Hotuba ya Rais John Magufuli kwenye hafla aliyoindaa kwa ajili ya mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa kukaribisha mwaka mpya 2019
Ikulu, Dar es salaam; Machi 8, 2019
Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Ahamada Fakih, Balozi wa Muungano wa Visiwa Vya Comoro na Kiongozi wa Mabalozi nchini;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda nitumie fursa hii kuwakaribisha hapa Ikulu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria hafla hii muhimu na maarufu kwenye nyanja za kidiplomasia, ambayo inajulikana kama Sherry Party.
Kama mjuavyo, sherehe hii kwa kawaida hutumika kukaribisha Mwaka Mpya. Hivyo basi, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutumia fursa hii, kuwatakieni Heri ya Mwaka Mpya wa 2019, ninyi Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, familia pamoja na watumishi wenu. Aidha, kupitia kwenu, naomba salamu zangu za Heri ya Mwaka Mpya ziwafikie Wakuu wa Nchi, Serikali na Mashirika yote mnayoyawakilisha hapa nchini.
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Mwaka mpya unapoanza ni wakati wa kufanya tathmini kuhusu mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza kwenye mwaka uliopita, na pia kupanga mikakati ya mwaka unaoanza. Kwa kuzingatia hilo, na kwa kuwa ninyi ni Mabalozi wa nchi rafiki wa Tanzania na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayoshirikiana vizuri na Tanzania, katika hotuba yangu ya leo nitajielekeza zaidi kwenye kufanya tathmini ya mwaka uliopita na halikadhalika kuwaeleza kwa kifupi mipango yetu kwa mwaka huu mpya.
Lakini, kabla sijaendelea, naomba kwanza, nitumie fursa hii kumtambulisha kwenu rasmi Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri Mpya wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ambaye nimemteua kuchukua nafasi ya Dkt. Augustine Mahiga ambaye nimemwamishia Wizara ya Katiba na Sheria. Ni matumaini yangu kuwa mtampa Waziri Mpya ushirikiano, kama mlivyofanya kwa Mhe. Waziri Dkt. Mahiga.
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Nikitathmini mwaka 2018, ni dhahiri kuwa, kwetu sisi Tanzania, ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa. Nasema hivyo kwa sababu, kama mjuavyo, jukumu la kwanza na muhimu kabisa la Serikali yoyote duniani, ni kulinda na kudumisha amani na usalama katika nchi. Na hiyo inatokana na ukweli kuwa, amani na usalama ndio msingi wa kila kitu. Penye amani ndipo maendeleo hupatikana, biashara hufanyika, wenye mitaji huweza kuwekeza, miradi ya maendeleo kutekelezwa kikamilifu, huduma za jamii kutolewa; na haki pamoja na uhuru wa wananchi kulindwa. Amani isipokuwepo, mambo hayo yote hayawezi kupatikana. Ni kwa sababu hiyo, nafurahi, mwaka jana, 2018, nchi yetu iliendelea kudumisha amani. Tanzania imebaki kuwa kisiwa cha amani. Mipaka yetu ipo salama. Usalama wa raia na mali zao umeendelea kuimarika. Napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama, viongozi wetu wa dini pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa kuendelea kudumisha amani nchini. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa kuendelea kushirikiana nasi vizuri katika kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu. Ahsanteni sana.
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Kama nilivyosema, penye amani ndipo penye maendeleo. Hivyo basi, kutokana na kufanikiwa kudumisha amani, nchi yetu mwaka jana iliweza kuendelea na jitihada zake za kukuza uchumi kwa lengo la kujiletea maendeleo. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2018, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tano bora zilizoongoza kwa kasi ya ukuaji uchumi Barani Afrika, zikitanguliwa na Ethiopia ambayo uchumi wake ulikua kwaasilimia 8.5, Cote d’Ivoire asilimia 7.4, Rwanda asilimia 7.2; Tanzania asilimia 7.0, na Senegal asilimia 7.0. Tulifanikiwa pia kudhibiti mfumko wa bei, ambapo kwa mwaka mzima, wastani wa mfumko wa bei ulikuwaasilimia 3.5. Kiwango hiki kilikuwa cha chini zaidi kuwahi kutokea nchini katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita. Aidha, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka 2018 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Biashara na Maendeleo Tanzania iliibuka kinara katika kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, ambapo tulivutia mitaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.18.
Sambamba na hayo, mwaka jana, tuliendelea kutekeleza miradi yetu mikubwa ya miundombinu yenye lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza uwezo wa nchi yetu kutoa huduma za jamii. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, ambayo kwa upande wa Dar es Salaam – Morogoro hadi mwezi Januari 2019, ilikuwa imefikia asilimia 42.8, na kutoka Morogoro hadi Dodoma imefikia asilimia 6.07. Tumeanza pia maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme, Megawati 2100, katika Bonde la Mto Rufiji na kuendelea na miradi ya kusafirisha na kusambaza umeme. Miradi mingine ni upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga; ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria; ujenzi wa barabara; viwanja vya ndege, jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rada nne.
Halikadhalika, mwaka jana, nchi yetu iliendelea na jitihada za kupanua wigo na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii, hususan afya, elimu na maji; ambazo ni haki muhimu zilizoanishwa katika Katiba ya nchi yetu. Nikianza na afya, tulifanikiwa kukamilisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya vipatavyo 305 na pia kuanza ujenzi wa Hospitali mpya za Wilaya 67. Lengo letu kubwa hapa ni kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto, ambalo pia ni moja ya malengo ya Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (AU Agenda 2063) na ile ya Umoja ya Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 (Sustainable Development Goals). Zaidi ya hapo, napenda niwaarifu kuwa nchi yetu imeendelea kuimarisha huduma za tiba za kibingwa kwa magonjwa ya moyo, figo, kansa, masikio, mifupa, ubongo, n.k. Mathalan, mwaka jana, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilifanya operesheni za moyo 1,361 (305 za kupasua na 1,056 za kutumia tundu dogo). Hiki kilikuwa kiwango kikubwa zaidi kwa nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa upande wa elimu, tumeendelea kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, tumeimarisha vyuo vyetu vya ufundi pamoja na kuongeza ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Kuhusu maji, miradi mingi inaendelea kutekelezwa, ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji maji nchini imefikia asilimia 65 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 80 kwa mijini.
Masuala mengine ambayo nchi yetu inajivunia kwa mwaka jana ni pamoja na kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na rushwa, kusimamia masuala ya utawala bora na haki za binadamu pamoja na demokrasia. Na kuhusu demokrasia, mwaka jana nilipata fursa ya kukutana na baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Siasa ili kubadilisha mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na pia kujenga umoja katika nchi. Nitumie fursa hii pia kuwaarifu kuwa baadaye mwaka huu, nchi yetu itafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Huu ni uthibitisho demokrasia inazidi kukomaa nchini.
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Katika nyanja za kimataifa, kama mnavyofahamu, nchi yetu tangu imepata uhuru mwaka 1961 imekuwa mstari wa mbele kwenye masuala ya kimataifa. Hivyo basi, mwaka jana pia hapakuwa na tofauti. Tulishiriki kikamilifu kwenye masuala ya kimataifa, ikiwemo kuhudhuria mikutano yote muhimu kwenye EAC, SADC, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Na katika hilo, napenda niwaarifu kuwa mwezi Agosti mwaka jana Tanzania ilichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC; na baadaye mwaka huu tutakuwa wenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC, ambapo tunataraji kukabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya hiyo. Nitumie fursa hii kuarifu kuwa, mandalizi ya Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za SADC yanaendelea vizuri.
Nchi yetu pia mwaka jana iliendelea kutekeleza majukumu yake mengine kimataifa, ikiwemo kulinda amani. Hivi sasa tuna takriban askari 1,900 ambao wanalinda amani kwenye nchi za DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Nchi yetu pia imeendelea kupokea na kuwahudumia wakimbizi kutoka nchi mbalimbali zenye migogoro, ambapo hadi mwezi Februari 2019 tulikuwa na wakimbizi 324,420. Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi pamoja na Shirika la Wakimbizi Duniani, mwaka jana, tulifanikiwa kuendesha zoezi la kuwarejesha makwao kwa hiari takriban wakimbizi 57,889 wa Burundi.
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Penye mafanikio hapakosi changamoto. Hivyo basi, licha ya mafanikio tuliyoyapata mwaka jana, zipo changamoto tulizokumbana nazo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta; kupungua kwa biashara na uwekezaji; kuimarika kwa Dola ya Marekani dhidi ya sarafu nyingine na pia kushuka kwa bei ya mazao kwenye soko la dunia. Changamoto hizi, kimsingi, zimeikumba karibu nchi zote duniani; na hizi pia ndiyo baadhi ya sababu zilizofanya thamani ya shilingi yetu kutetereka kidogo lakini pia Serikali kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la korosho.
Changamoto nyingine ambazo tulikumbana nazo mwaka jana ni pamoja na janga kubwa la kuzama kwa Kivuko cha MV. Nyerere kwenye Ziwa Victoria, ambapo zaidi ya Watanzania 200 walipoteza maisha. Nawashukuru kwa salamu nyingi za rambirambi mlizotutumia. Lakini, mwaka jana pia tulipoteza askari wetu saba waliokuwa kwenye jukumu la kulinda amani nchini DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina.
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Katika mwaka huu mpya tumejipanga kuendelea kutekeleza malengo yetu mbalimbali, kubwa likiwa kukuza uchumi wa nchi yetu; tukiongozwa na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2016/17 – 2020/2021. Kama mnavyofahamu, dhima kuu ya Mpango huu ni kuifanya nchi yetu kuwa ya Uchumi wa Kati wenye kuongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira yetu ya Maendeleo inaelekeza. Hivyo basi, mkazo wetu mkubwa utakuwa kuendelea kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda nchini; hususan vyenye kutumia nguvu kazi kubwa na malighafi zinazozalishwa hapa nchini.
Mbali na viwanda, tutaweka mkazo pia kwenye sekta ya kilimo (kwa maana ya kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi). Kama mnavyofahamu, kilimo ni sekta muhimu kwa nchi yetu. Takriban asilimia 70 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo na inachangia takriban asilimia 60 ya malighafi za viwandani. Aidha, nchi yetu ina zaidi ya hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji; tunashika nafasi ya pili kwa idadi ya mifugo; na pia tuna maeneo mengi yenye kufaa kwa uvuvi (Bahari, Maziwa makubwa matatu, mito na mabwawa makubwa). Hata hivyo, mchango wa sekta hii bado ni mdogo, ambapo inachangia takriban asilimia 30 tu kwenye Pato la Taifa. Hivyo, tumedhamiria kuifanyia mageuzi makubwa sekta hii. Mwaka jana tulianza kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Programme Phase Two– ASDP II), ambao unalenga kuongeza tija kwenye kilimo, hususan kwa kuhimiza kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya pembejeo na zana za kisasa za kilimo, kuzingatia matokeo ya tafiti mbalimbali, kuanzisha masoko ya mazao na pia kuongeza mikopo.
Mbali na kilimo, sekta nyingine ambayo tutaipa kipaumbe mwaka huu ni utalii. Kama mnavyofahamu, nchi yetu imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii: uoto wa asili, wanyama, fukwe, mali kale, n.k. Hivyo basi, tumejipanga kutangaza vivutio vyetu, hususan vilivyopo kwenye Ukanda wa Kusini mwa nchi yetu. Na katika hili, napenda kuwataarifu kuwa Kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC) kimeanzisha chaneli maalum ya kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini. Aidha, napenda niwaarifu kuwa, baada ya kuwasili kwa ndege zetu kubwa tatu mwaka jana, moja aina ya Boeing 787, Dreamliner na nyingine mbili aina ya Airbus A200 -300, Shirika letu la Ndege limeanza safari za kwenda Zambia na Zimbabwe. Aidha, hivi karibuni tutaanza safari za masafa ya mbali kwenda China, India na Thailand.
Sambamba na hayo, tumepanga kuweka kipaumbele kwenye sekta ya madini. Kama mavyofahamu, Tanzania pia ina utajiri mkubwa wa madini. Tuna kila aina ya madini: dhahabu, almasi, tanzanite, shaba, chuma, makaa ya mawe, urania, magadi, chumvi, rubi, tin, tantalite, titanium, tungsten, n.k. Hata hivyo, kwa bahati sana, kwa muda mrefu, utajiri wetu huo haujaweza kutunufaisha. Hivyo basi, tumejipanga kufanya mageuzi kwenye sekta hii kwa kudhibiti wizi na biashara za magendo, kuanzisha masoko hapa nchini na kuhimiza ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani madini.
Napenda nitumie fursa hii kuwasihi Waheshimiwa Mabalozi kutusaidia kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo hapa nchini. Aidha, nawaomba muwahimize watu wenye mitaji kutoka kwenye nchi zenu kuja kuwekeza nchini kwenye sekta za viwanda, kilimo, utalii na madini. Tanzania ni mahali pazuri pa kuwekeza. Najua wapo wenye kudai kuwa sisi hatupendi wawekezaji. Hiyo sio kweli. Sisi tunawapenda wawekezaji. Na katika kuthibitisha hilo, hivi karibuni tumeamua kuanzisha Wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, hivi sasa tunakamilisha Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini. Binafsi, tangu tulipokutana hapa mara ya mwisho, nimekutana na wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na uwekezaji (taasisi za Serikali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wachimba madini, wakulima, n.k.) Hii yote ni kudhihirisha kuwa tunawapenda na kuwahitaji wawekezaji na wafanyabiashara. Na kwa kusema kweli, tunataka mwaka 2019 uwe wa Uwekezaji. Lakini, narudia wito kwa wawekezaji na kwa watu wenye nia ya kuwekeza nchini kuhakikisha wanazingatia sheria na kuendesha shughuli zao kwa misingi ya win-win.
Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Nimesema mambo mengi. Lakini kabla sijahitimisha nina suala moja la mwisho, nalo linahusu kuhamia Dodoma. Zoezi la Serikali kuhamia Dodoma linaendelea vizuri. Watumishi wengi tayari wameshahamia na Ofisi za Serikali zinaendelea kujengwa. Tunaendelea pia kuimarisha miundombinu mbalimbali, ikiwemo barabara, hospitali, huduma za maji, shule, n.k. Mwaka jana, Serikali yetu iligawa viwanja kwa balozi zote zilizopo hapa nchini; na nafahamu baadhi yenu tayari mmeshaanza taratibu za kuhamia Dodoma. Hongereni sana. Nazihimiza Balozi na Mashirika mengine nayo kuanza michakato ya kuhamia kwenye Makao Makuu yetu mapya, Jijini Dodoma, ili kurahisisha mawasiliano kati ya Serikali yetu na Ofisi zenu.
Nihitimishe kwa kuwashukuru tena Waheshimiwa Mabalozi kwa kuitikia wito wangu. Napenda pia niwashukuru ninyi binafsi pamoja na Nchi na Mashirika mnayowakilisha kwa kwa kuendelea kushirikiana na nchi yetu. Mafanikio mengi niliyoyataja, tumeyapata kutokana na ushirikiano wenu. Hivyo basi, nawasihi mwendelee kutuunga mkono. Tuendelee kufanya kazi kwa karibu. Kuweni huru kuwasiliana na Serikali wakati wowote, hususan kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ambayo kimsingi ndiyo kiungo kikuu cha mawasiliano kati yenu na Serikali. Na katika hilo, napenda niwaahidi kuwa Serikali yetu itaendeleza ushirikiana nanyi nyote pamoja na nchi na mashirika mnayowakilisha katika misingi ya maelewano na kuheshimiana.
Baada ya kusema hayo, narudia tena kuwatakia Heri ya Mwaka Mpya 2019. Uwe mwaka wa Amani na Mafanikio ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano.
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”