Sitanii, wiki hii kama kuna jambo limeniburudisha basi ni taarifa hii ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, aliyoitoa Dar es salaam tarehe 25 Aprili, 2016. Na kabla sijafafanua nilichokifurahia, naomba kwa ruhusa yako niinukuu neno kwa neno kama ifuatavyo:-
Chian imekubali kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati yenye urefu wa kilometa 2,561 kwa kiwango cha kisasa yaani ‘Standard gauge’ ambao zabuni za ujenzi zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Balozi wa China hapa nchini, Mheshimiwa Dkt. Lu Youqing, ametoa kauli hiyo tarehe 25 Aprili, 2016 Ikulu Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ambapo pia amemkabidhi barua yenye ujumbe kutoka kwa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemweleza Balozi Lu kuwa Tanzania imedhamiria kuanza ujenzi wa Reli ya Kati haraka iwezekanavyo na tayari imetenga fedha kiasi cha shilingi trilioni moja katika bajeti yake ijayo, kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
“Tuna imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati zikiwamo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndiyo maana hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze na watu waanze kunufaika,” amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Dkt. Lu Youqing, amempongeza Rais Magufuli na Serikali yake imejiandaa kwa fedha, vifaa na rasilimali watu kwa ajili ya kutekeleza mradi huu mkubwa na kwamba Serikali ya China, taasisi za fedha za China na kampuni mbalimbali zitatoa ushirikiano wote katika utekelezaji wa mradi huu.
“Kama ambavyo Prof. Mbarawa amefanya mazungumzo na Serikali ya China, taasisi za fedha za China na kampuni, naahidi kuwa tutaanza kazi kama ambavyo taratibu na viwango vya ujenzi vimewekwa, tutafanya kazi kwa kujali muda, ubora na gharama nafuu,” amesema Balozi Lu.
Mradi mzima wa ujenzi wa Reli ya Kati unatarajiwa kugharimu dola bilioni 6.8 za Marekani na umepangwa kutekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa kilometa 1,216 za kutoka Dar es salaam-Tabora-Isaka-Mwanza na itajengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China.
Tayari Rais Magufuli amemtuma Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, kwenda nchini China kukamilisha mazungumzo juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwamo wa ujenzi wa Reli ya Kati, ambapo Prof. Mbarawa anasema hatua inayofuata sasa ni kutangaza zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kwa uwazi, ili kampuni mbalimbali za ujenzi ziombe na hatimaye kupata washindi watakaoanza kazi mara moja.
Sitanii, kutokana na taarifa hii ya Msigwa, nimesoma na gazeti la The East African la Kenya lililochapishwa Jumamosi iliyopita, wakilia kuwa Rwanda nayo sasa inataka kuweka nguvu katika ujenzi wa mradi wa reli ya Kigali-Isaka, ambapo sasa itapitishia mizigo yake yote kwa asilimia 100 nchini Tanzania.
Uamuzi wa Rwanda umetokana na ziara aliyofanya Rais Magufuli nchini humo hivi karibuni, na nchi hiyo inasema ni gharama kubwa kujenga reli ya kutoka Kigali hadi Kampala (Uganda) kisha kuitafuta Nairobi na Mombasa. Uamuzi wa Rwanda umekuja siku chache baada ya Uganda kuamua kupitisha bomba lake la mafuta nchini Tanzania na kutumia Bandari ya Tanga.
Hata hivyo, kama kawaida yao, Wakenya sasa wameanza kulalamika kuwa mizigo inayopitia nchini mwao inaendelea kushuka kwa kasi. Wanaona Rwanda ikifanya uamuzi huo, itakuwa ni kukiuka makubaliano ya mwaka 2013 yaliyojulikana kama Coalition of the Willing (Umoja wa Wenye Utashi), yaliyoelekea kutishia mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kimsingi, makubaliano hayo yaliyozijumuisha nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Sudani ya Kusini yalipofikiwa mwaka 2013 niliandika makala nikatahadharisha kwa kusema kuwa ushirika huo ulikuwa sawa na nyumba iliyojengwa kwa matofali ya barafu.
Nilitaja sababu za msingi kuwa Kenya ni mgogoro katika ushirika huo. Kwamba Kenya ilikuwa imejiandaa kuwatumia Waganda na Wanyarwanda kwa maslahi binafsi na si kwa maslahi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Namshukuru Mungu. Nilisema umoja huu utatikisika si muda mrefu, na kabla wino wa kalamu yangu haujakauka tayari limetokea.
Sitanii, yapo mambo yaliyohitaji moyo kama wa mwendawazimu Uganda kuwaamini Wakenya kwa asilimia 100. Waganda wanayo kumbukumbu ya ugomvi usioisha juu ya kisiwa cha Mingingo. Waganda wanayo kumbukumbu ya Wakenya kung’oa reli katika eneo la Malaba kutokana na mgogoro huo wa Mingingo. Wala hapa sitataja al-Shabaab, halafu bila soni uwapelekee bomba la mafuta! Hivi unakuwa nazo kweli?
Kwa Rwanda, nafahamu ule ulikuwa ugomvi wa muda na usio na tija kwa mataifa yetu. Ushauri uliotolewa na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete kuwataka akina Rais Paul Kagame kuzungumza na waasi ulizua tafrani. Haukua ushauri mbaya, ila bahati mbaya tu haukueleweka. Tunamshukuru Mungu tumeuvuka huo mstari, na sasa tuna zama na kitabu kipya.
Shida ninayopata, Benki ya Dunia tayari imeanza. Inasema bora tukarabati reli ya kiwango cha mita iliyopo, badala ya kwenda kiwango cha ‘standard’, ambayo ni gharama kubwa na kwa sasa nchi za Afrika Mashariki hazina mzigo wa kutosha kuhitaji kiwango hiki cha reli.
Kinachotokea ni kwamba Benki ya Dunia katika taarifa yake inasema inatufaa hii reli ya mita, ambayo kasi yake ni kilomita 80 kwa saa, yenye uwezo wa kubeba mzigo hadi tani milioni 5.5 tu, ikilinganishwa na hiyo ‘standard’ yenye uwezo wa kubeba hadi tani milioni 60 kwa mwaka.
Tena hii inaweza kuongeza zaidi uwezo kwa kubadilishwa kwenda kasi ya hadi kilomita 500 kwa saa ikitumia umeme, badala ya kilomita 130 inayokwenda bila kutumia umeme. Ni katika hatua hii, nimesema ni bora niandike makala hii kukumbusha machache.
Rais Magufuli amekwishasema kuwa katika bajeti ya mwaka huu, tayari wametenga Sh trilioni moja, kwa ajili ya ujenzi wa reli hii. Balozi wa China, Lu, amesema wako tayari kutoa utaalamu, fedha na kila kinachohitajika kufanikisha ujenzi wa reli hii.
Ikumbukwe mwaka 1974, wakati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anataka kujenga reli kati ya Tanzania na Zambia (Tazara), Benki ya Dunia hiyo hiyo ilikuja na maelezo kuwa reli hiyo haitakuwa na faida kiuchumi. China ilipoingia ikafadhili reli na bomba la mafuta la Tazama, Wamarekani nao wakajitosa kujenga barabara ya Dar es Salaam-Mbeya-Zambia (TanZam Highway).
Mwaka 2004 wakati gesi ilipopatikana kule Mnazi Bay, Benki ya Dunia ikasema hakukuwa na sababu ya kujenga bombo lenye upana zaidi ya inchi 16, kwani gesi isingelijaza bomba hilo kwa muda wa miaka 20 ijayo, bahati mbaya likajaa baada ya miaka miwili tu, na sasa tumejenga jingine la inchi 36 kwa msaada wa China.
Sitanii, wenye malori wanao marafiki ndani ya Benki ya Dunia. Hata hizo gharama walizotaja watu wa Benki ya Dunia si halisi. Zimewekwa makusudi kupotosha umma na kuogofya wananchi. Mwezi uliopita nimepata fursa ya kusoma kitabu cha ‘Confessions of an Economic Hit Man’ kilichoandikwa na Mmarekani John Perkins. Naandaa utaratibu kitafsiriwe katika Kiswahili kwa nia ya kuwapa Watanzania fursa ya kukisoma na kuelewa tunavyopigwa.
Wakenya na Wamarekani au Wazungu wote kwa ujumla milele hawatutakii mema. Kusema kwamba Tanzania kwa sasa haina mzigo wa kutosha kujenga ‘standard gauge’ hadi mwaka 2030 ni kutupumbaza. Nasema hatua tuliyofikia, Rais Magufuli yakupasa usirudi nyuma. Hakuna nchi iliyopata kuendelea katika eneo la usafirishaji kwa kutegemea malori.
Mwisho, China wanaweza kuwa na malengo yao, lakini wamethibitika kuwa marafiki wa kweli. Bomba la pili la gesi tulilojenga, Benki ya Dunia ilitunyima mkopo, China wakatupatia.
Wachina wamekuwa marafiki wa kweli katika wakati halisi wa uhitaji, ni vyema sisi Watanzania tukalitambua hilo na kupokea mikopo yao yenye riba ya asilimia 1 au 2, badala ya riba za Benki ya Dunia zinazokimbilia asilimia 16.
Reli ni ufumbuzi katika kujenga uchumi imara, Rais Magufuli shikilia. Ukijenga reli hii historia itakukumbuka.