Katika siku za karibuni kumekuwa na mtanziko mkubwa wa kisiasa nchini, huku Rais John Magufuli akizidi kusisitiza kwamba muda wa kufanya siasa umekwisha kilikochoko ni kusaidia wananchi kufikia maisha bora wanayostahili.

Huku Rais Magufuli akisema hayo, chama kikuu cha upinzani nchini Chadema, kimetangaza Septemba Mosi, kuwa siku maalum ya kuanza kwa operesheni ya kupinga ‘udikteta’ nchini, mpango unaolenga kupinga amri ya Rais.

Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba wanasiasa wafanye siasa majimboni mwao, na si kutwa kucha kuzurura na kusambaza siasa ambazo yeye hakubaliani nazo. Uamuzi huo wa Rais unaoekana kuwa mwiba mchungu kwa ustawi demokrasia ya vyama vingi nchini.

JAMHURI linashauri kuwepo namna bora zaidi ya kuviruhusu vyama vya siasa kuendesha siasa, maana kimsingi vimesajiliwa kwa kukidhi vigezo na mahitaji ya kisheria kufanya shughuli za kisiasa nchi nzima bara hata visiwani na si majiboni pekee.

Mheshimiwa Rais, tunatambua busara zako na uvumilivu wa kisiasa tangu ukiwa mbunge wa Jimbo la Chato kwa zaidi ya miongo miwili, umekuwa ukishandana kwa hoja na kuwafanya wapinzani wako kushindwa kupambana nawe kwa hoja.

Sisi tunaamini kwamba ukiamua kuruhusu siasa za masuala inawezekana kabisa utachangia katika kukuza demokrasia ya vyama vingi nchini, lakini kama utendelea kushirikilia msimamo wako, vyama vya siasa kwa sababu wanaheshimu mamlaka watatekeleza, lakini ukweli ni kwamba, utakosa watu makini wa kukukosoa na kuliendesha taifa letu vizuri.

Umeruhusu wabunge kufanya siasa majimboni mwao tu, hapa kidogo tunapata ukakasi. Kuna vyama ambavyo havina wabunge kabisa kama TLP, CHAUMA, UDP, je, ndio umevichimbia kaburi? Pengine kwa kutokujua mamlaka zinazohusika na kuvilea vyama vya siasa unaviweka katika wakati mgumu kutokana na ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa wewe ndiye mamlaka ya uteuzi.

Katika kutafuta namna ya kusikika, baadhi ya wanasiasa sasa wameamua kwa makusudi kuhakikisha wanasikika kwa gharama zozote. Mfano wa wanasiasa hao ni Mbunge wa Singida Mashariki, kupitia Chadema, Tundu Lissu ambaye amegonga vichwa vya habari wiki iliyopita.

Sisi tunaamini kwamba, matendo aliyofanyiwa Mheshimiwa Tundu Lissu ya kuletwa Dar es Saaam akiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi kama mlidhani mnamtia hofu, uhalisia yanamjenga zaidi kisiasa pengine kuliko hata wapinzani wangeruhusiwa kufanya mikutano. Jambo jingine ni namna ambavyo jeshi la Polisi limekuwa likitafsiri kauli zako na kuzua tafrani pasipo sababu za msingi.

Hapa tunajikita katika suala la Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, ambao kwa nyakati tofauti wamehojiwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuhusiana na kauli zao dhidi yako Rais. Lakini wakati hayo yanaendelea Rais Magufuli, unapata fursa ya kukutana na wananchi na kusikiliza kero zao.

Sisi JAMHURI, tunakusihi ujaribu kulegeza misimamo kwa maana wewe ndiye mlezi namba moja wa demokrasia hapa nchini, ukiviruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila shaka utatawala vizuri. Kama zuio lako litaendelea basi tutarajie kudorora kwa demokrasia ya vyama vingi nchini na utapoteza muda kupambana na wanasiasa badala ya kujenga viwanda.