Wiki hii naandika makala kwa kusukumwa na kauli za viongozi wakuu wawili wa taifa hili. Hawa si wengine, bali ni Rais John Pombe Magufuli na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango. Rais Magufuli ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuepuka kufunga biashara, badala yake wapokee kidogo wanachopewa kama kodi kinachobaki wakubaliane utaratibu wa kukilipa.

Dk. Mpango yeye amekuja na maagizo rasmi, akawapiga marufuku TRA kufunga biashara ya mtu yeyote, isipokuwa kwa wafanyabiashara wakwepa kodi sugu na hiyo amri itapaswa kutolewa na Kamishna Mkuu wa TRA.

Sitanii, naomba mnisikilize wakubwa. Uamuzi huu mlioufanya milele hamtakaa muujutie. Mmefanya uamuzi sahihi. Kuna watu ndani ya TRA wanafanya watakalo, si kwa masilahi ya uchumi wa taifa hili, bali kwa maslahi binafsi.

Kampuni yetu mwaka jana Desemba, tumeletewa barua yenye kuonyesha kuwa hatujalipa kodi ya PAYE na SDL tangu mwaka 2013. Tena wakabandika uongo mzito wakadai huwa tunachelewesha PAYE na SDL hadi siku 69. Cha ajabu karibu miezi yote tangu mwaka 2013 wanasema kama tulilipa tulichelewesha malipo kwa siku 69 kila mwezi (copy and pest).

Sitanii, hawakufahamu kuwa tangu tulipoanzisha kampuni hii tulikuwa makini kuliko maelezo katika masuala ya kulipa kodi. Ni sera ya kampuni yetu kuwa kama hatuna kodi inapofika siku ya 6 ya mwezi unaofuata, kwani sheria inataka uwe umeilipa si zaidi ya tarehe 7 ya mwezi unaofuata, huwa tunakwenda kwa mtu tunakopa tunalipa kodi, tukipata hela tunamrejeshea aliyetukopesha.

Ofisi ya Kodi Ilala ilituletea madai ya Sh milioni 72, tena wakataka tulipe ndani ya siku 7, vinginevyo tukatishiwa kufungiwa biashara. Kwa kuwa kumbukumbu zote tulikuwa nazo ilituchukua chini ya saa tatu, kurudufisha risiti zote tulizolipa kodi, tena tukajikuta Agosti, 2017 tulilipa kodi mara mbili.

Kwa mkono wangu nikaandika barua na kuweka nakala ya hizo risiti za malipo tena yenye mihuri ya TRA. Kwa masikitiko makubwa, Afisa wa TRA aliyepokea majibu yetu akamwambia mtu wetu wa fedha kuwa ataaminije kama hatukughushi muhuri wa TRA. Hii ilinikera sana. Nikawasiliana na aliyekuwa Meneja wao, akanitaka nimpe nakala ya maelezo yangu, nikafanya hivyo.

Sitanii, hadi Desemba imeisha sijasikia lolote kutoka TRA Ilala. Siku tunapeleka majibu, tulikuta watu wengi wenye malalamiko sawa na ya kwetu. Nikajiuliza sisi kama tumelipa bila kuacha hata senti moja, bado tunabambikiwa hivi, inakuwaje mtu asiyetunza kumbukumbu zake vyema?

Kimsingi niseme tuliamua kutunza kumbukumbu zote za kodi kwa kufahamu kuwa tunafanya habari za uchunguzi na kodi imekuwa ikitumiwa na watu mbalimbali katika nchi mbalimbali kunyamazisha vyombo vya habari. Kama yupo mtu au taasisi iliyotaka kutunyamazisha kwa kutumia kodi, jaribio hili limeshindwa.

Makala hii itakuwa ndefu kidogo. Leo nimeanza na utangulizi. Wiki ijayo nitaeleza umuhimu wa kujenga wafanyabiashara wazawa. China ilifanya uamuzi huo mwaka 1979 kwa maelekezo ya Deng Xiaoping. Marekani walifanya uamuzi sawa na huu alioufanya Rais Magufuli mwaka 1776. Uingereza, Japan, Denmark na nchi zote zilizoendelea, hadi serikali inafunga biashara yoyote mhusika anakuwa na tatizo kubwa lisilorekebishika.

Serikali za nchi zilizoendelea zinafikia hatua ya kutoa “ushauri nasaha” na mbinu za kufanya biashara kwa wafanyabiashara. Hii maana yake ni sawa na mfano wa kuku. Kuku akitaga mayai ukayala yote, hutapata vifaranga. Kuku huyo utabaki naye mmoja huyo huyo na siku akizeeka akafa, kitu kinachoitwa mayai unakisahau. Usikose mwendelezo wa makala hii wiki ijayo.