Wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemchagua Rais John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti wake. Uchaguzi huu umehitimisha minong’ono iliyokuwapo kitambo kuwa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete alikuwa na nia ya kung’angania madarakani. Rais Magufuli amepigiwa debe kuomba kura kati yao akiwamo Katibu Mkuu (mstaafu) wa CCM, Luteni Yusufu Makamba.
Makamba alitumia maandiko ya vitabu vitakatifu, ikiwamo Biblia na Korani, ila akahitimisha kwa kuwambia wana CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa Kikwete akiwa Rais na Mwenyekiti wa CCM alikuwa akiwabatiza kwa maji, sasa Rais Magufuli atawabatiza kwa moto! Haya ni maandiko ya vitabu vitakatifu, ila yamesheheni maana kubwa.
Sitanii, kati ya vitu alivyovisema Rais (mstaafu) Kikwete kwa uchungu mkubwa ni uhai wa chama. Ni bahati mabaya kuwa nikiziangalia hotuba ya Rais Magufuli na Mwenyekiti wa CCM na ile ya Rais (mstaafu) Kikwete, naona kama kisiasa zina mtazamo tofauti kidogo. Wakati Rais Magufuli akisema huu ni wakati wa kufanya kazi si siasa, mtangulizi wake anasema CCM ikitaka uhai, ni lazima ifanye mikutano ya hadhara.
Kikwete anatumia maneno kuwa watani zao wanakwenda kwa wapigakura, akiamaanisha wapinzani, na akamwambia Rais Magufuli kuwa bila kuwafikia wapigakura, itakipa wakati mgumu chama chake. Rais Magufuli nikichekecha na kuangalia falsafa yake, anaona wananchi atawafikia kwa kuwapelekea maendeleo ya kweli.
Falsafa hizi mbili zinaweza kuonekana zinakinzana, ila tuzipe muda kuona zinafanyaje kazi. Hata hivyo, wakati zinapewa muda inabidi kushauriana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akawaeleza uzoefu wa faida ya kufanya mikutano na kazi za wananchi. Kinana bila kufika kwa wananchi akafyatua tofali, akajenga, akalima, akaezeka na wananchi, CCM ingeisoma namba zamu hii.
Sitanii, nashawishika kuwa Rais Magufuli mikutano ya kuhamasisha maendeleo ni vyema akairuhusu kwa faida ya taifa hili. Enzi za Mwalimu Julius Nyerere, tulikuwa na mikutano ya matawi, vijiji na kata. Tuliitumia mikutano hii kuwapa mrejesho viongozi wetu na wakati mwingine kukosoa utendaji walipoteleza.
Bila kuhamasisha mikutano ya maendeleo, wananchi wakashiriki mchakato wa kujiletea maendeleo, maendeleo yakifikishwa na Serikali bila kuwashirikisha watayaona ni ya wafadhili hayawahusu. Bila mikutano tunaweza kutengeneza mkatiko wa mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, na vyama vya siasa na wananchi.
Wananchi wanahitaji kupewa taarifa mara kwa mara juu ya kinachoendelea ndani ya chama tawala na Serikali, lakini pia vyama vya upinzani vinapaswa kupata fursa ya kufanya mikutano ya hadhara kukosoa utendaji wa Serikali (si kutukana viongozi) na hiyo ndiyo afya ya kisiasa. Serikali ikifunga mlango na kuzuia mikutano hii, siku ikija kufungua mlango, inaweza kukuta giza limeishaingia nje!
Sitanii, nikiri kuwa nimevutiwa na mambo mawili; uhai wa CCM, kwa maana ya kuwafikia wanachama na kuwahamasisha kulipa ada na kuvitumia vitegauchumi vyake kupata pato halali. Hili ni muhimu si kwa CCM tu, bali kwa vyama vyote nchini. Vyama vikitegemea wafadhili, vifahamu kuwa misaada hiyo itakuja na masharti, na mengine yanaweza kuwa magumu kwetu, kama waliotaka turuhusu ndoa za jinsia moja!
Jambo la pili, ni nia ya kweli ya Serikali kuhamia Dodoma. Nilikuwa ukumbini. Nilimwangalia usoni, jinsi alivyosita na hatimaye akajikusanya na kutoa ahadi hiyo. Hakika chini ya Rais Magufuli na jinsi nilivyomwona sura yake, zamu hii Serikali inahamia Dodoma. Serikali ikiishahamia Dodoma, naamini miundombinu ya nchi hii itaimarika.
Sitanii, nakubaliana na Rais Magufuli, kuwa katika siasa za ushindani tusivumilie usaliti. Wakati nikikubaliana naye, niombe kutoa ushauri tu, ambao si lazima auchukue, kwamba kama usaliti ulivyo mbaya, siasa za vitisho pia zinapaswa kuepukwa. Siseme ndivyo afanyavyo, ila siasa za vitisho, ndizo huzaa usaliti. Rais Magufuli waruhusu watu wako ndani ya CCM waseme wanachokiamini kwa masilahi ya usatawi wa chama na nchi.
Sisemi unaelekea huko, ila ikiwa utaingia kwennye vikao ukaona kila mjumbe anasifia mawazo yote uliyowasilisha bila kukosoa hata chembe, pata hofu. Ukitaka kuongoza chama kwa kusifiwa, utajikuta unasafiri kwenye mtumbwi wa mabarafu, na wala usijiruhusu kufika huko. Nashukuru, umesema bayana kuwa uamuzi ndani ya chama ni kwa vikao, naomba hili ulishikilie kweli na visiwe vikao vya kubariki uamuzi wako!
Vinginevyo ukiacha hayo machache niliyoshauri, na wala si lazima uyachukue, ila ikikupendeza uyapokee, napenda kuungana na Watanzania wenzangu kuchukua fursa hii kukupongeza, hasa kwa nia ya kuhamishia Serikali Dodoma na kurejesha mali za CCM mikononi mwa chama. Hongera Rais Magufuli, Mungu akubariki sana.