Wiki iliyopita nilikuwa katika kipindi cha ‘Malumbano ya Hoja’ kinachorushwa ‘live’ na ITV. Mjadala kadiri ulivyoendelea nilipata shida kidogo. Niliwaona baadhi ya wachangiaji wakizungumza lugha ya hatari, ambayo ninaisoma katika baadhi ya magazeti. Wanasema Rais John Magufuli anahujumiwa.
Sitanii, neno hili linaweza kuonekana dogo, lakini tunakoelekea lisipokemewa linaweza kudumaza maendeleo ya nchi. Kwa sasa nchi ina tatizo la sukari. Sukari imepungua katika soko baada ya agizo la Rais Magufuli lenye nia ya kujenga viwanda vya ndani.
Tukumbuke agizo hili halikujengewa mazingira. Lilitolewa ghafla. Tanzania inatumia wastani wa tani 420,000 za sukari kwa mwaka. Nchi yetu ina uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 320,000. Tani 100,000 zimekuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi.
Ni bahati mbaya zaidi kuwa hata hizo tani 320,000 zinazotajwa si sahihi. Wapo waagizaji wengi wasio waaminifu waliokuwa wanaagiza sukari ya viwandani, kwa maana ya kutengenezea soda, keki, ice cream na bidhaa nyingine zinazotumia sukari, lakini hawa wamekuwa wakiiuza katika soko la kawaida.
Hii ina maana, hata hizo zinazoitwa tani 100,000 kuwa ndiyo uliokuwa upungufu pekee, si takwimu za kweli. Ni jambo jema kuwa Rais Magufuli ameliona hili, ameagiza bila kusita na sasa tumeshuhudia uwezo halisi wa viwanda vyetu. Ndiyo maana Serikali imeamua kwa dhati kusimamia uagizaji wa sukari nje ya nchi.
Tumesikia viwanda vyetu vimeanza kuzalisha sukari sasa, tunasubiri kwa hamu kuona bei zikishuka. Walisema hawana soko kwa sababu kuna sukari kutoka nje ya nchi, sasa uwanja ni wao. Sisi wananchi tunadai sukari, na wao waingize sukari sokoni, tena kwa bei ya kizalendo isiyo ya ulanguzi.
Sitanii, kwa miaka yote mimi nimekuwa muumini wa kujenga viwanda vya ndani. Nimesema na hapa narudia, kuwa nchi haiwezi kuendelea kwa kutegemea wawekezaji wa kigeni. Mungu apishie mbali, lakini tukiwa na wawekezaji wazawa, hata ikitokea wakakwepa kodi, hiyo pesa itakuwa bado ipo hapa ndani.
Badala ya kuwa na kampuni kama Tanzania Breweries Limited (TBL), ambayo inahamishia faida yote nje ya nchi kwenda Afrika Kusini, huku ikiwaacha wanahisa wakipiga miayo, ni lazima tuwalinde wawekezaji wa ndani sasa. Serikali iweke mazingira bora ya uwezeshaji.
Kati ya mambo Rais Magufuli aliyonifurahisha na tunayopaswa kuyachukua tukayageuza kama wimbo wa Taifa ni kukataa umaskini. Anasema wazi kuwa Tanzania si nchi maskini. Tunawaendekeza watu wetu kwa kuwaambia miaka nenda rudi kuwa nchi yetu ni maskini.
Sitanii, ni kweli kwamba sina fedha mfukoni, lakini naamini mimi na Watanzania wengi ambao hatuna fedha mfukoni kwa sasa sisi si maskini. Tusipime utajiri wetu kwa fedha za mfukoni, bali uelewa wa mambo, mali tunazomiliki, uhuru tulionao na kubwa zaidi hazina ya fikra.
Ni kwa bahati mbaya watu wengi huishia kuwa maskini kutokana na kutofikiri. Siku wakikosa fedha mfukoni wanaona huo ndiyo mwisho wa dunia. Ukiwauliza wananchi wanasema kilimo hakilipi. Mimi nasema huo ni ufinyu wa mawazo. Mwezi uliopita nimeshuhudia jambo Singida.
Nilikutana na mkulima mmoja, kijana aliyehitimu darasa la saba, lakini tayari amejenga nyumba, amenunua bodaboda na anasomesha watoto wake watatu shule kwa kazi ya kilimo. Kijana huyu anafuga kuku wa kienyeji. Kijana huyu anafuga kuku kati ya 200 na 300.
Kila kuku mmoja anamuuza kwa wastani wa Sh 12,000. Ameniambia kila mwezi anauza wastani wa kuku 60. Anasema anaokota wastani wa mayai 150 kila siku na yai moja la kuku wa kienyeji analiuza Sh 300. Hakuwa na gharama halisi ya chakula anachowalisha kuku hawa.
Hata hivyo, nilijaribu kumdodosa. Akasema kuku wanakula sana. Ananunua pumba karibu debe tano kwa wiki, ambapo kila debe la pumba linamgharimu Sh 6,000. Hii ina maana kwa mwezi wenye wiki nne anatumia pumba za Sh 120,000 na kwa mwezi wenye wiki tano anatumia Sh 150,000.
Baada ya kuwekeza kiasi hicho, anasema huwa kuna dawa za kuzuia minyoo anazowapa kuku zinamgharimu kama Sh 40,000 kwa mwezi. Vijana wawili anaosaidiana nao kutunza kuku hao huwa anawapa angalau mayai 10 kila mmoja kila siku nje ya hayo 150 na mwisho wa mwezi anawalipa Sh 30,000 kila mmoja.
Sitanii, baada ya mazungumzo na kijana huyo, haraka nilikaa chini nikaanza kupiga hesabu. Kijana huyu hanunui vifaranga. Kuku wanatotoa wenyewe. Kiuhalisia kuna siku anaokota hadi mayai 200 anapokuwa na kuku 300. Niliacha hiyo idadi ya mayai 200 nikapiga hesabu ya mayai 150 aliyosema. Nikakuta kwa siku anapata Sh 45,000 sawa na Sh 1,350,000 kwa mwezi.
Nikapiga hesabu wale kuku 60 anaouza kwa wastani wa kuku 2 kila siku, nikakuta kwa Sh 12,000 kila kuku anapta wastani wa Sh 720,000 kwa mwezi. Nikaangalia hao vijana wawili anaowalipa Sh 30,000 kila mmoja kwa maana ya Sh 60,000 kwa mwezi. Mishahara ya vijana hao nikaijumlisha na matumizi ya dawa Sh 40,000 na pumba Sh 150,000 jumla ya matumizi ikawa Sh 250,000.
Ukichukua Sh 720,000 za mauzo ya kuku, ukajumlisha na Sh 1,350,000 za mayai inakuwa Sh 2,070,000. Ukitoa Sh 250,000 za matumizi niliyoonesha hapo juu anabaki na Sh 1,820,000. Hebu fikiri, je, hata wewe unayesoma gazeti hili kama ni mwalimu, askari, mtumishi wa Idara ya Afya, msafisha mitaro barabarani…unaingiza pato hili kwa mwezi? Kumbuka hajazi mafuta kwenye gari au kulipa nauli ya daladala na anapata chakula asilia!
Nimetumia mfano wa kijana huyu kuonesha umaskini wetu unavyotokana na fikra na si ukosefu wa fedha. Sisi waandishi wa habari tuko wachache mno tunaopata hiyo Sh 1,820,000 kwa mwezi. Hata wale wauza baa, ni wachache wanaoipata kama si kujiuza au kuibia wateja.
Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema: ‘Rais Magufuli epuka ushauri huu.’ Nafahamu wakati unaendelea kusoma makala hii hapo juu ulijiuliza uhusiano uliopo kati ya kichwa cha makala na kijana kuuza kuku na mayai. Ulianza kuona kama makala yangu imepotea njia, la hasha.
Mijadala mingi inayoendelea hapa nchini bado watu wana mning’inio wa siasa na uchaguzi uliopita. Nimesema hili na leo nalirudia; uchaguzi umekwisha. Wapo watu sasa wameanzisha lugha ya Rais Magufuli anahujumiwa, na kwenye mijadala ya kitaifa wanapiga kelele mithili ya nguruwe hadi wanatokwa na mapovu wakidai Rais Magufuli anahujumiwa.
Kauli hizi zinaweza kumhamisha Rais Magufuli katika kazi ya msingi ya kujenga uchumi wa viwanda akaanza kutafuta wanaomhujumu na nchi ikapoteza mwelekeo. Serikali ya Awamu ya Nne tulikuwa tunaambiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete anashauriwa vibaya, leo tunaambiwa Rais Magufuli anahujumiwa.
Tena ukisikiliza zinazoitwa hujuma, unabaki mdomo wazi. Mkuu wa wilaya anakwenda kwenye ghala la mfanyabiashara anakuta mifuko 5,000 ya ngano, mifuko 1,000 ya sukari, mifuko 4,000 ya unga wa sembe, chumvi, mafuta ya kula na kadhalika, lakini anatangaza kuwa amenasa sukari iliyokuwa imefichwa.
Sitanii, kwangu hii ni kero kuliko. Ghala ambalo mfanyabiashara miaka yote hulitumia kuhifadhia sukari na bidhaa nyingine eti leo kwa kuwa kuna uhaba wa sukari tukikuta sukari kwenye ghala lake tunasema alikuwa ameficha? Ebo! Tusifike huko.
Tunachopaswa kufanya ni kusimamia sheria. Kama imetangazwa kuwa bei ya sukari ni Sh 1,800 kwa kilo, mapambano yetu tuyaelekeze kwa wanaouza zaidi ya bei hiyo lakini si kwenye maghala. Nawahakikishia, mkiwafungulia kesi hawa wenye maghala ya sukari yakiwa maghala halali, wataishinda Serikali mahakamani mchana kweupe.
Najua, wapo watu wanadhani wakisikika au kuonekana kwenye TV wakisema Rais Magufuli anahujumiwa, basi watateuliwa angalau kwenye cheo fulani familia zao zineemeke. Nasisitiza, huu si wakati wa kutafuta wachawi. Huu ni wakati wa kupambana kwa kubuni mbinu za uwekezaji zitakazozalisha ajira, zikakuza biashara na watu wakapata fedha.
Nilitaraji mijadala mingi katika jamii kwa sasa ingejikita katika kuibua mawazo ya uwekezaji sawa na kijana huyu anayefuga kuku. Wanasiasa wetu walipaswa kuanza kubuni mazao ya kilimo, viwanda vidogo vya misumari, biskuti, pipi, viwanda vya kutengeneza baiskeli, pikipiki, matrekta, vikombe, mashati…
Ni aibu kuona hapo ulipo wewe unayesoma makala hii au hadi nyumbani kwako huna bidhaa hata moja uliyonayo – kuanzia nguo ulizovaa hadi viatu, nguo za ndani, saa, kofia, miwani au chochote kilichoandikwa MADE IN TANZANIA.
Bila kuwa na viwanda hapa nchini tutaimba sana. Rais Magufuli amehoji hao walioendelea wana DNA za aina gani wawe matajiri na sisi tubaki maskini milele? Mimi nasema hapana. Wakati umefika tuzungumze uwekezaji. Dhana ya kuwaona wafanyabiashara kama wezi, walanguzi, wahujumu uchumi zimepitwa na wakati.
Sitanii, Rais Magufuli umeanza vizuri. Dhana yako ya kutumbua majipu imerejesha nidhamu kwa baadhi ya watumishi ingawa bado katika eneo kama hospitali na vituo vya polisi, nidhamu ni sifuri. Unahitaji kujenga mfumo wa kuwezesha Watanzania kiuchumi na urais wako uwe kama wa Rais Benjamin Mkapa. Ukweli na Uwazi.
Kamwe usiendekeze majungu. Hakuna wa kukuhujumu, hawakuwezi. Chapa kazi baba, jenga uchumi usiendekeze siasa za mdumange. Wapo viongozi ambao maisha yao yametegemea umbea miaka yote, hawa watakuwa wa kwanza kukuletea maneno ya kwenye khanga, wakatalie. Kazi ni moja tu, kuondoa umaskini nasi tutakuunga mkono. Mungu ibariki Tanzania.