Lowassa pembaRais John Pombe Magufuli alipohutubia mkutano wa hadhara alioufanya Manyoni, amenukuliwa akisema; “Hao wanaotaka kuandamana wataona. Nawaomba watangulie wao wawe mstari wa mbele, wasitangulize watoto wa maskini na wao kujificha hotelini mimi sijaribiwi.”

Hii ni kauli ya hatari inayoashiria Amiri Jeshi Mkuu akitangaza vita dhidi ya wananchi wasiokuwa na silaha. Tumuulize Rais Magufuli anawataka watangulie ili awaonyeshe nini?

Rais Magufuli akijaribiwa yuko radhi kuwapatililiza hao wanaomjaribu? Hii ni kauli ya kujikweza, kwani Rais Magufuli akiwa binaadamu hawezi kuepuka majaribu. Asiyejaribiwa ni Mungu peke yake. Ndio maana hata Mwokozi wetu Yesu Kristu alijaribiwa.

Rais angesema tuombe Mungu atuepushe na jaribu hilo, maana tangu aapishwe kuwa Rais amewahamasisha Watanzania kumtanguliza Mungu, ila kuhusu maandamano haonyeshi kumtanguliza Mungu bali ametanguliza jazba.

Kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pale Dodoma alitoa kauli tata akimsifia Kikwete kuwa mvumilivu, kwani angekuwa yeye ndiye Mwenyekiti wajumbe wa Mkutano Mkuu walioimba “Tuna imani na Lowassa” Hajui ingekuwaje?

Rais Magufuli hatambue kwamba Mwenyekiti ni mkubwa kwa mjumbe mmoja mmoja, lakini Mkutano Mkuu katika ujumla wake, ndio bosi wa

Mwenyekiti, kwani ndio unaompa uenyekiti na una mamlaka juu yake.

Si vyema, Rais Magufuli kuufananisha Mkutano Mkuu na Baraza la Mawaziri, ambalo anaweza kutengua uteuzi wa Waziri, lakini kwenye chama hana uwezo wa kutengua ujumbe wa yeyote. Kumbe anapojiapiza kwamba sijui ingekuwaje, anadhani hata leo wakirudia atawafanya nini?

Anapowataka “hao” watangulie mbele wasiwatangulize watoto wa maskini awaonyeshe, amekusudia kutoa fundisho kwa Watanzania, kwamba watakapoyaona madhara yanayowakuta waandamanaji (ambao Rais Magufuli amewakamia), wananchi wengine hawatathubutu tena kuandamana!

Hili litakuwa funzo baya linaloweza kuzaa matokeo asiyotarajia. Somo analotaka kulitoa Rais Magufuli limelenga kuwajengea wananchi hofu na woga ule ule ambao Serikali za Kikomunisti ziliwaumbia raia wake. Rais atambue kwamba wananchi wanatawaliwa kirahisi, hawahitaji kuogopeshwa, kinachotakiwa ni Rais wao kuheshimiwa siyo kuhofiwa.

Pili Rais Magufuli aelewe haki inayomwezesha kuzunguka Manyoni, Singida na Nzega, akifanya mikutano ya hadhara kuwashukuru wananchi waliomchagua, ni haki hiyo moja ndiyo walionayo Edward Lowassa, Freeman Mbowe na wanasiasa wengine.

Kwa hiyo asiwaonyeshe Watanzania kwamba akiwa kama Mwenyekiti wa CCM haki yake inaanzia pale zinapoishia haki za wanasiasa wa vyama vingine. Akifanya hivyo atachochea sintofahamu nchini.

Tatu Rais Magufuli atambue kwamba Watanzania wanaomkusanyikia kwenye mikutano ya hadhara anayoifanya ndio watakaoandamana siku wakienda Mbowe na Lowassa. Asituaminishe kwamba Watanzania wakikutanishwa na CCM wanaongezeka thamani hadi wanastahili kulindwa, lakini Watanzania hao wakikutana kwa jina la CHADEMA wanakosa thamani kiasi cha kustahili kupigwa mabomu.

CHADEMA haina Watanzania wake tofauti na hao wanaomkusanyikia Mheshimiwa Rais. Nasihi Rais Magufuli ulitafakari dua la Mfalme Suleiman na dua lililo kwenye wimbo wetu wa Taifa. Suleiman aliomba akisema “Ee Mungu wangu nipe hekima ili nitawale kwa haki, nijaalie maarifa nijue jinsi ya kutoka na kuingia, maana ni nani awezaye kuongoza kwa haki watu wako walio wengi kama mchanga wa pwani?”

Katika wimbo wetu wa Taifa tunaomba “Mungu aibariki Afrika, awabariki viongozi wake, hekima umoja na amani, hizi ni ngao zetu (yaani ndio kinga yetu), Afrika na watu wake.” Rais Magufuli afahamu hapa duniani sisi hatujilindi kwa nguvu za nyukilia wala kujihami kwa makombora ya masafa marefu kama Marekani na Russia, bali ngao zetu ni “hekima umoja na amani”

Mambo hayo matatu ndio mafiga yanayoibeba Tanzania, kwa hiyo Rais Magufuli ataivunja ngao ya umoja endapo ataifanya Tanzania yetu iwe na “wao” au “hao” wanaopaswa kupigwa na “sisi” tunaopaswa kulindwa.

Zikiwepo vurugu badala ya amani maana yake figa la tatu litakuwa limeharibiwa Tanzania haitasimama. Kupitia wimbo wetu wa Taifa tunaomba “Mungu aibariki Tanzania, dumisha uhuru na umoja, wake kwa waume na watoto.” Maana yake, uhuru unaweza kudumishwa kwa kuendelea kuwako ama kukomeshwa, usiweko tena uhuru wa kujumuika, uhuru wa kukosoana na uhuru wa kutofautiana.

Ngao yetu ya taifa ina picha ya Adamu na Hawa, wakishirikiana kufanya kazi pamoja. Chini yao kuna maneno mawili; uhuru na umoja. Haya si madogo. Yana maana yake halisi na tafsiri iliyo pana ndiyo maana tunayaomba kila mara. Tunapomsihi Mungu kudumisha uhuru na umoja, kwa wanawake, wanaume na watoto tunamaanisha mshikamano.

Tanzania inaundwa kuwa kitu kimoja kizima kutokana na makundi haya, waume, wake na watoto. Kwa hiyo Rais Magufuli atakapowashughulikia waandamanaji ajue madhara yatakitokea lazima yawaguse wanawake, wanaume na watoto. Hapo hautakuwepo umoja kati ya waliojeruhi na hao waliojeruhiwa.

Kwenye Tanzania moja yakiumbwa makundi ya “wao” au “hao” na “sisi” utakuwa ndio mwanzo wa kulimong’onyoa taifa maana, Tanzania inaundwa na mshikamano wa waume, wake na watoto.

Mfalme Suleiman alipoomba hekima ili imwezeshe kutenda haki kwa kufanya maamuzi sahihi, alimsisimua Mwenyezi Mungu ambaye kwa asili yake ni Mungu wa haki. Mungu alifurahi kusikia Mfalme anataka haki ndiyo itawale kwenye maisha ya watu. Anaowaongoza, akamwambia hata yale usiyoyaomba nimekupa utajiri, fahari, heshima na utukufu.

Hekima ni uwezo wa mtu kutumia kile anachokifahamu (the ability to use knowledge). Kumbe Suleiman alipoomba Mungu ampe hekima na maarifa ajue jinsi ya kutoka na kuingia maana yake halisi ni kwamba mtu akijua jinsi ya kuanza na jinsi ya kumaliza atapata suluhisho.

Kwa sababu mtizamo potofu (wrong concept), unazaa tafsiri iliyopotoka, nayo tafsiri potofu, inazaa namna potofu, hiyo namna

Potofu, inahitimisha kwa kutoa matokeo mabaya, ambayo mwisho yanaumiza wananchi.

Umuhimu wa hekima aliyoomba Mfalme Suleiman kwa Mungu wake ulionekana kwenye suala gumu na tete la makahaba ambalo kwake lilikuwa jaribu la aina yake dhidi ya ufalme wake, sawa na jaribu la waandamanaji dhidi ya utawala wa Rais Magufuli.

Makahaba wawili walifikishana kwa Mfalme wakigombea mtoto mmoja aliye hai huku wote wakimsusa aliyekufa. Mfalme Suleiman angekuwa mbabe na asiyethamini haki angewajibu kwa hasira kwamba “enyi malaya msiniletee mambo yenu ya kikahaba ondokeni.”

Lakini Suleiman alijua hata makahaba walio nchini mwake wanastahili kutendewa haki, vivyo hivyo Rais Magufuli aelewe kwamba ikiwa makahaba walisikilizwa na haki ikatendeka, yeye pia anapaswa kuwasikiliza waandamanaji na kuwatendea haki hata kama haupendi utamaduni wao wa kuandamana.

Imeandikwa, “Nao Waisraeli waliposikia habari ya hukumu ile walimwogopa Suleiman kwa sababu waliona dhahiri hekima ya Mungu iko juu yake kumwezesha kutoa hukumu na kuwaongoza katika haki.” Hapa neno kuogopa linatumika kumaanisha kuheshimu na kumkubali, yaani watawaliwa walimheshimu na kumkubali (appreciate) Mfalme wao, baada ya Suleiman kuwadhihirishia kwamba anayo sifa ya ziada katika kushughulikia masuala magumu.

Rais Magufuli atambue kwamba matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya raia na yanayoishia kusababisha madhara kama ya kuua ama kujeruhi, humpunguzia mkubwa uhalali wa kutawala. Mkubwa akikosa uhalali wa kutawala hujitengenezea mwenyewe kifo cha kisiasa. Ataanza kwa kuua watu, lakini baadaye kitafuatia kifo cha utawala wake.

Hayo ndiyo yaliyomkuta Chausesco, mtawala wa Romania ambaye wananchi waliokata tama walilala barabarani wakisema vifaru vipite juu ya migongo yetu, lakini hatuutaki utawala wako. Rais Magufuli hajafika huko, ila kasi aliyonayo asipofunga breki, treni ya mwendokasi inaelekea mkondo huo.

Hapa Afrika ikamtokea Musa Traore aliyekuwa Rais wa Mali. Aliagiza maaskari wawashughulikie waandamanaji kikatili, maaskari wakawamiminia watu risasi za moto, lakini haikusaidia. Ninatoa mifano hii si kwa nia mbaya, bali kumkumbusha Rais wetu, kuwa ubabe na matumizi ya nguvu tangu enzi havijawahi kuwa na ufanisi.

Nampa ushauri wa bure Rais Magufuli kwamba aachane kabisa na mawazo ya kutumia nguvu dhidi ya wanaotaka kuandamana kwa sababu nchi hii ina vijana wengi waliokata tama (the desperate), ambao mwanamapinduzi Carl Marx alisema hawana la kupoteza isipokuwa minyororo yao ya utumwa.

Watu wa aina hiyo yaani wasiokuwa na chochote cha kupoteza maishani, kwa maana kuwa hawamiliki nyumba, shamba, gari au baiskeli, hawastahili kuchokozwa. Wala si watu wa kupambana nao. Rais Magufuli amenukuliwa akisema watu walizoea kubembelezana, inaonyesha yeye hayuko tayari kuudumisha utamaduni wa kubembelezana.

Anaweza kuwa sahihi kwa walioajiriwa haifai kuwabembeleza ila hilo lisielekezwe kwa waliokata tamaa kwani wakichokozwa watapagawa na wakipagawa hatima inaweza kutokuwa nzuri.

Ipo sayansi nyepesi ambayo Rais Magufuli akiitumia kuwashughulikia waandamanaji atazuia maafa. Kwanza amwelewe mwandamanaji ni mtu wa namna gani na ana nini mkononi mwake. Mtu anayetembea kutoka eneo moja kwenda eneo jingine akiwa hana silaha yoyote hata jiwe, hakuna haja kwa askari mwenye silaha kukabiliana naye kwa lengo la kumzuia asitembee kutoka eneo A kwenda eneo B.

Rais Magufuli anaweza “ku- pre empty” maandamano yao kwa kuwaambia wanaoyaongoza wajulikane na washirikiane na Polisi kuhakikisha waandamanaji hawaleti madhara kwa wananchi wengine. Watakapoanza kuandamana waanzie eneo rasmi litakalotambuliwa na Polisi na waishie uwanjani unakofanyika mkutano wao wa hadhara.

Badala ya nguvu iliyopo kutumika kupambana na maandamano nguvu hiyo itumike “kuya-monitor” kuepusha maafa. Kinachotakiwa maandamano yasichukue sura nyingine ya uporaji au uharibifu wa mali, vinginevyo kama wafuasi wa CHADEMA wataandamana kutoka Kinondoni au Ilala hadi Jangwani kuna ubaya gani wa kumshitua Rais hadi ashawishike kupambana nao?

Mwisho, Magufuli aelewe hakuna mwenye uwezo wa kuandamanisha Watanzania kila siku, kila wiki na kila mwezi kwa sababu watu hawataacha shughuli zinazowapatia riziki wabakie kushughulikia maandamano tu. Kwahiyo hao wanaotaka kuandamana ifikapo Septemba Mosi, awaache wazime kiu yao.

Rais Magufuli anayo nafasi ya kujenga uchumi huu kwa kupambana na kazi ya kujenga viwanda, badala ya kujiingiza kwenye siasa za kuzuia maandamano zisizo na tija. Tupambane kujenga uchumi bila kufuta uhuru wa watu kutoa mawazo kwa kukosoa wanapodhani jambo fulani haliendi sawa.

 

Mwandishi wa Makala hii, Mwinjilisti Kamara Kusupa ni msomaji mzuri wa gazeti na JAMHURI na anapatikana kwa Na 0786 311 422.