Jumamosi iliyopita nilikuwa jijini Arusha. Nikiwa nimeegesha gari kwa ajili ya kupokea simu, nikamwona mama aliyeonekana mwenye mawazo mengi. Hakuwa na furaha usoni. Hapa ni jirani na Uwanja wa Ndege wa Kisongo. Sikuhitaji kumuuliza maswali mengi. Nilichofanya baada ya kumtazama, nilimwita. Akasogea akionekana mwenye shaka nyingi.
Nilimuuliza anakokwenda. Akajibu kuwa anakwenda Soko la Kilombero ambako anauza mbogamboga. Kwa namna nilivyomwona miguuni akiwa amejaa vumbi, yaliyonijia akilini ni kuwa mama huyu hakuwa na nauli ya kumwezesha kufika huko alikokuwa akienda. Kutoka pale Kisongo hadi Soko la Kilombero ni mwendo wa kilometa kadhaa.
Alipoingia ndani ya gari nikataka kujua ni wapi alikokuwa akitoka. Akanijibu kuwa alikuwa akitoka Gereza la Kisongo kumwona mwanae, Gerald Silvanus Sambayuka, mwenye umri wa miaka 23. Huyu mama anaitwa Hawa, na ndiye mama mzazi wa Gerald.
Nikamdadisi mama yule sababu za mwanae kuwekwa rumande, naye akasema alikamatwa Mei, 2017. Anasema Gerald ni dereva wa bodaboda. Siku alipokamatwa alikuwa na mteja. Walipofika kwenye maduka, yule mteja akaomba asimame ili akapate mahitaji ya nyumbani. Anasema wakati akimsubiri yule mteja wake, wakatokea polisi na kumkamata Gerald.
Anasema alijaribu kuuliza ni sababu gani za kukamatwa kwake, lakini polisi wakamzaba vibao na kumtaka anyamaze. Baadaye akiwa polisi anadai kuwa akaambiwa kosa lake ni la unyang’anyi wa kutumia silaha; na kwamba alishiriki tukio hilo siku kadhaa zilizopita! Kulia kwa Gerald hakukumsaidia kitu.
Akapelekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi, Arusha. Akawekwa rumande kwa mwezi mmoja na nusu bila kufunguliwa mashtaka!
Mama Hawa anasema baada ya mwezi mmoja na nusu ndipo Gerald alipofikishwa mahakamani na wenzake, lakini baadaye waliachiwa na akabaki Gerald. Tangu mwaka 2017 amekuwa akipelekwa mahakamani, lakini kwa maelezo ya mama yake ni kwamba kesi imekuwa ikitajwa tu. Hajapata kuambiwa mlalamikaji ni nani! Mara zote upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika! Hakuna mtu aliyejitokeza kulalamika kuwa Gerald kweli alishiriki uporaji huo wa kutumia silaha.
Kadiri mazungumzo yalivyoendelea, Mama Hawa alianza kutokwa machozi, hasa akikumbuka kuwa Gerald ndiye mtoto wake wa kwanza; na kwa umri wake kama angekuwa huru angemsaidia kwenye mapambano ya maisha. Baba Gerald alikwisha kufariki dunia. Hana msaada wowote zaidi ya kuuza mboga na kumhudumia Gerald aliyeko mahabusu kwa karibu mwaka wa tatu sasa.
Kilio cha Mama Hawa kilikolea hasa pale aliposema amekwisha kwenda polisi mara kadhaa na kuambiwa atafute shilingi milioni mbili ili mtoto wake afutiwe kesi. Sina hakika na madai haya, lakini haya si mambo ya kushangaza kuyasikia kutoka kwa baadhi ya polisi wetu.
“Baba, [akiwa amenyanyua mikono kama mtu anayeomba msaada] mimi nitoe wapi shilingi milioni mbili? Niuze mboga malori mangapi hadi nipate hizo hela?” Aliuliza kwa mshangao.
Nilipokaribia Soko la Kilombero, Mama Hawa aliomba ashuke; lakini kabla hatujaagana nikamwomba namba yake ya simu. Akanipa. Ninayo. Kwa mamlaka zinazohusika endapo zitaihitaji nitawapa.
Simulizi hii ya Mama Hawa, japo ni maneno yasiyo na uthibitisho wa moja kwa moja, inabeba vimelea vya kuwapo jambo lisilo la haki. Majuzi tu, tumesikia kazi kubwa ya kijasiri iliyofanywa na Rais John Magufuli, kupitia kwa DPP. Mwananchi mmoja mkoani Tabora alibambikiwa kesi, lakini baada ya maagizo ya Rais Magufuli, ikabainika kuwa kweli mwananchi yule alionewa.
Malalamiko ya aina hii ya kina Mama Hawa na mtoto wake Gerald ni mengi mno. Kesi za mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na ugaidi sasa ndiyo fasheni. Watu wanyonge wanaonewa mno.
Malalamiko haya yapo maelfu kwa maelfu katika magereza na mahabusu zote nchini mwetu. Kwa wingi wake, hayawezi kumalizwa na Rais Magufuli kwa kusikiliza ‘kesi’ moja moja. Ni mengi mno. Kuna mamia kwa maelfu ya Watanzania maskini – wanyonge – makabwela wanaoteseka magerezani bila kuwa na chembe ya hatia.
Magereza na mahabusu zimejaa hadi pomoni kwa kesi nyingi za kutungwa na wala watu hawana hofu ya Mungu. Tuna binadamu wenzetu wanaoteseka kwa sababu tu ya unyonge wao. Hakuna aliyependa azaliwe katika mazingira ya unyonge.
Wapo Watanzania mamia kwa maelfu walionyimwa dhamana kwa makosa au tuhuma zinazostahili dhamana. Matokeo ya uamuzi huo ndiyo haya tunayoona leo ya kujaa kwa magereza na mahabusu zote nchini.
Tukio la Tabora limewagusa wengi wenye ndugu magerezani na mahabusu. Hawa wangependa kuona wakitendewa haki kama mwenzao wa Tabora.
Kama nilivyosema awali, kuiacha kazi hii kwa Rais Magufuli pekee ni jambo la kumwonea. Anaweza kupokea makontena ya malalamiko.
Tunavyo vyombo vya kikatiba na kisheria vya kushughulikia mambo ya aina hii ili kuondoa uonevu katika taifa letu. Tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, tuna vyombo vingi vya kusimamia masilahi na haki za wananchi.
Tunao viongozi, kuanzia kwa waziri wenye mamlaka ya kuchunguza malalamiko haya. Lakini tukiri kuwa, ama sheria zetu hazivipatii vyombo hivi nguvu zinazostahili, au wenye dhima hiyo wameamua kukaa kimya, maana wanaoumia bila hatia si ndugu au jamaa zao. Bodi ya Parole sijui kama ina ubavu wa kukabiliana na hali hii kwa wafungwa.
Kwa hali ilivyo, napendekeza kwa Rais Magufuli, kwa mamlaka aliyonayo kama kiongozi wetu mkuu wa nchi, aone uwezekano wa kuunda chombo maalumu chenye wataalamu wa sheria na haki za binadamu – kitakachopita katika mahabusu zote nchini kusikiliza malalamiko ya waliowekwa humo.
Mahabusu wanaoamini kuwa wameonewa wapewe uhuru wa kuandika malalamiko yao. Yakusanywe. Yapitiwe na jopo la wanaounda chombo hicho. Wayapime na kutoka miongoni mwayo waone mangapi “yanayokaribiana na ukweli”. Wayachukue, wawaite wahusika ili wajieleze mbele yao. Kwa kufanya hivyo ukweli utabainika. Tunaambiwa wapo hadi mahabusu ambao ni wagonjwa wa akili. Wako rumande kwa miaka sasa. Hao wapelekwe kunakostahili wakatibiwe.
Chombo hicho kiwe na majaji wastaafu na wataalamu wengine wa masuala yanayoendana na kusudio la kuundwa kwake na kiwezeshwe kwa hali na mali kwa ajili ya kupata ukweli utakaosaidia kuwaokoa Watanzania na wasio Watanzania wanaoozea mahabusu kwa kuonewa.
Zipo taarifa zisizotiliwa shaka kwamba kuna watuhumiwa walioko mahabusu kwa miaka minane au 10 kesi zao zikiwa “hazijulikani”. Watu wa aina hiyo ni rahisi kubainishwa na kusaidiwa.
Naamini kwa dhati kabisa kuwa endapo tutakuwa na chombo cha aina hiyo kitaifa, mambo mengi mabaya ya uonevu dhidi ya binadamu wenzetu yataibuliwa na watu wengi wataokolewa. Jela au mahabusu si mahali pa mtu kupelekwa kwa uonevu.
Tanzania ni nchi huru. Viongozi wetu wanaapa kulinda haki za watu na masilahi ya nchi. Katika hali hiyo hatuwezi kuendelea kukaa kimya ilhali wapo wenzetu wanaoteseka bila hatia yoyote.
Matamko ya kukemea ubambikiaji kesi yanayotolewa na viongozi hayawezi kupunguza wala kumaliza tatizo hili. Lililo la msingi ni kwa chombo ninachopendekeza kuingia mahabusu zote kufukua vilio vya kweli vya wanadamu wanaoteseka kwa ghiliba na husuda za wenye madaraka.
Kwa pamoja tuifanye Tanzania iwe mahali pazuri kwa kila binadamu kuona fahari na raha ya kuishi kwa uhuru na haki. Rais Magufuli ukilifanya hili utakuwa umewatendea haki maelfu ya wanyonge walio mahabusu na ndugu wanaokosa huduma zao. Kwa kufanya hivyo utaandikwa kwenye vitabu vya historia njema ya taifa letu.