Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kushauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha Kitengo cha Kuanzisha na Kukuza Biashara. Nimepata mrejesho mkubwa. Nimekuta kumbe vijana wengi wanataka kuanzisha biashara lakini hawafahamu ni wapi pa kuanzia.

Sitanii, nimepata fursa ya kusoma kitabu cha Mfanyabiashara Reginald Mengi cha ‘I Can, I Must, I Will’. Ni vema nichukue fursa hii kumpongeza mzee Mengi kwa kuamua kutumia kitabu chake kuwatia moyo Watanzania wenye nia ya kufanya biashara.

Ameeleza mazingira magumu ya biashara aliyopitia na wanayoyapitia wafanyabiashara Watanzania. Kwa kweli kila alichoeleza mzee Mengi ni cha kweli. Jambo moja amezungumzia – mtaji wa kisiasa.

Ni bahati mbaya kuwa nchi yetu wanasiasa wengi wanamwona kila mfanyabiashara kama mwanasiasa au mpinzani wao wa kisiasa mtarajiwa. Hii inawafanya wanasiasa wanapopata fursa kuziba kila mwanya wa mfanyabiashara kupiga hatua, wakidhani hiyo ndiyo njia pekee ya kujihakikishia nafasi dhidi ya mfanyabiashara.

Mimi sina chembe za ubaguzi wa kijinsia, kikabila, rangi, dini au vinginevyo, lakini katika kumiliki Kampuni ya Jamhuri Media Limited, nimeshuhudia ukweli wenye ladha mbaya. Hadi leo unaposoma makala hii bado wapo watu wasioamini kuwa sisi vijana wa kizalendo, Deodatus Balile na Manyerere Jackton tuliamua kuanzisha Gazeti la JAMHURI.

Hawaamini ukiwaambia tunaye Mkurugenzi mwenzetu kijana mzalendo, Mkinga Mkinga, aliyepata ukurugenzi kutokana na uchapakazi wake uliotukuka katika kampuni hii. Hadi leo bado wapo watu wanatafuta nani mmiliki halali wa kampuni yetu.

Sitanii, nikiwa jeshini nilikuwa kombania moja na kijana wa Kihindi – Ramesh Patel. Kijana huyu ameanzisha biashara nyingi na kubwa hapa nchini, sijawahi kusikia anayemtilia shaka alipata wapi mtaji.

Akienda benki kuomba mkopo anapokewa kama mfalme. Kuna vijana wa Kihindi niliomaliza nao Shahada ya Uzamili ya Biashara (MSc Business Management) nchini Uingereza, hawa wanamiliki biashara kubwa, hawatiliwi shaka umiliki wao.

Wakienda benki kukopa wanapokewa haraka. Nakiri kuwa wimbo unaoimbwa kuwa nchi yetu ni maskini unatokana na fikra finyu za viongozi wetu wengi kuwaza kisiasa katika kila jambo. Ni hadi Rais John Magufuli alipokuja na maelezo kuwa “Tanzania si Nchi Maskini” na inapaswa kuwa taifa la kutoa misaada, kidogo ndiyo tunaona sasa wazawa tunaanza kuthaminika.

Pamoja na kuanzishwa Sera ya Uzawa ya Mwaka 2004, na sheria kutungwa, vitu hivi vimebaki vitabuni. Rais Magufuli na Dk. Philip Mpango mnapaswa kuwa makocha wa biashara katika nchi hii. Zinahitajika juhudi za makusudi kuwafungulia mlango wa mikopo wazawa huko benki.

Tatizo si riba peke yake, bali hata ile kuaminika tu. Prof. Hernando de Soto kutoka Peru, mwaka 2004 alikuja hapa nchini akaeleza jinsi Watanzania walivyo matajiri, lakini wamekalia mitaji mfu. Aliletwa na Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa, akazungumzia mpango wa kurasimisha mali zisizo rasmi.

Sitanii, Prof. De Soto alikuwa akililia mno urasimishaji wa majengo na viwanja kwa nia ya kuviongeza thamani. Namshukuru Rais Magufuli chini ya uongozi wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kazi hii anaifanya kwa kiwango cha kufurahisha.

Makazi ya watu yanarasimishwa sasa, hivyo watu wakipata hati za ardhi itakuwa ni hatua muhimu mno katika safari ya kujikomboa kiuchumi. Asikudanganye mtu. Hauwezi leo ukaanza kukusanya mtaji hadi ufikishe Sh milioni 500 kabla haujazeeka. Lakini unaweza kuingia benki saa 3 asubuhi, kama unayo hati yako kufikia saa 7 mchana ukawa tayari una Sh milioni 500. Kwa kuaminiwa tu, unaweza kuweka hati benki ndani ya siku moja ukawa tajiri.

Sitanii, hiyo ndiyo njia pekee ya kutajirisha wananchi. Wananchi wakipata urahisi wa kukopa mikopo, ikawa na riba ndogo, biashara zikaweza kufanyika na kurejesha mkopo kwa wakati, ajira zinaongezeka, kodi zinazolipwa zitaongezeka na huduma za jamii zitakwenda juu.

Je, unafahamu biashara ndiyo mlango wa nchi yetu kulipa madeni yanayoikabili na kujenga miundombinu ya kisasa? Je, unajua Tanzania ikiwa na wafanyabiashara kama Aliko Dangote watano tu, nchi inaweza kufuta umaskini? Usikose sehemu ya tano ya makala hii wiki ijayo, inayosema ‘Rais Magufuli, Dk. Mpango jengeni wafanyabiashara.’ Mungu ibariki Tanzania.