Mwezi mzima wa Oktoba tumeadhimisha na kushiriki kwenye makongamano mbalimbali ya kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa.
‘Vumbi’ la makongamano na maneno mengi kwenye vyombo vya habari, mitandaoni na vijiweni sasa limetulia, lakini limeacha mambo ya kufikirisha.
Naamini litakuwa jambo jema Watanzania tukibadili mtindo wa kumuenzi Mwalimu Nyerere ili sote tunaothamini kazi nzuri aliyoifanya kwa taifa letu, Afrika na dunia tuanze kuyatekeleza yale aliyotufundisha kwa vitendo, badala ya kumuenzi kwa maneno kwenye kumbi zenye viyoyozi. Tutoke twende mitaani na vijijini tushiriki kufanya kazi za maendeleo kama Mwalimu alivyokuwa anafanya.
Kwenye shughuli za aina hiyo Mwalimu alikuwa haendi kujionyesha tu kwamba anashiriki. Alipanga kushiriki kikamilifu, alivaa ‘nguo za kazi’, alishika jembe na kulima pamoja na wananchi, alibeba mawe na matofali kujenga madarasa, kujenga zahanati, alishika sururu kuchimba mitaro na visiki. Alipanda miti mingi sana. Hakufanya geresha ya kutandikiwa mkeka asichafuke ili apande mti mmoja tu!
Pia vijana wetu wajifunze juu ya uongozi wake uliotukuka na wahimizwe kuyaishi maisha ya Mwalimu ya uzalendo na uadilifu ili na wao waje wawafundishe vizazi vijavyo. Hapo tutakuwa tunamuenzi Mwalimu barabara!
Nampongeza sana Rais wetu Dk. John Magufuli kwani katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake amedhihirisha wazi na kujipambanua kwamba yeye anamuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo. Ni dhahiri kwamba alikuwa na mapenzi makubwa kwa uongozi na utendaji uliotukuka wa Mwalimu Nyerere.
Wanaomfahamu Rais Magufuli kabla hajawa rais, wanasimulia jinsi alivyokuwa akipenda sana kusikiliza hotuba za Mwalimu na kusoma maandiko yake. Kwa hiyo alipoingia kwenye siasa na kuwa mbunge mwaka 1995 na kuchaguliwa kuwa naibu waziri na baadaye waziri kamili, alijipambanua kuwa ni mzalendo wa kweli, aliyeamua kuitumikia nchi yake kwa moyo. Utendaji wake ulikuwa tofauti.
Kwake yeye “hapa kazi tu” ilidhihirika tangu alipoanza kushika nafasi hizo za uongozi. Alidhihirisha kuwa mfuasi wa kweli wa Mwalimu Nyerere na siasa zake.
Hakuna ambaye hakumbuki jinsi nchi yetu ilivyokuwa imepoteza mwelekeo kabla hatujaingia kwenye kipindi cha Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Huko nyuma wakati Baba wa Taifa letu alipokuwa hai, alikuwa akiombwa akemee pale Watanzania wenye kuitakia mema nchi yao walipoona mambo hayaendi sawa. Baada ya kifo chake, wapo walioona kama wamepata ruksa ya kufanya watakavyo! Matokeo yake, wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 Watanzania walipaza sauti zao kutaka yawepo mabadiliko ili nchi irudishwe kwenye mstari.
Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, ambaye aliwahi kuhojiwa na Gazeti la JAMHURI kuhusu uongozi wa nchi mwaka ule wa 2015, alisema Watanzania wanahitaji kupata mtu ambaye anaonekana ana malengo ya kutumikia wananchi, siyo kula.
Akaongeza: “Tunataka tupate mtu mwenye mwelekeo wa ki-Nyerere Nyerere hivi. Mwadilifu, asiye mlaji wa mali ya umma, asiye na ubinafsi, asiye na upendeleo…. Mtu mwenye kuamua na kukabiliana na matatizo kulingana na wakati uliopo.” Akasema: “Tuombe Mungu tupate kiongozi mwenye ‘zero tolerance’ (asiyevumilia) ufisadi, rushwa na kadhalika… Mtu yeyote anayeshughulika na rushwa asihurumiwe kabisa…!”
Waziri Mkuu mstaafu Msuya akatuasa Watanzania akisema: “Tusije tukaweka jambazi au fisadi awe kiongozi wetu! Nchi itapasuka kama Nigeria au DRC wakati wa Mobutu.”
Sote tunafahamu kazi kubwa aliyofanya Rais Magufuli na timu yake kwenye kampeni hadi akapata ushindi. Pia tunafahamu alianzaje kazi alipoingia Ikulu. Baada ya kuapishwa tu, akaanza kazi hata kabla hajateua Baraza la Mawaziri. Alifanya ziara za kushitukiza kwenye wizara. Kitendo hicho kilifikisha ujumbe kwa watumishi wa serikali kwamba rais tuliyempata hana mchezo, hatavumilia wazembe na wategaji kazini.
Rais alikwenda kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kuona wagonjwa walivyokuwa wakilala ‘mzungu wa nne’ kwenye kitanda kimoja na wengine wengi wakiwa wamerundikana sakafuni. Akaagiza vitanda, magodoro na mashuka vinunuliwe haraka na kupelekwa Muhimbili na kwenye hospitali zote nchi nzima.
Kwa hatua mbalimbali alizoanza kuchukua alipoingia Ikulu tayari alianza kudhihirisha kwamba anaguswa na matatizo ya kiutendaji yaliyokuwepo nchini, anaguswa na huduma duni za kijamii na anaguswa sana na shida za wananchi. Wenye macho wakatamka: “Tunamuona Nyerere ndani ya Magufuli!”
Hata Baraza dogo la Mawaziri alilolitangaza baada ya mwezi mmoja tangu achaguliwe, na hatua zingine mbalimbali alizochukua vilitoa ujumbe kwamba alikuwa amedhamiria kubana matumizi na kuijenga Tanzania.
Kwenye hotuba yake ya kwanza aliyoitoa bungeni Rais Magufuli alisema: “…Katika mipango yetu tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu. Mambo tuliyoahidi tutatekeleza; ahadi ni deni. Sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi…”
Rais alitoa orodha ya mambo makubwa ambayo serikali yake ilidhamiria kuyafanya kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla. Miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli sote tumeona jinsi ambavyo amekuwa akitekeleza ahadi zote alizotoa kwa wananchi kwenye kampeni za uchaguzi mwaka ule wa 2015.
Jingine kubwa ambalo ninaamini alikuwa amekwisha kupanga, ni namna gani angeshughulika na uchumi wa nchi. Alielewa wazi kwamba Mwalimu alikuwa sahihi katika kujenga viwanda vya kila aina nchini. Tulichotakiwa Watanzania kufanya ni kuweka uzalendo mbele na ‘kukomaa’ tu ili kuviendeleza kwa gharama yoyote ile. Lakini yaelekea uzalendo ulitushinda, vikauzwa kimoja baada ya kingine ama tukaacha vikafa.
Rais Magufuli kwa ujasiri mkubwa alitangaza kuwanyang’anya viwanda wale ambao hawakuviendeleza, akaanza kuvifufua vilivyokufa na kuweka mikakati ya kujenga vingine vingi. Ndani ya miaka minne tu, nchi yetu ina viwanda takriban elfu nne na vingine vinaendelea kujengwa.
Ili viwanda vifanye kazi ipasavyo na visije vikafa tena, Rais Magufuli alikwisha kupanga pia kuwa atahakikisha unakuwepo umeme wa uhakika – akaendeleza Kienyerezi I na kuanzisha ‘vinyerezi’ vingine II hadi IV. Akawadhibiti walioweka mirija yao kwenye miundombinu ya umeme. Akawataka wafanyakazi wa TANESCO wafanye kazi kwa uadilifu na watoe matokeo chanya kwenye utoaji wa huduma hiyo.
Ndani ya miaka minne umeme wa uhakika upo nchini kote hadi vijijini. Yale majenereta wananchi waliyokuwa wanalazimika kununua yatumike kila umeme unapokatika, hivi sasa yanatumika kama meza ndogo (stuli) majumbani!
Kama hili la umeme wa uhakika halitoshi, na kwa kuwa Rais Magufuli alikuwa shabiki na mwanafunzi ‘binafsi’ wa Mwalimu Nyerere, hakuwa na kigugumizi kuamua kukamilisha ndoto ya Mwalimu ya kujenga bwawa la kuzalisha umeme la Stiegler’s Gorge na akalibadilisha jina na kuamua liitwe Bwawa la Mwalimu Nyerere!
Rais Magufuli kwa kuwa ni msomi wa uhakika na si wa kubabaisha, ‘akajiongeza’ akaelewa kwamba uwepo wa njia bora za usafiri ni muhimu kwenye kukuza uchumi. Mbali na kukarabati Reli ya Kati na kufufua reli zilizokuwa hazifanyi kazi, akaamua kuiweka Tanzania kwenye viwango vya kimataifa kwa kujenga reli mpya ya kati ya Standard Gauge na kuendeleza upanuzi na ujenzi wa barabara bora, na kadhalika.
Alipoingia madarakani, Gazeti pendwa la JAMHURI lilikuja na kichwa cha habari “JPM akuta zigo la Madeni ATCL.” Maelezo ya taarifa hiyo ni kwamba, mwaka 2014 Shirika la Ndege la Tanzania – ATCL – lilikuwa na deni la Sh bilioni 95.7!
Kwa ‘hasira’, Rais Magufuli akaamua kununua ndege tano mpya na kuzilipia kwa pesa taslimu! ‘Wajuaji’ wakalalamika kwamba anakosea kununua kwa pesa taslimu. Ununuzi wa aina hiyo hufanywa kwa mkopo, ili ulipie riba! Cha kushangaza, wajuaji hao baada ya kulaumu sana, wakawa miongoni mwa abiria wa kwanza kuzipanda ndege hizo!
Watanzania wasioitakia mema nchi yao, Rais Magufuli alipoingia madarakani na kuonyesha uongozi mahiri, walisema ilikuwa ni nguvu ya soda tu! Lakini sasa inabidi waambiwe wameze maneno yao kwa sababu ni miaka minne rais ameendelea na msimamo wake uleule alioanza nao. Anachukua hatua zilezile alizoanza nazo za ‘kutumbua’ watu wanaofanya uzembe kazini, anawashughulikia wala rushwa na mafisadi kwa kasi ileile – wako wapi wale mafisadi wa bandarini waliokuwa wanafanya kufuru katika kushindana kutajirika kwa kuiibia nchi?
Rais anakusanya kodi kwa nguvu mpya; ameonyesha ari ya ajabu katika kuwatumikia wananchi wanyonge – tumeona na kusikia kila anapozunguka nchini jinsi anavyosikiliza shida za wanyonge wake na zingine kuzitatua papo kwa papo.
Mungu atupe nini? Watoto wetu na wajukuu zetu wanapata elimu bure tangu shule za msingi hadi sekondari na kila siku shule mpya zinajengwa, majengo ya shule za zamani yanakarabatiwa na vyumba vya madarasa kuongezwa.
Rais Magufuli anajali sana afya za wananchi. Serikali yake imekwisha kujenga vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya zinazokaribia 70; anasambaza dawa kote nchini – mwaka 2015/2016 bajeti ya dawa ilikuwa Sh bilioni 29, sasa imefikia Sh bilioni 262!
Hivi sasa hatuendi tena India kwa matibabu ya moyo, figo na kadhalika. Mambo yote yanafanyika Muhimbili, Mloganzila, JKCI, Bugando, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na kadhalika.
Wapo jamaa wanaotaka Rais Magufuli pamoja na kutoa elimu bure atoe na matibabu bure. Hawa wanaonyesha kwamba hawajui madhumuni ya matumizi ya bima za afya. Nchi zote zilizoendelea na zinazotaka kuendelea zinatumia bima za afya.
Pengine viongozi wa mashirika ya bima za afya ndio watakiwe ‘kujiongeza’ na kuangalia namna ya kuboresha huduma zao ili hatimaye wananchi waweze kupata matibabu ya aina yoyote ile kwa kutumia bima, hususan kwenye matibabu yenye gharama kubwa.
Rais Magufuli ndani ya miaka minne anatekeleza ari endelevu ya kukuza uchumi wa nchi yetu. Kote nchini, tunashuhudia ujenzi wa viwanda, barabara na miundombinu mingine mbalimbali. Amekwisha kudhibiti uporaji wa madini yetu uliokuwa ukifanywa na walafi wa nje ya nchi wakishirikiana na wa ndani wasio na uzalendo.
Tunaweza kusema Rais Mafuguli tangu aingie madarakani yeye anakimbia mchakamchaka tu, hajatembea wala kupumzika, anataka kuhakikisha anafikia ndoto yake ya kuijenga Tanzania Mpya, Tanzania ya Viwanda, Tanzania ya Uchumi wa Kati. Anajenga Tanzania ambayo Makao Makuu yake ni Dodoma na si Dar es Salaam tena! Watanzania tunatakiwa tumuunge mkono kwa sababu anayofanya ni kwa manufaa yetu sote.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi leo anakumbukwa sana na Watanzania, Waafrika na dunia kwa sababu moja kubwa ya kuwatumika wananchi wa taifa lake na binadamu wengine kwa moyo na kwa nguvu zake zote.
Kwa msingi huo tupo tunaofananisha utendaji wa Rais Magufuli na ule wa Mwalimu kwa sababu moja kubwa ya kujali na kuwatumikia wananchi anaowaongoza.
Kwa muktadha huo, na kwa yale yote makubwa ya kimkakati na madogo ya kizalendo ya kuwajali wanyonge – wakulima, wafugaji, wavuvi, wamachinga, wachimbaji wadogo wadogo, wajasiriamali, kina mama na bibi lishe na kadhalika, yote hayo Rais Magufuli aliyoyatenda ndani ya miaka minne ya uongozi wake kwa manufaa ya taifa letu, anastahili kupongezwa na kila Mtanzania mwenye nia njema.
Wapo watu ambao eti hawataki Rais Magufuli afananishwe na Mwalimu Nyerere! Mwalimu Nyerere alikuwa ni wa Watanzania wote. Wala hatujawahi kusikia kwamba Rais Magufuli anajitangaza, anajitapa ama kujifananisha na Mwalimu, ila kila akiongea anamtaja Baba wa Taifa kwa mapenzi makubwa.
Hata hivyo, sidhani kwamba kuna mwenye ‘hatimiliki’ na hakuna anayeweza kujitapa kwamba yeye anayafahamu ya Mwalimu kuliko Watanzania wengine wote, kwa sababu wapo Watanzania ambao hawakuwahi kukutana na Mwalimu, wamekuwa wakimsoma tu kwenye magazeti, machapisho yake na kusikiliza hotuba zake lakini wameweza kumuelewa Mwalimu na kuwa waadilifu na wenye kuipenda nchi yao utadhani walikuwa wakiongea naye kila uchao!
Nilipenda sana unyenyekevu aliouonyesha Rais Magufuli kwenye hotuba yake aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Mwalimu Nyerere, Septemba 9, 2019. Alisema: “…..Tunaye hapa Mama yetu, Maria Nyerere pamoja na familia yake; yupo mzee Mwinyi ambaye aliachiwa madaraka na Baba wa Taifa; wapo pia makamu wa rais na mawaziri wakuu wastaafu ambao walifanya kazi kwa karibu na Baba wa Taifa; lakini pia wapo waliokuwa wasaidizi wake, wakati akiwa rais na hata alipong’atuka madarakani, akiwemo mzee Mkapa, mzee Msekwa, mzee Butiku, na kadhalika. Sasa nimejiuliza, hivi kweli mimi John Pombe Joseph Magufuli nitawaambia nini watu hawa ambacho hawakifahamu kumhusu Baba yetu wa Taifa?…”
Wapo waliokuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Kwanza, wapo waliokuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere, wote hawa walipata fursa nzuri ya kumfahamu Mwalimu. Naamini pia kila mmoja wao alijaribu kwa kadiri ya uwezo aliokuwanao kuchukua aliyoweza kujifunza kwa Mwalimu na kuyafanyia kazi.
Nia yangu si kudharau watu wengine, bali ninaona Rais wetu Dk. Magufuli anastahili kuingizwa kwenye kundi hili la ‘wateule’ hawa kwa sababu yeye ametudhihirishia kwa vitendo kwamba alimuelewa vizuri sana Mwalimu. Tangu aingie madarakani amekuwa akichukua yale aliyoyasimamia Mwalimu moja baada ya jingine na kuyafanyia kazi ama kuyaendeleza.
Kwa maoni yangu, Rais Magufuli amekamilisha takwa la Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, kwamba tupate mtu mwenye mwelekeo wa ki-Nyerere Nyerere hivi!
Kwa msingi huo basi na kwa mazuri yote aliyoyafanya Rais Magufuli ndani ya miaka minne tu ya uongozi wake uliotukuka, yeye ndiye anastahili sana KUTEMBEA KIFUA MBELE!
Kuna sababu tatu ninazoziona za kumfanya yeye atembee kifua mbele. Moja, ni kwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo. Pili, ni kututoa Watanzania kwenye shimo ambalo tulikuwa tunaelekea kutumbukia kutokana na makosa yetu wenyewe, makosa yaliyofanya tukalilia mabadiliko ambayo tumefanikiwa kuyapata kwenye uongozi wa Rais Magufuli. Tatu, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya ndani ya miaka minne ya uongozi wake uliotukuka.
Anna Julia Mwansasu ni Katibu Muhtasi mstaafu, anapatikana kwa simu namba 0655774967.