Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli shikamoo. Leo nakuandikia waraka huu mfupi kupitia safu yangu ya Sitanii. Kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu kukupongeza na kukushukuru kwa hatua ya kudhibiti wizi wa madini yetu na pia kumwondoa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo.
Unaweza au baadhi ya wasomaji wanaweza kushangaa kwa nini nifurahie kuondolewa kwa Muhongo.


Sitanii, kwanza niseme tarehe 24 inaweza kuwa tarehe mbaya kwa Profesa Muhongo. Ni mara ya pili sasa anajiuzulu au kufukuzwa uwaziri. Tarehe 24, 2015, Prof. Muhongo alilazimika kujiuzulu uwaziri baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotaja sehemu ya fedha za Escrow zipatazo bilioni 330. Mei 24, 2017, Prof. Muhongo amefukuzwa kazi kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini.


Nakiri kwa muda mrefu nilikuwa shabiki mkubwa wa Prof. Muhongo. Nilivutwa na wimbi la wizara hiyo kuanza kuchapa kazi, hasa pale aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alipoanza kudhibiti uingizwaji wa nguzo hewa. Maswi alidhibiti zilizokuwa zinaitwa nguzo kutoka Afrika Kusini, kumbe zinatoka Mufindi.


Kuanzia wakati huo niliburudika kuona watu hawa wanafanya uzalendo wa hali ya juu. Nilifurahi zaidi kwa jinsi walivyoshiriki kuondoa urasimu wa Tanesco katika kuwapatia wateja umeme. Kutoka katika kuambiwa hakuna kadi, mita, vikombe na nyaya, hadi kufikia mteja akiomba umeme kupigiwa simu akaulizwa atakuwa nyumbani saa ngapi afungiwe umeme, ni hatua kubwa.
Sitanii, baada ya Maswi kuondoka, kidogo kidogo nikaanza kumfahamu Prof. Muhongo. Yakaanza kutokea matukio yenye kutia shaka juu ya uadilifu wa huyu profesa. Tabu ya wateja kuambiwa hakuna mita ikarejea. Watu wakaanza kumkubuka Maswi. Si hilo tu, Prof. Muhongo alinipa mshangao wa mwaka alipoingia katika ulingo wa kutetea wachakachua mafuta.


Prof. Muhongo aliendelea kunishangaza aliposhirikiana na baadhi ya wabunge maslahi kutaka kuishinikiza Serikali iivunje Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) au ihamishwe kutoka Wizara ya Maji kwenda Wizara ya Nishati na Madini. Kwa muda nimepingana na mpango wa Muhongo dhidi ya Ewura na kusitisha matumizi ya vinasaba kwenye mafuta ya ndani kuepusha uchakachuaji.


Wabunge hawa walifika mahala wakasema vinasaba vinapatikana kwa magendo (black market). Hii Prof. Muhongo alielekea kuishikia bango. Nikasema angefahamu ukubwa wa tatizo lililokuwapo kabla ya kuanza kuweka vinasaba, asingethubutu hata kuwaza kuivunja Ewura. Mafuta ya ‘transit’ ya kwenda nje yalikuwa yanaishia kwenye soko la ndani, leo wamedhibitiwa, ilikuwa wanaelekea kupata msaada wa Prof. Muhongo kurejesha uchakachuaji.
Sitanii, wakati nikiendelea kushangaa hili mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, Kampuni ya Sahara Energy ya Nigeria ilileta mafuta machafu mara tatu nchini mwaka 2016, lakini kwa masikitiko makubwa Prof. Muhongo akawa anaitetea kampuni hii ipewe zabuni ya kuingiza mafuta nchini akishirikiana na aliyekuwa Kaimu Mkurugeni wa Wakala wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja (BPA), Michael Mjinja.


Hili nililisimamia, tukapingana hadi tukafikishana TAKUKURU na Prof. Muhongo kikaeleweka. Sahara wakanyimwa kazi, Mjinja akatumbuliwa. Katika mchakato huu ndipo nilipoanza kukubaliana na maneno ya Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla, aliyepata kusema: “Sijawahi kuona msomi mwenye uwezo wa kudanganya kama Prof. Muhongo.”
Sitanii, ya Prof. Muhongo yako mengi. Ukiacha hilo la Sahara Energy na Michael Mjinja na vinasaba vya kuzuia mafuta kuchakachuliwa, ukipata fursa muulize aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk. James Mataragio, atakwambia vimbwanga vya Prof. Muhongo. Hata ule mgogoro wa Dangote kukosa gesi mkono wake haukuwa mbali.


Wakati Mhe. Rais ukiamini kuwa Watanzania wanaweza, na ukihoji wenye viwanda wana DNA zipi, Prof. Muhongo anabeza Watanzania kuwa kazi pekee wanayoiweza ni ya kuuza maji, soda na juisi. Nimesikia leo au kesho Prof. Muhongo anahojiwa kutokana na kushindwa kusimamia sera. Nasema wamhoji hadi mikataba kadhaa anayodaiwa kushinikiza iingiwe kwenye gesi kujua ilikuwa ni kwa maslahi ya nani.


Mhe. Rais, kama ulivyosema vita ya uchumi ni vita ngumu, nakubaliana na wewe. Naomba kukuhakishia kuwa sisi watumishi wa Gazeti la JAMHURI, tumeamua kuingia kwa miguu yote miwili katika vita hii ya madini.
Tutafanya uchunguzi wa kina na kuifikishia jamii ukweli. La msingi, tunaomba ushirikiano. Huu ni wakati wa kutetea nchi yetu. Kwa pamoja tusema mwisho wa kuporwa madini ni sasa. Hongera Mhe. Rais Magufuli.