badala ya kukumbatia mfumo wa Wamarekani. Mbili, tuunganishe mfumo wa Wamarekani, wa Rais na Mgombea Mwenza, ambaye ni Makamu wa Rais, sisi tuongeze iwe

 

Rais na Wagombe Wenza Wawili.

Hawa Wagombea Wenza, vyama vikiwateua ndiyo wawe marais wa Serikali za Tanganyika na Zanzibar.

 

Namaanisha nini? Kila chama kinapoingia kwenye uchaguzi kinakuwa na mgombea urais wa Muungano, ambaye anakuwa na wagombea wenza wawili; mmoja kutoka Zanzibar ambaye pia akishinda atakuwa Rais wa Zanzibar na mwingine kutoka Bara, ambaye naye akishinda atakuwa Rais wa Tanganyika.

 

Hapa tutarejea sawa na ilivyokuwa makubaliano ya Aprili 26, 1964 ambapo kulikuwapo Makamu wa Kwanza wa Rais, Sheikh Abeid Amani Karume na Makamu wa Pili wa Rais, Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwa maana nyingine, kama Karume alivyokuwa Rais wa Zanzibar, Kawawa naye angekuwa Rais wa Tanganyika.

 

Ninaupendekeza  mfumo huu ufanye kazi kama ifuatavyo:  Rais wa Muungano akitoka Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais atoke Bara na Makamu wa Pili wa Rais atoke Zanzibar. Rais wa Muungano akitokea Bara, basi Makamu wa Kwanza atoke Zanzibar na Makamu wa Pili atoke Tanganyika.

 

Utaratibu huu utatuwezesha kukwepa kigingi alichokitumia Mwalimu Nyerere kupendekeza mgombea binafsi. Kwamba ikitokea Rais wa Muungano akafariki, basi Makamu wa Kwanza chini ya utaratibu huu akaimu urais wa Muungano kwa miezi sita, kisha tuitishe uchaguzi.

 

Sitanii, huyu Makamu wa Kwanza akikaimu urais wa Muungano, atakuwa na haki ya kufanya hivyo (locus stand), kwani alipigiwa kura na watu kutoka pande zote mbili katika ngazi ya Muungano. Mapendekezo haya yasikupe hofu. Najua unajiuliza upigaji kura utakuwaje.

 

Hii inaweza kukupa shida kwamba eneo kama Zanzibar ikiwa watu hawa watapigiwa kura za jumla Tanzania nzima watasababisha ushindi bandia kwa ama Rais wa Zanzibar, au Rais wa Tanganyika. Hili nalo nimelifikiria.

 

Ninapendekeza hawa Makamu wa Rais kama wagombea wenza, watapigiwa kura mara mbili. Watapigiwa kura ya jumla wakati Rais wa Muungano anachaguliwa, lakini hawatashika wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais au Makamu wa Pili wa Rais hadi wawe wameshinda urais wa Tanganyika au wa Zanzibar.

 

Hii ina maana kuwa Rais wa Zanzibar au Rais wa Tanganyika, katika wadhifa huu atapigiwa kura na Wazanzibari au Watanganyika peke yao. Kwa maana hiyo, ikitokea katika hatua hii atakayeshinda ama Tanganyika, au Zanzibar akatoka chama tofauti na aliyeshinda urais wa Muungano, kwa kuwa vyama vyote wagombea wa Zanzibar na Tanganyika watakuwa wamepigiwa kura nchi nzima kama wagombea wenza katika ngazi ya Muungano, basi ataapishwa kuwa Makamu wa Rais, ama wa Kwanza, au wa Pili.

 

Kwa mfano, ikiwa CUF watashinda urais Zanzibar kupitia Maalim Seif, lakini Serikali ya Muungano Profesa Lipumba akashindwa na mgombea wa CCM au Chadema, basi huyu Maalim Seif ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, na siku anaapishwa Rais wa Muungano, kama ametoka Bara ataapishwa pia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini ikiwa aliyeshinda urais wa Muungano anatokea Zanzibar, basi huyu Maalim Seif ataapishwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais.

 

Hapo juu niligusia suala la kurejea kwenye uchaguzi miezi sita ikitokea Rais wa Muungano amefariki. Nimependekeza hivyo kwa sababu moja tu ya msingi, kuwa inawezekana ama Tanganyika, au Zanzibar wakashinda wagombea wa vyama tofauti.

 

Inawezekana pia nchi ikawa na marais watatu kutoka vyama tofauti. Wa Muungano anaweza kutoka Chadema (kwa mfano) wa Tanganyika akatoka CCM na wa Zanzibar akatoka CUF. Mwisho wa siku hawa wote siku Rais wa Muungano anaapishwa, wataapishwa kushika umakamu wa Muungano kwa utaratibu nilioueleza hapo juu.

 

Sababu ya kukaimu miezi sita ni kwamba si haki Rais anayetoka kwa mfano CCM akifariki, basi Makamu wa Kwanza wa Rais kama anatokea CUF au Chadema, akapanda pale juu na kuwa Rais. Ridhaa ya wananchi inaweza isiwepo. Ila kukaimu kwa miezi sita si tatizo, maana hata Mzee Nelson Mandela aliwahi kumkaimisha mpinzani wake mkuu, Chifu Mangusuthu  Butelezi na mambo yakaenda bila tabu.

 

Sitanii, imenichukua siku zaidi ya nane na saa mbili kuwaza na kupata ufumbuzi wa tatizo hili. Ikiwa mapendekezo yangu yamekuchanganya, usihofu. Funga breki, yapitie makala haya kwa mara ya pili. Hata mimi ilinipa shida kupata ufumbuzi huu, hivyo isome tena na tena utaielewa na kuikubali.

 

Mwisho, ni kwamba nia ya Rais wa Zanzibar na Tanganyika kuwa makamu wa Rais wa Muungano, ni kumpatia mamlaka si tu ya kisheria, bali ya kimaadili (moral authority) Rais wa Muungano juu ya pande hizi mbili; Zanzibar na Tanganyika, bali pia kudumisha umoja.

 

Lakini pia hawa marais wa Tanganyika na Zanzibar, nia ya kutaka wawe wagombea wenza na kupigiwa kura nchi nzima katika ngazi ya urais wa Muungano, ni kuwapa mamlaka ya kukaimu hiyo miezi sita wakati wanasubiri kuitisha uchaguzi ikiwa Rais wa Muungano atakuwa amefariki.

 

Pia huyu anayekaimu urais, itamkwe bayana kuwa hatakuwa mgombea urais wakati anashikilia urais wa Zanzibar au Tanganyika. Akitaka kufanya hivyo, ajiuzulu kisha agombee. Akijiuzulu taifa anakotokea – Zanzibar au Tanganyika – nalo litafanya uchaguzi wa rais wao. Huyu mgombea urais wa Muungano baada ya hiyo miezi sita, atapaswa kusimama na wagombea wenza sawa na ilivyokuwa katika uchaguzi uliomweka madarakani aliyefariki.

 

Kwa ufupi, vyama vyote vitakuwa na wagombea wenza wawili kwenye urais wa Muungano. Rais wa Muungano akishinda, wagombea wenza wataapishwa kushika wadhifa wa umakamu ikiwa tu wameshinda ama urais wa Zanzibar, au urais wa Tanganyika.

 

Wakishindwa ama wote, au mmoja wao, aliyeshinda urais wa Tanganyika au Zanzibar hata kama anatoka chama tofauti na aliyeshinda Muungano, kwa kuwa alikuwa mgombea mwenza wa mgombea wa chama chake katika Muungano, tayari anayo mamlaka kisheria aapishwe kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kwa kufuata utaratibu nilioueleza hapo juu.

 

Zanzibar wametufunza jambo katika hili. Maalim Seif Shariff Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais (CUF) na Balozi Seif Iddi (CCM) ni Makamu wa Pili wa Rais, na bado Serikali ya Umoja wa Kitaifa inakwenda. Masuala ya ndani ya Zanzibar au Tanganyika, wananchi wanaweza kuchagua chama wanachodhani kitayaendesha vyema.

 

Majukumu ya Serikali ya Muungano yataainishwa na hivyo hawa watatu, Rais wa Zanzibar, Rais wa Tanganyika na Rais wa Muungano, lao liwe moja kuelekea jamii ya kimataifa. Ndiyo maana Rais Barrack Obama wa Marekani anakuja na ujumbe wa watu 700 Tanzania mwezi Julai, wote wanajiita Wamarekani.

 

Hutasikia Mmarekani akikwambia yeye ni Mnew York, Mflorida au Mwoshington. Wakitoka nje wanakuwa Wamarekani, ila wanaingia mikataba kwa ajili ya majimbo yao 50. Huwezi kusikia mtu akijitaja kwa jimbo lake. Hata sisi tupige marufuku Mzanzibari au Mtanganyika kikatiba kwenda nje ya nchi akajitangaza kama Mtanganyika au Mzanzibari. Ajinadi kama Mtanzania.

 

Atakayekaidi, anyang’anywe hati ya kusafiria. Naamini tukiwa na mfumo huu, hata malalamiko yaliyokuwa yanatolewa na Wazanzibari kuwa Rais wa Zanzibar alienguliwa kimamlaka na mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Tanzania kwa kumfanya asiwe Makamu wa Rais wa Muungano yatakuwa yamekwisha.

 

Tutabaki na Tanzania moja, Tanzania imara na makamu wa marais wote wawili watakuwa na mamlaka sehemu zote mbili za Muungano na Muungano wetu utaimarika zaidi. Nipo tayari kufafanua mbele ya Tume pendekezo hili, ikiwa itawapendeza.