Leo ni wiki ya kwanza ya mwaka 2017. Wiki iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ametoa mwenendo wa hali ya uchumi nchini, akisema Taifa halina mdororo wa uchumi. Ametoa takwimu kuwa kwa sasa uchumi unakua kwa asilimia 7.2. Kiwango hiki ni cha kuridhisha. Ametaja sekta zinazokua kwa kasi kuwa ni Ujenzi na Mawasiliano.

Hata hivyo, katika taarifa hiyo, Dk. Mpango amesema kati ya Agosti na Oktoba, mwaka huu kwa Jiji la Dar es Salaam katika Wilaya ya Ilala, wafanyabiashara 1,076 wamefunga biashara zao. Wilaya ya Kinondoni, wafanyabiashara 443, Temeke 222 na Arusha 131 wamefunga biashara zao. Hali ni hivyo karibu mikoa yote. Katika kusisitiza akasema:

“Hata hivyo, sababu hasa zilizosababisha biashara hizo kufungwa hazijafahamika kutokana na ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wenye biashara zilizofungwa. Sababu za mtu kufunga biashara yake zinaweza kuwa nyingi, ikiwamo kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au, kulipwa madeni, kubadilisha aina ya biashara na kushindwa kusimamia biashara.”

Sekta ya Utalii iliyokuwa inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni, amesema haijaathiriwa na ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za utalii. Mwaka jana wakati sisi tunapitisha bajeti ya kuweka VAT katika huduma za utalii, nchini Kenya wao wameondoa VAT katika huduma hizo na huduma za Bandari.

Sisi tunaamini msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Tunao wajibu wa kumweleza ukweli Rais wetu kwani amekuwa mkweli muda wote. Tunamwomba maneno ya Dk. Mpango juu ya hisia zake za kwa nini wafanyabiashara wanafunga biashara asiyaamini mno. 

Nchini Iraq, aliwahi kuwapo Waziri wa Habari aliyefahamika kwa jina la Muhammad Saeed al-Sahhaf. Al-Sahhaf aliihadaa dunia kuwa Iraq ilikuwa na uwezo wa kuteketeza majeshi ya Marekani mara tu yafikapo Baghdad. Kilichotokea ni aibu. Majeshi ya Marekani yalipoingia Baghdad hayakukuta simba wala ndezi. Maelezo ya Dk. Mpango hatudhani kama yana uhalisia. Hatuna historia iwapo Dk. Mpango aliwahi kufanya biashara na iwapo anaeleza hali halisi.

Hofu yetu ni kuwa ikiwa wafanyabiashara wataendelea kufunga biashara, muda si mrefu Serikali itakosa mahala pa kukusanya kodi.  Ni kutokana na hofu hiyo tunaomba Rais Magufuli asimwamini mno Dk. Mpango. Waziri huyu akiwa kama Al-Sahhaf nchi itajikuta kwenye shimo kubwa. Mwamini waziri wako, ila uwe na mipaka. 

Uraiani hali mbaya. Uchumi hauna afya aisemayo. Shauriana na wataalamu wabobezi wa ndani na nje, uzuie mserereko wa kutisha unaoendelea. Heri ya Mwaka Mpya 2017.