Aya mbili za mwisho za makala hii wiki iliyopita zilisomeka hivi: “Makala hii itakuwa ndefu kidogo. Leo nimeanza na utangulizi. Wiki ijayo, nitaeleza umuhimu wa kujenga wafanyabiashara wazawa. China ilifanya uamuzi huo mwaka 1979 kwa maelekezo ya Deng Xiaoping. Marekani walifanya uamuzi sawa na huu (alioufanya Rais John Magufuli) mwaka 1776. Uingereza, Japan, Denmark na nchi zote zilizoendelea, hadi serikali inafunga biashara yoyote mhusika anakuwa na tatizo kubwa lisilorekebishika.
“Serikali za nchi zilizoendelea zinafikia hatua ya kutoa ‘ushauri nasaha’ na mbinu za kufanya biashara kwa wafanyabiashara. Hii maana yake ni sawa na mfano wa kuku. Kuku akitaga mayai ukayala yote, hautapata vifaranga. Kuku huyo utabaki naye mmoja huyo huyo na siku akizeeka akafa, kitu kinachoitwa mayai unakisahau. Usikose mwendelezo wa makala hii wiki ijayo.”
Sitanii, makala hii inarejea uamuzi wa Rais John Magufuli na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuipiga marufuku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga biashara ya mfanyabiashara yeyote, isipokuwa wakwepa kodi sugu, ila nao kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA.
Hivi karibuni dunia imeshuhudia mtikisiko kati ya Marekani na China. Nchi hizi mbili zilikuwa zinawekeana vikwazo vya biashara. Marekani chini ya Rais Donald Trump ndio walioanza mchezo huu wa kuweka vikwazo. Rais Xi Jinping akajibu mapigo. Sasa miamba hii miwili imeelewana, wamepeana miezi mitatu kupitia uamuzi wao huu.
Naomba kufafanua kidogo hapa. Si Serikali ya China au Serikali ya Marekani inayofanya biashara kwa kila hali. Biashara zinafanywa na wafanyabiashara. Vikumbo vyote hivyo wanavyopigana wanatetea wafanyabiashara wa nchi zao. Tanzania nasi tunapaswa kufikia hatua hii.
Sitanii, ni bahati mbaya nchi yetu ilianza na mguu mbaya katika kitu kinachoitwa biashara tangu tulipopata uhuru. Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo baadaye ziliungana na kuitwa Tanzania, ziliamini tangu mwanzo kuwa taifa hili ni la wakulima na wafanyakazi.
Kwa mantiki hiyo, wafanyabiashara walionekana kama watu wezi, wahujumu uchumi, wajanja wajanja, watu wasio waaminifu na kadhalika. Ndiyo maana hadi leo baadhi ya mahakama mtu akienda kuomba dhamana, anaambiwa ulete barua ya dhamana ya mtumishi wa umma.
Nilipata kumuuliza hakimu mmoja kwamba katika kitu kuaminika, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni kama Vodacom na Afisa Mtendaji wa Mtaa, nani anaaminika zaidi na mwenye dhamana zaidi katika jamii? Akacheka. Ni ukweli ulio wazi kuwa ukikutana na hakimu mkorofi, anaweza kukataa barua ya dhamana ya CEO wa Vodacom akaikubali ya Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Nkunya, Mtwara!
Sitanii, nchi yetu ilifanya kosa kubwa kutothamini wafanyabiashara. Kwa mfano, hata ndege hizi tulizonunua, reli ya Standard Gauge tunayoijenga, barabara za lami, malori ya mizigo, meli na miundombinu karibu yote tunayoijenga, kwa asilimia 98 tunawajengea wafanyabiashara.
Kwa mfano, mfanyakazi aliyeajiriwa kama mwalimu, daktari, injinia au mwanasiasa kama mbunge, diwani na wengine, hawana mizigo ya kusafirisha. Wafanyakazi husafirisha mizigo yao mara moja tu wanapofikisha miaka 60 wakastaafu utumishi wa umma au kama watahamishwa kituo cha kazi.
Safari za wafanyakazi ni mara moja kwa mwaka wanapokwenda likizo. Kama zipo nyingine za dharura ni za kufiwa au kuhudhuria harusi. Wafanyabiashara ndio wenye kutumia ndege, treni, mabasi, malori… asubuhi na jioni hukimbiza biashara zao. Treni inabeba makontena ya mizigo ya wafanyabiashara ili kuzalisha kodi, si majalada ya wafanyakazi.
Sitanii, mazao ya mkulima baada ya kutoka shambani yanahamia mikononi mwa wafanyabiashara. Wafanyabiashara ndio wanaouza mahindi, mchele kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam, Kahama kwenda Mwanza au Kyela na Iringa kwenda Dar es Salaam, si wakulima.
Kubwa kuliko yote, katika kila hatua anayopita mfanyabiashara, iwe kusafirisha mzigo, kupata leseni, kuwa na ghala, analipa kodi. Kodi ndiyo inayotumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma, huduma za jamii kama maji, barabara, elimu, afya na nyinginezo.
Mtu akiwaangalia wafanyabiashara kwa jicho hili, hapana shaka atabaini kuwa wafanyabiashara ni wadau namba moja katika ustawi wa taifa lolote duniani. Heshima aliyowarejeshea Rais Magufuli na Dk. Mpango, kuzuia wasikimbizwe kama digidigi italipa. Wiki ijayo nitazungumzia umuhimu wa kudai kodi kwa staha. Usikose nakala yako.